Maafisa wa misitu nchini India wamewakamata na kuwafungia simba 13 wa bara Asia, magharibi mwa India baada ya watu watatu kuuawa.
Simba hao walizungukwa na kukamatwa baada ya kijana mmoja kutolewa katika kijiji chake, kuuawa na kuliwa kiasi.

Watu wengine wawili waliuawa katika kipindi cha miezi miwili ijapokuwa maafisa wanasema kuwa mashambulio kama hayo huwa nadra.
Simba hao wa Asia wanaoorodheshwa kuwa hatari ni miongoni mwa simba 500 wanaoishi katika msitu wa Gir mjini Gujarat.
Afisa mkuu wa uhifadhi wa wanyama pori katika mji huo J A Khan,alisema simba hao walikamatwa katika eneo moja la mashariki mwa eneo hilo la uhifadhi wa wanyama pori.
''Simba ambao wanawawinda binaadamu watakamatwa na kuchunguzwa huku waliosalia wakirudishwa msituni'',alisema bw Khan