Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde
WAKATI wabunge wengi wamekuwa wakipinga mapendekezo ya serikali kuwakata kodi kwenye kiinua mgongo chao, Mbunge wa Mtera (CCM), Livingstone Lusinde, amekuwa wa kwanza kusimama bungeni na kusema anaunga mkono mapendekezo hayo.
Akichangia Bejeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/15 na hali ya uchumi kwa mwaka 2015 bungeni mjini Dodoma jana, Lusinde alisema yeye yuko tayari kukatwa kodi kwenye kiinua mgongo chake kwa sababu anaamini serikali ina nia nzuri.

Aliwashauri wabunge kuacha kulalamikia mpango huo, unaotarajiwa kutekelezwa mwaka 2020 pale Bunge la sasa litakapovunjwa, badala yake alisema wabunge wanao muda wa kutosha wa kukaa na serikali kwa kuangalia faida na hasara ya hatua hiyo ingawa yeye aliona ni hatua njema.
“Mimi (katika hili) ninajitoa mhanga na ninawataka wananchi wasituelewe vibaya kwani tunayo nia pia ya kuchangia mapato ya serikali. Wabunge tukae na serikali, tuzungumze nayo tuone athari na faida. Tusiilazimishe kwa sababu Rais wetu ana nia nzuri na hawezi kukosea katika hili,” alisema.
Mbunge huyo alipoanza kutetea hoja hiyo wabunge wengi waliokuwa wakimshangilia kabla wakati akiwapa wapinzani ‘vidonge’, waliduwaa na kuonekana kumshangaa, aliposema katika kutafuta maendeleo ni wakati sasa wa wabunge kujifunga mkanda, na kama mtu alikuwa anakunywa bia 10 kwa siku basi anywe bia moja.
Mbunge huyo pia aliwataka wabunge wanapojadili hoja hiyo, wasiwaguse au kujilinganisha na watu wengine, akimaanisha kile ambacho kimekuwa kikisemwa na baadhi ya wabunge kwamba kama ni suala la kukatwa kodi ya kiiunua mgongo, basi isiwaguse peke yao bali na viongozi wengine ambao pia husamehewa kodi hiyo.
Mbunge mwingine ambaye ameunga mkono hoja hiyo, ingawa hakutumia jukwaa la Bunge ni wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe. Zito ambaye amekuwa pia akiishauri serikali, iondoe posho za wabunge, hususani za vikao akisema hazina tija.
Alisema mbunge hulipwa Sh 220,000 kwa kila kikao anachohudhuria. Akizungumza katika mdahalo wa uchambuzi wa bajeti ya serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 ulioandaliwa na kampuni ya Ukaguzi wa Hesabu ya KPMG, Zitto alikaririwa akisema wabunge wakikatwa kodi kwenye posho hizo pamoja na kiinua mgongo, serikali itaongeza mapato ambayo yatatumika kwa shughuli zingine za maendeleo.
Kwa mujibu wa mbunge huyo wa upizani, kwa mwaka wabunge hupokea posho ya Sh milioni 40 ambayo ikizidishwa kwa miaka mitano ni zaidi ya Sh milioni 200 huku kiinua mgongo ambacho wabunge wanapinga kisikatwe kodi kikiwa Sh milioni 172.
Wananchi wengi wakiwemo wasomi na wachambuzi wa masuala ya uchumi, wamekuwa wakipongeza hatua ya serikali kuamua kukata kodi kiinua mgongo cha wabunge na wengi wakiona kana kwamba hatua hiyo imekuja ikiwa imechelewa.
Hata hivyo, ndani ya Bunge jana wabunge wengi waliopata nafasi ya kuchangia akiwemo Mbunge wa Kasulu Mjini (CCM), Daniel Nsanzugwanko, waliendelea kukataa kodi hiyo ya kiinua mgongo wakiitaka serikali iache kuwakata.
“Sisi wabunge si wafanyakazi wa serikali, tunakatwa kodi kwenye mishahara na hatuna hata bima ya afya, kwa hiyo hicho kiinua mgongo hakina sababu ya kukatwa kodi,” alisema Nsanzugwanko.
Naye Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Milinga, alidai ana wasiwasi kwamba hatua ya kubana matumizi na kukusanya mapato inaweza kwenda hata kusikostahili. “Leo watatukata kodi wabunge ya kiinua mgongo, kesho wanaweza kusema hata magari tusitumie badala yake tutumie baiskeli,” alisema.