|
KAMATI Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) imepitisha majina ya wabunge 21 walioomba nafasi ya ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya chama hicho.
Msemaji Mkuu wa CCM, Christopher Ole Sendeka alisema Kamati Kuu ilifanya maamuzi hayo kupitia kikao chake kilichofanyika jana, Ikulu ya Chamwino Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma chini ya Mwenyekiti wake, Jakaya Kikwete na kuhudhuriwa pia na Rais John Magufuli.
Pamoja na kupitishwa kwa majina hayo, Kamati Kuu imewataka wagombea wote kufuata sheria na taratibu za chama na kwamba atakayekiuka, atachukuliwa hatua za kinidhamu, ikiwa ni pamoja na kuenguliwa kwa jina lake katika nafasi za wagombea.
Waliopitishwa kuwania nafasi 10 za NEC kutoka Bunge la Tanzania kwa CCM ni Munde Tambwe, Jamal Kassim Ali, Faida Mohamed Bakari, Mbaraka Dau, Alex Gashaza, Hawa Ghasia, Ibrahim Hassanali Raza, Angela Kairuki, Dk Hamis Kingwangalla, Profesa Norman King, Livingstone Lusinde na Angelina Mabula.
Wengine ni Almasi Maige, Angelina Malembeka, Agness Marwa, Yahaya Massare, Steven Ngonyani ‘Maji Marefu,’ Stanslaus Nyongo, Mattar Ali Salum, Peter Serukamba na Hafidh Ali Tahir. Pia Kamati Kuu imepitisha majina 19 ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, walioomba kugombea nafasi ya ujumbe wa NEC kupitia Baraza la Wawakilishi Zanzibar.
Waliopitishwa ni Nassoro Salim Ally, Ally Hamisi Bakari, Salma Mussa Bilal, Mgeni Hassan Juma, Riziki Pemba Juma, Yussuph Hassan Idd, Khadija Omary Kibano, Shamata Shaame Khamisi, Mmanga Mjawiri na Dk Khalid Salum Mohamed. Pia wamo Aska Abdallah Mussa, Mihayo Juma N’hunga, Zulfa Mmaka Omar, Hamad Abdallah Rashid, Mohamed Ahmada Salum, Harusi Saidi Suleiman, Haroun Ali Suleiman, Issa Haji Ussi na Bahati Khamisi Kombo.
Aidha, Sendeka alisema kuwa Kamati Kuu pia imepitisha majina ya wabunge wa CCM wanne, walioomba nafasi ya Katibu wa Kamati ya Wabunge wote wa CCM. Waliopitishwa ni Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza, Mbunge wa Korogwe Mjini, Mary Chatanda, Mbunge wa Viti Maalumu, Mariam Kisangi na Mbunge wa Mkuranga, Abdallah Ulega.
Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Mbunge wa Peramiho na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama. Katibu wa wabunge huingia moja kwa moja katika Kamati Kuu. Pia imepitisha majina matatu ya wajumbe wa Baraza la Wawakilishi walioomba nafasi ya Katibu wa Kamati ya Wajumbe wa Baraza hilo kupitia CCM.
Hao ni Ali Suleiman Ali (Shihata), Ali Salum Haji na Abdallah Ali Kombo. Msemaji huyo wa CCM alieleza kuwa Kamati Kuu pia imepitisha majina ya wana CCM walioomba nafasi wazi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ya Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma ambayo wamepitishwa Josephat Ntambindi, Gilbert Kagoma na Malck Rudugu. Kwa nafasi ya Mjumbe wa NEC Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, waliopitishwa ni Omar Kigoda, Maajabu Hamis, Mussa Kidato, Hamisi Mnondwa na Athuman Lukoya.
Aidha, nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Mkoa wa Mbeya, Sendeka aliwataja waliopitishwa kugombea ni Charles Mwakipesile, James Mwasunga na Stephen Mwakajumulo. Kwa nafasi ya Katibu wa Uchumi na Fedha, Mkoa wa Njombe waliopitishwa ni Creiton Lulambo, Salu Sanga na Erick Nyagawa. Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imempongeza Dk Ali Mohamed Shein kwa kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar kwa kura nyingi katika uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20, mwaka huu.
Aidha, Kamati Kuu imewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kuendelea kukiamini Chama Cha Mapinduzi kwa kukipa ushindi wa kishindo katika nafasi ya Rais, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani.
Wakati huo huo, Msemaji wa CCM, Christopher Ole Sendeka amesema chama hicho kiko katika hatua za mwisho za makabidhiano ya nafasi ya Uenyekiti wa Taifa kati ya Mwenyekiti wa sasa, Jakaya Kikwete na Rais John Magufuli.
Akizungumza jana wakati wa mkutano wake na waandishi wa habari, Sendeka alisema suala la kukabidhiana mikoba kati ya Kikwete na Rais Magufuli kwa mujibu wa uzoefu wa CCM anayechaguliwa kuwa Rais kwa tiketi ya chama hicho ndiye anayepokea nafasi ya uenyekiti wa CCM.
“Bahati nzuri hawa wakubwa walikuwa wameshauriana kwamba Uenyekiti ni miaka mitano, Dk Kikwete angeweza kuendelea kuwa mwenyekiti, lakini uzoefu wa kupokezana vijiti na uongozi tangu wakati wa Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na sasa ni Kikwete unaonesha kwamba umekuwa ukifanyika mwaka unaofuata baada ya uchaguzi kwenye mwezi Juni,” alieleza Sendeka.
“Sisi mwaka huu wakubwa hawa walishashauriana Kikwete alishatangaza wazi kwamba anakusudia kumkabidhi nafasi ya uenyekiti Rais wa sasa, Dk Magufuli wakati wowote mwaka huu na kinachofanyika sasa ni maandalizi tarehe na mwezi ambao Mkutano Mkuu utafanyika tutawaarifu lakini tumekubadiliana tupo kwenye mchakato wa Mkutano Mkuu Maalumu ili Kikwete aweze kukabidhi uenyekiti kwa Magufuli.”
Alisema nafasi ya Mwenyekiti wa chama kikubwa kama CCM inapotokea mamlaka ya Rais ipo kwa mtu mwingine inaweza kuleta mkanganyiko wa kudhoofisha lengo la mtu aliyekabidhiwa nchi ya kuyafanya. “Ni mazoea na utamaduni wetu wa CCM kwamba wana CCM mwingine ataweza kujitokeza kugombea hazuiwi Katiba ipo kanuni zipo ataelekezwa,” alisema Sendeka.
0 Comments