Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa
ASKOFU Msaidizi wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa amesema wafanyabishara wanaoficha sukari nchini, wanafanya dhuluma kwa kutumia uwezo wao kuwanyanyasa wanyonge na ameishauri Serikali kutowafumbia macho watu hao.
Aidha, ameshauri serikali kuwasikiliza na kuchunguza kwa kina na uadilifu maelezo ya wafanyabiashara waliokamatwa na bidhaa hiyo kabla ya kuwachukulia hatua ili kutenda haki.

Wakati Nzigirwa akisema na kushauri kuhusu suala hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ametoa saa 24 kwa ghala la kampuni ya Mohammed Enterprises (MeTL) la Kiwalani kupeleka nyaraka katika mamlaka zinazohusika, kubaini kama kweli sukari tani 5,800 iliyokutwa jana katika ghala hilo ni bora kwa matumizi ya wananchi.
Sukari hiyo ambayo ni ya viwandani (nyeupe) imezuiliwa kutumika hadi hapo wahusika watakapokamilisha kupeleka vielelezo vyote katika mamlaka hizo na kufanyika kwa uchunguzi. Sukari hiyo tani 5,800 ni tofauti na sukari mifuko 160 ya ujazo wa kilo 25 iliyokamatwa juzi katika msako kwenye nyumba inayomilikiwa na Bashiru Ismail jijini humo.
Askofu Nzigilwa akijibu swali la waandishi kuhusu suala la sukari nchini baada ya mahafali ya Nane ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph (SJUIT) yaliofanyika jijini humo jana, alisema kama wapo kweli wanaoficha sukari, wanafanya dhuluma dhidi ya wanyonge.
Alisema wafanyabiashara wanaoficha sukari kwa manufaa yao binafsi wanafanya jambo la kusikitisha kwa kuwa haitegemewi kwa mtu kama mfanyabiashara kuficha bidhaa hiyo inayotegemewa na wananchi wengi. Alisema watu wanaotumia uwezo wao kuficha sukari ni sawa na kuwadhulumu wananchi wengine, ambao wanahitaji bidhaa hiyo.
Aliongeza kuwa hatua ya kuficha sukari, inatokana na watu kutokuwa na maadili mema ya dini, kwani kama wangekuwa na maadili mazuri wangekuwa na hofu ya Mungu hivyo wasingeficha sukari na kusababisha bidhaa hiyo kuadimika.
Nzigilwa alishauri wafanyabiashara wanaokamatwa kwa tuhuma hizo na kutoa maelezo yao, Serikali inapaswa kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini ukweli kama wameficha au lah.
“Hili suala lipo kisheria, waliokamatwa wamekuwa wakitoa maelezo kuhusu sukari yao, lakini nafikiri uchunguzi wa kina ufanyike ili kubaini ukweli kama hizo sukari zilifichwa au ni sawa na maelezo yanayotolewa na wamiliki wake,” alisema Askofu Nzigilwa.
Alisema anaamini uchunguzi wa vyombo vya Serikali, utafanyika kwa makini na kwa haki kubaini ukweli.
Makonda
Akiwa Kiwalani jana, Makonda ametoa saa 24 kwa kiwanda cha MeTL cha eneo hilo kupeleka nyaraka katika mamlaka husika kuthibitisha kama sukari 5,800 iliyokutwa katika kiwanda hicho inafaa kwa matumizi ya binadamu.
Akizungumza wakati alipofanya ziara ya kushtukiza katika ghala hilo, Makonda alisema ameamua kuzuia sukari hiyo baada ya kukuta inafungashwa kwa matumizi ya kawaida ilihali ililetwa kwa ajili ya matumizi ya viwanda.
Aliitaka Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), kuchunguza sukari hiyo kama ni bora kwa matumizi na kuangalia kama kibali cha mamlaka hiyo cha kubadili sukari hiyo kuwa ya matumizi ya kawaida walichokionesha kama ni cha kweli.
“Kama kweli wana mfumo wa kubadilisha sukari hii kuwa ni ya matumizi ya kawaida wangekuwa tayari wamebadilisha kutokana na hali hii ya ukosefu wa sukari wanayopata wananchi kwa hali hii mtu huyu anaingia kwenye kipengele cha wale wanaoficha sukari,” alisema Makonda.
Alitaka TFDA, TBS na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuwa weledi, pale wanapofanya kazi zao katika viwanda mbalimbali, kwani inaonekana watumishi wengine si waaminifu wamekuwa wakichukua fedha na kuacha kutenda haki.
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi wa kampuni ya MeTL, Gulam Dewji, jana alikanusha kuwa sukari tani 2,990 zilizokamatwa juzi na kuelezwa na baadhi ya vyombo vya habari (si HabariLeo) kuwa ni mali ya kampuni hiyo si kweli, bali ni ya kampuni ya Commodities Trading Company Ltd.
Dewji alisema kuwa utoaji wa taarifa hiyo, ambao haukuzingatia ukweli, unachochea hasira za wananchi katika kipindi hiki kigumu cha kupungua kwa sukari ya majumbani katika soko la nchini.
Taarifa za kukamatwa kwa sukari hiyo zilitolewa juzi na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda na kwa mujibu wa vyombo vya habari, sukari hiyo yenye thamani ya Sh bilioni 5.4 ilikutwa ikiwa imehifadhiwa kwenye makontena 155.
Dewji alisema MeTL Group pamoja na kuwa kampuni ya biashara kimataifa ikiuza bidhaa za kilimo na kununua, pia inajishughulisha na utengenezaji wa bidhaa ambazo zinahitaji sukari ya kiwandani.
“Tunapoagiza sukari ama kwa mahitaji ya kiwanda yetu, kampuni ya MeTL hufuata taratibu zote za nchi,” alisema Dewji kupitia taarifa yake kwa vyombo ya habari iliyosambazwa jana. Sukari tani 2,990 zilizokutwa Bandari Kavu (ICD) ya PMM ya Vingunguti jijini Dar es Salaam ni mali ya kampuni ya Tanzania Commodies Trading Company Ltd.
Akielezea kuhusu sukari hiyo, Mutarza Dewji ambaye ndiye mmiliki wa kampuni hiyo, alisema sukari hiyo ilikuwa njiani kuelekea Uganda, lakini kutokana na uhaba wa sukari hapa nchini, Serikali iliruhusu mzigo huo kubaki nchini ili kuingiza sokoni mara moja kati ya jana ama leo.