Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
KATIBU wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah leo ataeleza kinachoendelea kuhusu kusudio la Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutaka kumwondoa madarakani Naibu Spika, Dk Tulia Ackson (pichani).
Kambi hiyo inayoongozwa na Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Taifa, Freeman Mbowe katika migomo yake dhidi ya vikao vinavyoongozwa na Dk Ackson, iliwasilisha kusudio hilo kwa Ofisi ya Spika wa Bunge wiki iliyopita kwa maelezo kuwa haina imani naye.

Kwa mujibu wa Dk Kashillilah, ataeleza kinachoendelea leo baada ya kumaliza kupitia taratibu zote na kujiridhisha kuhusu kila hatua inayopaswa kufuatwa kuhusu suala la aina hiyo. “Nitaeleza kinachoendelea kesho (leo) baada ya kujiridhisha kuhusu taratibu zinazopaswa kufuatwa kuhusu suala hilo,” alisema.
Katika kusudio hilo lililowasilishwa na Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya, Kambi hiyo ya Upinzani ilieleza mambo sita yaliyoisukuma kuona kuwa Dk Tulia hafai kuendelea kushika kiti cha Naibu Spika.
Mambo hayo ni upendeleo kwa wabunge wa CCM, kusimamia maslahi ya Serikali badala ya umma, kutokuwa mwanasiasa, jambo linalomfanya akose uzoefu wa kuendesha vikao vya Bunge, ubabe, unyanyasaji kwa wabunge wa upinzani na kusimamia fedha za Mfuko wa Bunge zirudishwe kwa Rais.
Millya alisema walipeleka kusudio hilo kwa Ofisi ya Spika kwa kuzingatia ibara ya 85(4) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia hatua za kuchukua ili kumwondoa madarakani Naibu Spika.
Ibara hiyo inasema, “Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na ataacha kiti cha Naibu Spika ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu Spika kwa azimio la Bunge.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa ili hoja hiyo ijadiliwe bungeni italazimika kujadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge ambayo nayo inahitaji theluthi moja ya saini za wabunge wote.