Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.
WABUNGE wameitaka serikali kuweka mkazo katika kuhakikisha ardhi yote nchini inapimwa. Pia, wametaka kuwepo na programu ya kupima ardhi nchi nzima na kuwauzia wananchi, jambo litakalosaidia kuondoa migogoro ya ardhi.
Wametaka suala la upimaji kutoachwa kwa sekta binafsi, ambayo kwa mujibu wa wabunge, ina gharama kubwa; badala yake, serikali ijiwekee mkakati wa kupima angalau mikoa miwili kila mwaka.

Aidha, wabunge wameyashukia mabaraza ya ardhi huku wakikosoa kutumia watu wasio na taaluma ya sheria katika kuamua kesi. Walitoa maoni hayo jana wakati wakichangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Walisisitiza umuhimu wananchi kupimiwa ardhi na kupatiwa hati. Walia upimaji ardhi Mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda (CCM), alisema kuwe na programu maalumu ambayo serikali itakuwa na vifaa vya upimaji nchi nzima na kupima ardhi yote ; na pale mwananchi anaponunua ardhi anakuta eneo limepangwa.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa usumbufu wa kupima kwa gharama kubwa na wakati huo huo kukabili migogoro ya ardhi. Alitoa mfano wa Jiji la Dar es Salaam, ambalo serikali inakabiliwa na usumbufu wa kulipanga.
Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Omary Mgumba (CCM) aliunga mkono umuhimu wa kupima maeneo yote, kuondoa utata na kumaliza migogoro ya ardhi. Mwingine aliyehimiza upimaji wa maeneo yote ni Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso (Chadema ) ambaye alishauri wananchi wapimiwe maeneo kwa kuwakopesha kisha walipe madeni hayo taratibu.
Alisema kwa kufanya hivyo serikali mbali na kuondoa migogoro ya ardhi, pia itaingiza kipato kutokana na wananchi kulipia hati. Wakosoa mabaraza Wakati huo huo katika kuchangia, baadhi ya wabunge wametaka kazi za kiutendaji katika masuala ya ardhi zifanywe na wataalamu wa ardhi ; na serikali iachane na utaratibu wa sasa wa kuwapa kazi watu kiholela.
Walitaka mabaraza ya ardhi yasimamiwe na wataalamu wa ardhi, badala ya kuchukua watu wasio na taaluma. Mbunge wa Manyoni Mashariki, Daniel Mtuka (CCM), alieleza kushangazwa na kitendo cha serikali kukabidhi jukumu kubwa la usuluhishi wa masuala ya ardhi kwa watu ambao hawajasoma na hawajui sheria za ardhi.
Alisema, wapo wataalamu wengi nchini ambao wamekwenda kusomea masuala ya ardhi wanaotakiwa kufanya kazi hiyo, lakini wamekuwa wakitumiwa watu maarufu vijijini kufanya kazi hiyo.