Wizara ya Maliasili na Utalii imetoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari katika maeneo hatarishi hususani ambayo yamebainika kuwa na Mamba au Viboko na kuwasilisha taarifa za matukio haraka kwa Viongozi wa Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori walio karibu ili kumbukumbu za matukio na hatua stahiki ziweze kuchukuliwa mapema.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni Dodoma na Naibu Waziri, Wizara ya Maliasili na Utalii, Mhe. Ramo Makani wakati akijibu swali la Mbunge wa Bunda Mjini, Mhe. Esta Bulaya ambaye alitaka kujua jinsi gani Serikali imejipanga katika kuokoa maisha ya Wananchi kutokana na hatari kubwa ya mamba hao.
Mhe. Makani amesema kwamba baadhi ya Vijiji vilivyotajwa na Mhe. Mbunge Esta Bulaya vinapatikana na Ziwa Viktoria na mazingira hayo yanasababisha kuwepo na mwingiliano wa shughuli za kibinadamu na makazi ya wanyamapori kama vile mamba pamoja na viboko ambayo yanaweza kusababisha matukio ya wananchi kuuawa na kujeruhiwa na wanayamapori hao.
“Wizara yangu imepokea taarifa zilizowasilishwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambazo zinaendelea kuhakikiwa, kwamba katika kijiji cha Guta jumla ya wananchi wanne waliuawa na wengine tisa kujeruhiwa na mamba katika kipindi cha mwaka 2013 hadi 2015”, alisema Mhe. Makani.
Aliendelea kusema kwamba katika kipindi hicho, hakuna taarifa yoyote iliyotolewa na kupokelewa kuhusu matukio katika vijiji vya Tairo, Nyamtwali na Njabeu.
Alifafanua kuwa, Kifungu cha 69 cha Sheria ya Kuhifafhi Wanyamapori Na. 5 ya mwaka 2009, kimempa mamlaka Mkurugenzi wa Wanyamapori kukasimu majukumu ya kushughulikia masuala ya Wanyamapori wakali na waharibifu kwa Afisa aliyeidhinishwa.
Aidha, Sheria imeainisha utaratibu wa kutoa taarifa za matukio kuanzia kwa Mtendaji wa kijiji, Maafisa Wanyamapori walioko karibu hadi Wizarani kwa hatua zaidi.
“Ili kuokoa maisha ya wananchi kutokana na hatari ya mamba na viboko katika vijiji vilivyotajwa, Wizara yangu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda itafanya tathmini ya ongezeko la mamba, na iwapo itadhihirika kuwa idai yao ni kubwa kuliko viwango vinavyokubalika hatua stahiki zitachukuliwa ikiwa ni pamoja na kuweka utaratibu wa kuwavuna wanyama hao”, alisema Mhe. Makani.
Aliongeza kuwa utaratibu huo utatumika katika maeneo yote yenye uhatarishi wa mamba na viboko. Wizara itaendelea kutoa elimu kuhusu uhifadhi, jinsi ya kujilinda na kujiepusha na wanayamapori wakali na waharibifu wakiwemo mamba pamoja na taratibu za kuwasilisha madai ya malipo ya kifuta jasho na machozi kwa wale watakaoathirika.
“Pamoja na jitihada hizo za Serikali, Wizara inatoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadahari katika maeneo hatarishi hususan ambayo yamebainika kuwa na Mamba au Viboko na kuwasilisha taarifa za matukio hayo haraka kwa Viongozi wa Vijiji husika na Maafisa Wanyamapori”, alisisitiza Mhe. Makani.
Na Benedict Liwenga – MAELEZO, Dodoma