hn Magufuli akikagua Kituo cha Mawasiliano ya Polisi katika Kituo Kikuu cha Polisi Kati katika Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, jana. Kushoto ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Ernest Mangu
RAIS John Magufuli ameagiza hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya kampuni nne za makandarasi ambazo Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda alisimamisha zisipewe zabuni kutokana na kazi nyingi walizopewa kuwa chini ya kiwango.

Kampuni hizo ni Inshinomya ambayo mkataba wake umesimamishwa kutokana na uwezo wake wa kujenga kuonekana kuwa mdogo, wakati kampuni za Del Mononte, Skol Building Contractors na Germinex Construction zikisitishiwa kupewa zabuni mpya hadi watakapojiridhisha kuwa wana uwezo.
Magufuli aliyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa mpango wa usalama wa raia na kutaka Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB) na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuanza kulishughulikia suala hilo kwa mujibu wa Sheria ya 16 na 17 ya mwaka 1997 ikiwa ni pamoja na Injinia aliyekuwa akisimamia miradi yote ya wazabuni hao naye pia kuchukuliwa hatua za kisheria.
“Lazima twende mbele kwa yale tuliyoahidi ninakupongeza RC kwa hatua anazochukua kwani analalamika pamoja na vyombo vya dola kuwepo na hawataki kuchukua hatua,” alisema Magufuli.
Akizungumza jana, Makonda alitoa mfano wa barabara iliyojengwa kwa kiwango cha chini kuwa ni ile inayotoka Ubalozi wa Ufaransa-Biafra mpaka Mwananyamala. Alisema makandarasi hao walilipwa zaidi ya Sh bilioni nne na nyingine milioni 400 kinyume cha utaratibu, hivyo aliagiza makandarasi hao kujenga upya barabara hizo kwa fedha zao na zile walizolipwa bila utaratibu wazirejeshe