Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameagiza wakuu wa mikoa ya Geita, Arusha na Kagera kuhakikisha wanaondoa mifugo itokayo nje ya nchi pamoja na kuwaondoa wanachi waliovamia maeneo ya hifadhi za taifa (Tanapa) ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Aidha ameagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kuhakikisha wanatenga maeneo maalumu kwa ajili ya mifugo inayotolewa ndani ya hifadhi na kupunguza mgogoro kwa wananchi wengine.

Samia alitoa maagizo hayo jana jijini hapa, wakati alipokuwa akikabidhi hundi ya thamani ya Sh bilioni moja kwa wakuu wa mikoa 19 inayozunguka hifadhi za taifa (Tanapa) kwa ajili ya kununua madawati. Alisema, wakuu wa mikoa wakizembea kutekeleza uondoaji mifugo ndani ya hifadhi za taifa serikali itawawajibisha.
Alisema waliohifadhi mifugo ndani ya hifadhi hiyo waondoke na mifugo yao hadi Juni 30 mwaka huu kwani mkoa wa Kagera una ng’ombe milioni mbili wanaotoka nje ya nchi, na mikoa ya Arusha na Geita ina ng’ombe milioni tatu kutoka nje ya nchi.
Akizungumzia kuhusu kukabidhi madawati 16,500 katika wilaya zote 55 zilizopo kwenye mikoa 19 nchini, Samia aliipongeza Tanapa kwa kusaidia elimu nchini kwani baada ya serikali ilipotangaza kuwa elimu bure wanafunzi wengi wamejitokeza huku kukiwa na changamoto ya madawati Samia alisema, kutokana na msaada huo wanafunzi wataondokana na adha ya kukaa chini na kuumia migongo kwani kila wilaya itapata madawati 300 huku wanafunzi 49,500 wakiwa wanakaa kwenye madawati na kuongeza usikivu zaidi.
Naye Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema Tanapa wanatambua mchango wa elimu ndio maana wametoa msaada huo kwa mikoa 19 inayopakana na hifadhi za taifa.
Mkurugenzi wa Tanapa, Allan Kijazi alisema Tanapa itaendelea kushirikiana na serikali katika sekta ya elimu kwa lengo la kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwa bidii pamoja na kujua jinsi ya kuhifadhi maliasili za Taifa.
Akitoa salamu za shukrani kwa Makamu wa Rais, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Meck Sadiki aliishukuru Tanapa kwa kutoa madawati kwa wakuu wa mikoa na kusema kuwa, mkoa wa Kilimanjaro umepiga marufuku usafirishaji wanyama pori kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) kuanzia jana.