Maafisa 5 wa polisi wa Kenya wameuawa mapema leo mjini Mandera katika shambulizi lililotekelezwa na wapiganaji wa kundi la wanamgambo la Al shabab kutoka Somalia.
Kamishna wa jimbo hilo la kaskazini mashariki mwa Kenya bwana Job Borongo ameithibitishia BBC kuwa wapiganaji hao walifanya shambulizi la kuvizia dhidi ya msafara wa magari ya polisi uliokuwa ukienda El Wak wakitumia guruneti.
Maafisa hao tano waliangamia papo hapo huku gari walimokuwa wakisafiria likiharibiwa kabisa.
Maafisa wengine wanne wamejeruhiwa vibaya.
Msafara huo wa polisi ulikuwa ukitoa ulinzi kwa msafara wa mabasi ya uchukuzi wa umma, desturi iliyoanzishwa baada ya wapiganaji hao kuteka basi moja na kuua abiria 28 wakristu.
Gavana wa Mandera bwana Ali Roba aliwalaumu maafisa wa polisi katika eneo hilo kwa kupuuza tahadhari iliyotolewa na wenyeji kuhusiana na mashambulio ya kigaidi.

Image copyright
Image captionMaafisa hao tano waliangamia papo hapo huku gari walimokuwa wakisafiria likiharibiwa kabisa.

Roba anasema walipuuza vyanzo vya kiintelijensia vilivyotolewa kuhusiana na kuonekana kwa wapiganaji hao waliojihami.
Hii si mara ya kwanza Mandera kushuhudia mashambulizi ya al shabaab.
Shambulizi hilo la Novemba mwaka wa 2014 liliwaacha wasafiri wengi wasiokuwa waislamu na hofu ya kusafiri na hivyo kuilazimu serikali kutoa usalama kwa mabasi ya uchukuzi wa umma.
Mwezi mmoja baadaye wapiganaji hao waliwaua wachimba migodi 36 katika eneo hilo la Mandera.
Kundi hilo la wapiganaji wa kiislamu limekuwa likitekeleza mashambulizi katika maeneo ya kaskazini mwa Kenya likitaka kuishinikiza taifa hilo jirani kuondoa majeshi yake nchini Somalia.

Image captionGavana wa Mandera bwana Ali Roba aliwalaumu maafisa wa polisi katika eneo hilo kwa kupuuza tahadhari iliyotolewa na wenyeji

Kenya ilipeleka vikosi vyake vya jeshi nchini Somalia mwaka wa 2011 ikitaka kuzima mashambulizi ya mara kwa mara.
Hata hivyo kundi hilo limeongeza mashambulizi nchini kenya ikiwemo mauaji ya watu 67 katika maduka ya Westgate mjini Nairobi mwaka wa 2013.
Mwaka uliopita Al Shabab ilitekeleza mashambulizi katika chuo kikuu cha Garissa na kusababisha vifo vya wanafunzi 148