|
MBUNGE wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) ametolewa nje ya Bunge baada ya kutaka kumkwida Mbunge wa Kasulu Vijijini, Agustine Holle (CCM) aliyedai kuwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika wote wa Chadema kuwa wanaugua kichaa.
Waitara alionesha kukerwa na kauli hiyo hasa pale Holle alipokataa kufuta kauli yake, licha ya kutakiwa kufanya hivyo na Naibu Spika, Dk Tulia Akson.
Wakati Holle akichangia, Waitara alinyanyuka kwenye kiti chake na alipofika alipo mbunge huyo alimzungumzisha maneno ambayo hayakusikika na kuonesha kama kutaka kumpiga kabla ya kukaa kwenye kiti kilicho mbele yake ndipo, Holle alisikika akisema “wewe unataka nini” ndipo Naibu Spika alipogundua kuwa Waitara anataka kumpiga Holle na kumuamuru atoke nje lakini hakutii amri hiyo.
Kutokana na kutotii, Naibu Spika aliamuru askari wamtoe ndipo walipoingia zaidi ya askari watano na kutoka naye hadi nje ya geti kubwa la kuingilia bungeni.
Holle wakati anachangia bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka wa fedha 2016/2017, alimtaja Lissu ambaye ni Waziri Kivuli wa Wizara hiyo kuwa ana taarifa kuwa Lissu amewahi kuugua ugonjwa wa kichaa na hadi sasa ana faili kwenye Hospitali ya Vichaa ya Mirembe iliyopo mkoani Dodoma.
Hata hivyo, alipopewa nafasi na Naibu Spika kufuta kauli yake akasema “nafuta kauli yangu lakini kwa taarifa zilizozagaa nimeamini ni kweli na mbona kwao(Chadema) wapo wengi hata Mnyika sasa hivi yupo Muhimbili anatibiwa kichaa”.
Kutokana na kauli hiyo, Lissu alisema licha ya kuifahamu Hospitali ya Mirembe, hajawahi hata kuingia kwenye geti la hospitali hiyo wala kuugua ugonjwa huo na kutaka kiti cha Naibu Spika kimtake Holle athibitishe ; na akishindwa kanuni zielekeze hatua za kuchukua kama zilivyowekwa.
0 Comments