Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
CHAMA Cha Kijamii (CCK) kimelaani mpango unaofanywa na wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, wa kutaka kumng’oa Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson na kimewataka kufuata kanuni za uendeshaji wa Bunge.

Hayo yamo kwenye taarifa ya Mwenyekiti wa Taifa wa CCK, Constantine Akitanda aliyoitoa kwa vyombo vya habari jana, iliyotokana na tathmini ya Bunge tangu kurejeshwa Mfumo wa vyama vingi vya siasa, chanzo na kupevuka kwa ususaji wa shughuli za Bunge.
Kuhusu mpango wa kutaka kumng’oa Dk Tulia, Mwenyekiti huyo wa CCK alisema; “Hivi sasa kuna propaganda inayoenezwa ya kutaka kumng’oa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kwa madai ametumwa na Rais kuminya uhuru na demokrasia ndani ya Bunge.
“Hii si mara ya kwanza kwa kambi ya rasmi ya upinzani kulalamikia kiti cha Spika. Pia si mara ya kwanza kwa kambi hiyo kususa na kutoka nje ya bunge, pia si mara ya kwanza wabunge wa upinzani kukorofishana na kiti cha spika na kususa,” alisema.
Akitanda alisema tatizo la kambi hiyo ni pale spika anaposimamia kanuni huku wao wakikataa kwa makusudi, kufuata taratibu na kanuni za uendeshaji wa shughuli za Bunge, jambo alilosema haliwezi kufumbiwa macho.
“Kanuni zipo wazi kama hujaridhika na maamuzi ya kiti cha Spika unaruhusiwa kukata rufaa na hoja ikajadiliwa, sasa wabunge wetu wa Kambi Rasmi ya Upinzani sijui ni kwa nini hawataki kufuata utaratibu huu, ambao ni wa kikanuni.
Wao wanataka kumng’oa Naibu Spika tu basi, kanuni je?” Alisema dalili za kukataliwa kwa Naibu Spika na wabunge hao zilionekana tangu mwanzo kwani walimkataa hata kabla ya kuanza kazi kwa madai kuwa ametumwa na Ikulu, na hata siku ya kujieleza akiomba kura alikuwa anazomewa na wabunge wa kambi hiyo.
“Kimsingi tangu mwanzo wabunge wetu wa upinzani hawakumtaka Dk Tulia kutokana na umahiri wake wa kuzijua na kuzisimamia kanuni kwa ustadi mkubwa.” Akitanda alisema tangu Bunge la vyama vingi lianze mwaka 1995, wabunge wa upinzani kutokana na uchache wao wamekuwa wanalalamikia kiti cha Spika na kutofautiana na Spika au kudai wanaburuzwa na wenzao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Alisema katika kipindi cha mwaka 2010 hadi sasa ambapo Chadema kwa mara ya pili imetoa kiongozi wa upinzani bungeni, nchi imeshuhudia wabunge wa upinzani wakitumia muda mwingi kulalamikia kiti cha Spika.
“Kwa kipindi cha 2010 hadi 2015, Spika wa Bunge alikuwa Anne Makinda na Naibu Spika Job Ndugai. Wapinzani walimlalamikia sana spika wakimtuhumu kuwa anailinda serikali na kuwa kiti cha Spika kimemshinda.
Alisema picha ambayo Watanzania wanaipata kutoka kwa Kambi Rasmi ya Upinzani yenye nia ya kumng’oa Dk Tulia kwa kupiga kura ya kutokuwa na imani naye, ni mwendelezo wa wazi wa udhalilishaji wa wanawake kuwa hawana uwezo wa kuongoza.