WAKUNGA wanaokiuka maadili ya kazi ikiwemo kuwatolea wajawazito maneno ya kashfa na kejeli, wametangaziwa ‘kiama’ baada ya serikali kuagiza Baraza la Wakunga kuhakikisha wanaobainika, wanafutiwa leseni.
Aidha, serikali imeamua kuanzia mwaka ujao wa fedha, halmashauri zote zitapaswa kuorodhesha idadi ya watakaopoteza maisha wakati wa kujifungua sanjari na sababu za vifo na kama upo uzembe, ifahamike mtu wa kumwajibisha.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo jana kwenye maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani yaliyofanyika jijini Dar es Salaam. Alisema ingawa wapo wakunga wengi wazuri na waadilifu, wapo wachache wasio waadilifu ambao amesisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli haitawavumilia.
“Ukweli ni kuwa wakunga wengi ni wazuri na waadilifu, kwani wanafanya kazi katika mazingira yenye changamoto nyingi. Lakini wapo wachache ambao siyo waadilifu, … wakumbusheni wanachama wenu maadili ya kazi zao mara kwa mara, ” alisisitizia Baraza la Wakunga.
Katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya ‘Wanawake na watoto mhimili wa wakunga’, Waziri alisema ili kuwawajibisha wakunga wenye tabia hizo, ni vyema wananchi wanaofanyiwa ukatili kuwataja wahusika moja kwa moja badala ya kuunganisha wakunga wote kwenye kituo husika.
Alisema katika masomo ya ukunga, wanataaluma hao wanafundishwa jinsi ya kuhudumia mjamzito. “Anayeona hawezi kazi hiyo ni vyema kuacha na kutafuta kazi nyingine,” alisema.
Alisema serikali haitamwonea huruma yeyote atakayesababisha vifo kwa wajawazito. Alisema watapitia halmashauri zote kuangalia zilivyotenga bajeti kwa ajili ya kukabili vifo hivyo.
Alifafanua kuwa pamoja na wakunga kukabiliwa na mzigo mzito wa kufanya kazi katika mazingira magumu ya ukosefu wa vitendea kazi, kuhudumia wajawazito wengi kuliko viwango vinavyotakiwa, hiyo si sababu ya kufanya vitendo hivyo vya ukatili kwa wajawazito.
Waziri alikiri wanataaluma hao kukabiliwa na changamoto kwa kusema, kwa sasa mkunga mmoja anahudumia wajawazito kati ya 10 na 80 wakati viwango vya kawaida inapaswa mkunga mmoja kuhudumia mjamzito mmoja hadi sita.
Hata hivyo alisema, kuanzia mwaka ujao wa fedha, serikali itaongeza idadi ya wanafunzi wanaojiunga kusomea masuala ya ukunga ikiwa ni pamoja na kuongeza ajira kwa wakunga serikalini.
Marekebisho elimu ya ukunga
Akizungumzia ubora wa elimu kwa wakunga, alisema wameanza kufanyia marekebisho kwani baadhi ya mambo yanatokea kutokana na kutoa elimu kwa muda mfupi wa miaka miwili tofauti na ilivyokuwa awali miaka minne.
“Hivyo tumeanza kuboresha utoaji wa elimu kwa kushirikiana na Baraza la Wakunga na tayari imefika Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (NACTE) ambapo majadiliano yanaendelea na watakapokamilisha, suala la mishahara nalo litaangaliwa kwa watakaosoma miaka mingi tofauti na sasa,” alisema.
Awali Mkurugenzi wa Chama cha Wakunga Tanzania (Tama), Feddy Mwanga alisema kwa sasa wana matawi 23 na wanachama 4,000 . Alisema serikali itakapowekeza kwa wakunga kwa kuwapa utaalamu wa stadi zote zinazotakiwa watapunguza vifo vya wanaojifungua kwa asilimia 70.
Alisema mkunga akipata utaalamu huo ana uwezo wa kumhudumia mjamzito kwa asilimia 87 na zinazobaki ni kwa wachache wanaotakiwa kufanyiwa upasuaji.
“Hivyo tunaona ni vyema kuangalia upya elimu ya uuguzi na ukunga iliyopunguzwa kutoka miaka minne hadi miwili kwani muda hautoshi kumtengeneza mkunga ipasavyo,”alisisitiza.
Alisema Tama inasikitishwa na tabia ya wakunga wachache wanaokiuka maadili kwa kutoa huduma isiyostahili. Alisema wataendelea kuwachukulia hatua watakaobainika.
Hata hivyo, akizungumzia changamoto mbalimbali zinazowakabili ikiwemo lawama na tuhuma kwa wakunga, alisema wakati mwingine hutokana na uelewa mdogo wa huduma za afya ya uzazi.
Alitoa mfano wa tukio la hivi karibuni lililoripotiwa kwenye baadhi ya vyombo vya habari; ambalo mjamzito alilalamika kutupiwa mtoto kifuani baada ya kujifungua, alisema haikuwa unyanyasaji bali ni suala la kitaalamu.
“Tunaomba wananchi watutie moyo kwa kazi nzito tunayofanya na wasitupige pale kunapotokea tatizo kwani wakati mwingine ni kutokana na uelewa wa kazi yetu kama ilivyokuwa kwa mama aliyewekwa mtoto kifuani,” alisema.
Alikiri kwamba bado hawajaelimisha kuhusu suala hilo la kuweka kifuani mtoto anayezaliwa kwa ajili ya kumpatia joto jambo ambalo lilitafsiriwa na mama huyo kuwa ni unyanyasaji