Mahakama moja huko Qatar imempata na hatia mwanamke raia wa Uholanzi kwa kushiriki ngono nje ya ndoa.
Alizuiwa mnamo mwezi Machi baada ya kuwaambia maafisa wa polisi kwamba alibakwa.
Mwanamke huyo amepigwa faini ya dola mia nane na kifungo cha mwaka mmoja japo hatatumikia jela. Kwa mujibu wa mawakili wake, mama huyo alikua amekwenda kwenye hoteli moja ya burudani mjini Doha.
Wakati aliporejea mezani alipokua akikunywa kinywaji chake na kuanza kusinzia, hapo akafahamu kinywaji hicho kiliwekwa kemikali fulani.
Alipopata fahamu alijipata akiwa ndani ya makaazi ya mtu asiyemhafamu na alikuwa amebakwa. Msemaji wa ubalozi wa Uholanzi mjini Doha ameiambia BBC kwamba mwanamke huyo ameachiwa huru kutoka korokoroni na anatarajiwa kurejeshwa nyumbani.
Taarifa zaidi zinasema kwamba, mwanamme aliyepatikana na hatia ya kufanya mapenzi na mwanamama huyo amehukumiwa viboko 140.
Nchini Qatar ni hatia kubwa kunywa pombe au kupatikana ukiwa mlevi hadharani. Hata hivyo kuna baadhi ya hoteli za kitalii ambapo wateja hukubaliwa mvinyo.
Kufanya mapenzi nje ya ndoa pia ni hatia katika nchi hiyo. Hapo mwaka wa 2013, mwanammke raia wa Norway alihukumia miezi 16 gerezani katika nchi jirani ya Umoja wa Falme za kiarabu, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya mapenzi nje ya ndoa, na kuwa mlevi hadharani.
Alipokamatwa aliwaambia polisi alikua amebakwa. Alipewa msamaha na kurejeshwa nyumbani.
Kesi hii ya mwanamke raia wa Uholanzi inazua wasi wasi jinsi mamlaka za Qatar zitakavyowashughulikia maelfu ya watalii wa kigeni kutoka magharibi ambao watazuru nchi hiyo kwa fainali za kombe la dunia mwaka 2022.
Wengi wa watalii hawalewi kuhusu baadhi ya sheria hizi.
0 Comments