Naibu Spika Dk Tulia Ackson.
WATENDAJI wa serikali wametajwa kuwa kikwazo katika uendelezaji wa miradi ya kuondoa kero kwa wananchi, kupitia mfumo wa ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP).
Wabunge walisema hayo jana katika semina iliyotolewa kwao kuhusu sera ya uendelezaji wa miradi mbalimbali kupitia mfumo huo, iliyotolewa na Kamishna wa PPP, Dk Frank Mhilu, kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.

Akichangia mada katika semina hiyo, Mbunge wa Muheza, Adadi Rajabu (CCM), alitoa mfano wa wawekezaji kutoka China aliowapeleka katika wizara hiyo, ili wajenge barabara ya Dar es Salaam Chalinze na hoteli ya hadhi ya nyota saba.
Mbunge huyo alisema wawekezaji hao alikutana nao Zimbabwe ambako wamefanya kazi kubwa, lakini urasimu waliokutana nao katika wizara hiyo,ulisababisha waondoke na kwenda Msumbiji, ambako wamejenga barabara kutoka Bandari ya Beira mpaka Zimbabwe, pamoja na uwanja wa ndege.
Naye Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu (CCM), alitoa mfano wa mwekezaji mwingine, ambaye alitaka kujenga barabara ya njia sita kutoka Daraja la Selander mpaka Kawe, lakini kwa kuwa mawazo ya watendaji wa serikali, wanaona sekta binafsi kama ni wezi, mradi huo ukashindikana.
Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), yeye aliwataka watendaji hao wabadili mawazo yao kwa sekta binafsi, ili wawatazame wawekezaji kuwa ni wadau katika maendeleo.
Aliwataka wawekezaji hao, kuacha urasimu kwa kuwa sekta binafsi wanaweza kuwa na mawazo mazuri wakayapeleka serikalini na kutekeleza miradi mizuri. Alitoa mfano wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha ‘standard gauge’ ambapo alitaka serikali badala ya kwenda kukopa fedha kwa ajili ya kununua vichwa vya treni, watumie sera hiyo kumpata mwekezaji aendeleze mradi huo bila ulazima wa serikali kwenda kukopa.
Mbunge wa Vwawa, Japhet Hasunga (CCM), alisema huenda tatizo hilo linasababishwa na sera za Ujamaa, kwa kuwa mifumo ya PPP, ni vigumu kufanya kazi katika Ujamaa. Kwa upande wake Mbunge wa Moshi Mjini, Jafari Michael (Chadema), alimtaka Dk Mhilu kueleza tofauti ya mradi ambao serikali inamiliki hisa pamoja na sekta binafsi (joint venture), mradi wa kubuni, kujenga, kuendesha na kuhamishia serikalini na PPP.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alimkosoa Dk Mhilu kwa kutoa mfano wa mabasi ya haraka jijini Dar es Salaam (Dart) kuwa ni mradi wa PPP na kusema mradi huo si mfano hai kwa kuwa ujenzi wake ulifanywa na Serikali.
Alisema tatizo la alichosema longolongo za watendaji wa serikali katika miradi ya PPP, ni kutaka asilimia 10 ya rushwa kwa kuwa wanajua sekta binafsi itazuia tabia hiyo. Akitoa majibu ya hoja hizo za wabunge, Dk Mhilu alisema suala la urasimu na matakwa ya wabunge kwa watendaji wabadili mitazamo yao, amelichukua na atawafikishia ujumbe.
Alisema pamoja na changamoto hizo, lakini Serikali ya Awamu yaTano, imeamua kuelekeza nguvu katika PPP, ambapo kazi iliyopo ni kuchambua Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano, ili kupata fursa za miradi itakayohitaji kuendelezwa kupitia mfumo huo na kuzitangaza.