Sehemu ya Jiji la Dar es Salaam
SERIKALI imesema inakamilisha taratibu za kuanzisha mfumo wa ulinzi wa raia na mali zao kwa njia ya mtandao wa kamera za usalama, ikianza na Mkoa wa Dar es Salaam kwa mwaka ujao wa fedha.
Aidha, itakamilisha taratibu za kuanzisha ukaguzi wa lazima wa magari yote nchini pamoja na taratibu za ufuatiliaji wa magari yaendayo mikoani kwa njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama).

Sambamba na hilo, katika kusaidia kudhibiti ajali za barabarani, Jeshi la Polisi lina mpango wa matumizi ya mfumo wa pointi na ufungaji wa kamera za kudumu za barabarani.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana wakati akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Kitwanga alisema ufungaji wa kamera za usalama (CCTV) utaanzia katika Mkoa wa Dar es Salaam katika mwaka ujao wa fedha na kisha kuhamia mikoa mingine nchini. Alisema katika mwaka huo, polisi itaanza rasmi kutekeleza Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni kama sehemu ya kuboresha utendaji na kuimarisha usalama wa nchi.
“Inatarajiwa kuwa mpango huu utatekelezwa nchi nzima baada ya kubaini changamoto zitakazotokana na utekelezaji huo katika Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni,” alisema Kitwanga.
Kuhusu kukabiliana na ajali, alisema ukaguzi wa lazima wa magari yote nchini pamoja na ufuatiliaji wa magari ya mikoani kwa Tehama, utasaidia kupunguza ajali za barabarani pamoja na kuondoa magari chakavu ili kuweka mazingira salama.
Pia alisema mifumo mipya ya udhibiti wa makosa ya usalama barabarani ikiwemo tozo za papo kwa papo kwa kutumia mashine za kielektroniki umeweza kusaidia kupunguza ajali za barabarani. Aidha, alibainisha kuwa kuna upungufu wa ajali za barabarani kwa asilimia 13 kati ya mwaka 2014/15 na Julai 2015 hadi Machi mwaka huu.
Alisema katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 jumla ya ajali za barabarani 6,984 zilitokea katika maeneo mbalimbali na watu 2,577 walipoteza maisha na wengine 7,503 walijeruhiwa.
Alisema katika kipindi kama hicho mwaka 2014/15 zilitokea ajali 8,072 na kusababisha vifo vya watu 2,883 na majeruhi 9,370.
“Upungufu huu wa ajali ni sawa na asilimia 13. Ajali hizi zimeendelea kuleta madhara makubwa kwa wananchi kwani idadi ya majeruhi na vifo bado ni kubwa,” alieleza Waziri Kitwanga.
Akizungumzia hali ya uhalifu na makosa ya jinai, Kitwanga alisema kimsingi hali ya usalama nchini ilikuwa ya kuridhisha, kwa mujibu wa takwimu.
Alisema katika kipindi cha Julai, 2015 hadi Machi, 2016 jumla ya makosa makubwa 53,201 yaliripotiwa katika vituo vya Polisi kote nchini ikilinganishwa na makosa 47,942 yaliyoripotiwa katika kipindi kama hicho mwaka 2014/15 ikiwa ni ongezeko la makosa 5,259 sawa na asilimia 11.
“Ongezeko la makosa haya yaliyoripotiwa limetokana na kusogezwa kwa huduma za kipolisi hadi ngazi ya Kata/Shehia na kuongezeka kwa elimu ya Usalama wa Raia kwa wananchi ambao wameelewa umuhimu wa kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya dola,” alisema Kitwanga.
Aidha, alisema matukio ya uvamizi wa vituo vya polisi yamepungua kutoka manane mwaka 2014/15 hadi kufikia matukio sita mwaka 2015/16 ambayo askari wanne na raia mmoja waliuawa na silaha 22 na risasi 273 ziliporwa.
Alisema Jeshi la Polisi limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 17 waliohusika na uvamizi wa vituo vya Polisi na kupata silaha zote zilizoporwa katika vituo vya Stakishari, Tanga na Ikwiriri.