Baadhi ya Wabunge wanaotoka Kanda ya Ziwa wameomba Wizara ya Ujenzi , Uchukuzi na Mawasiliano kujenga Uwanja wa Ndege wa Mwanza kwa kiwango cha Kimataifa ili kuimarisha sekta ya Utalii na usafiri wa anga katika kanda ya Ziwa.
Walisema kuwa hatua itasaidia watalii wanaokuja nchini kushuka moja kwa moja mkoani Mwanza na kisha kuelekea katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti na maeneo mengine ya vivutio vya hapa nchini bila kupitia nchi jirani.

Kauli hiyo imetolewa jana na Wabunge Dkt.Raphael Chegeni  na Mhe. Ezekeil Maige wakati wakichangia hotuba kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Ujenzi ,Uchukuzi  na Mawasiliano kwa mwaka ujao wa fedha.
Mhe. Dkt.Chegeni alisema kuwa Uwanja wa Ndege wa Mwanza ni muhimu ukajengwa kwa viwango vya Kimataifa ili uweze kuruhusu ndege mbalimbali kubwa na ndogo kuweza kutua bila tatizo.
Alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kuunganisha Mkoa wa Mwanza na nchi jirani za Rwanda, Uganda na Burundi na hivyo kuruhusu ndege nyingi kutoka Nchi hizo kutua bila kwenda katika Uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere .
Mhe. Dkt. Chegeni  aliongeza kuwa uwanja huo endapo utajengwa kwa kiwango cha Kimataifa utasaidia kuwa kiungo muhimu kwa mikoa 10 ya kanda ya ziwanana kati.
Naye Mbunge wa Jimbo la Msalala Mhe. Maige alisema kuwa ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza sio tu utasaidia kuunganisha mkoa huo na mikoa mingine bali utasaidia kuchochea  uchumi wa eneo la Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla kwani watalii na wasafiri wengine watakuwa na fursa ya kuingia Mwanza bila kupitia nchi jirani.
Aliongeza kuwa endapo zoezi hilo litafanyika kwa kiwango cha kimataifa litatoa fursa kwa ndege nyingi za ukumbwa tofauti tofauti kutua katika Uwanja huo na hivyo kupunguzia wananchi ughali wa bei unaotozwa na baadhi ya Kampuni za Ndege ambazo zinatoa huduma za usafiri mkoani humo.
Na Tiganya Vincent – Dodoma