Waziri wa Habari, Vijana na Michezo Nape Nnauye.
SERIKALI imesema ipo tayari kuyafanyia kazi malalamiko yaliyotolewa na wadau wa habari juu ya Muswada wa Sheria ya Haki ya Kupata Habari na kuhakikisha kuwa sheria hiyo inakuwa tayari mwaka ujao wa fedha.
Aidha, serikali imetaka wadau wa vyombo vya habari kuunda kamati ambayo itapitia malalamiko juu ya kuonesha mijadala ya Bunge moja kwa moja na kutafutia ufumbuzi. Akizungumza wakati wa kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Dunia jijini Mwanza jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alisema timu itakayoundwa, itatakiwa kwenda kutembelea studio za Bunge na kujionea zinavyofanya kazi.

Alisema serikali haifurahii kwa namna ambavyo inalalamikiwa na wadau mbalimbali juu ya agizo hilo la kurusha matangazo ya Bunge yaliyorekodiwa na kusema kuwa haina mkono wake katika agizo hilo.
“Maamuzi ya kuwa na matangazo ya Bunge yanayoendelea hivi sasa si ya serikali bali ni ya Bunge lenyewe, kwani ni mhimili unaojitegemea, lakini ni bahati mbaya azimio hilo limeleta mkanganyiko miongoni mwa wadau,” alisema Nape.
Nape alisema anaamini kamati itakayoundwa kufuatilia na kutafuta ufumbuzi wa sakata hilo itakuja na ufumbuzi na kumaliza tofauti zilizopo. Hata hivyo, alisema Tanzania inatakiwa kuwa na utaratibu wa urushaji wake wa matangazo ya Bunge kama ilivyo kwa nchi nyingine na kinachofanyika ni mazoea tu ya uhuru wa kupata habari.
Alisema serikali daima inahakikisha kunakuwepo na uhuru wa kujieleza na kupata habari na ndio maana ipo tayari kupitia upya Sheria ya Makosa ya Mitandao na Sheria ya Takwimu ili ziwe rafiki zaidi.
Kwa upande wake, mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohammed Chande Othman alisema wakati ikipigania uhuru wake, vyombo vya habari vinapaswa kwa karibu kuangalia mchango wake katika kukuza utawala wa sheria na utawala bora.
Jaji Chande aliyewakilishwa na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Ziwa, Robert Makaramba alisema watendaji wa vyombo vya habari, wanatakiwa kuzingatia elimu, na kukabiliana na changamoto huku wamiliki wa vyombo vya habari nchini wakiweka mazingira mazuri na kuwajengea uwezo watumishi wao.
Mwakilishi Mkazi wa Umoja wa Mataifa, Alvaro Rodriguez na Naibu Mkuu wa Umoja wa Nchi za Ulaya nchini, Luana Reale walisema wao kwa pamoja wana nia ya kuendeleza na kuunga mkono uhuru wa maoni na kujieleza wa haki za msingi za binadamu.
Mwenyekiti wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari (MOAT), Reginald Mengi alisema kuwa baadhi ya vyombo vya habari haviwezi epuka tuhuma za rushwa lakini kufuata maadili ni jambo la muhimu.
Wakati huo huo, Kituo cha Kisheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimetoa mwito kwa serikali kuruhusu vyombo vya habari kutekeleza majukumu yao kwa uhuru bila kuingiliwa. Katika taarifa yake iliyotolewa jijini Dar es Salaam, LHRC imeikumbusha serikali kushirikisha vyombo vya habari na mashirika yasiyo ya kiserikali kufanya tafiti na kutoa taarifa ambazo zitasaidia kuongeza uwajibikaji.