RAIS John Magufuli amelitembelea Kanisa la Maombezi, linaloongozwa na Mchungaji Antony Lusekelo (Mzee wa Upako) lililopo Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam. Amewaahidi waumini wa kanisa hilo kuwa serikali yake itatengeneza barabara ya kutoka Ubungo Kibangu hadi River Side, ambako itaungana na barabara ya Mandela.

Rais Magufuli ambaye amezungumza katika ibada ya asubuhi ya Kanisa hilo iliyofanyika jana, alisema amepita katika barabara hiyo, ambayo imekuwa ikitumiwa na waumini wa kanisa hilo na wananchi wengine wa eneo la Ubungo Kibangu kwa lengo la kujionea hali halisi.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu, Rais Magufuli alimpongeza Kiongozi wa Kanisa hilo, Mchungaji Lusekelo “Mzee wa Upako” kwa huduma ya maombezi anayoitoa kwa waumini wake na watazamaji wanaofuatilia vipindi vyake vya mahubiri kupitia runinga.
“Mimi ni mfuatiliaji mzuri sana wa mahubiri yako, kwa hiyo mahubiri unapoyatoa yanasambaa, kwa kweli mimi na familia yangu huwa yanatubariki sana, kwa hiyo nataka kukuthibitishia ninakupenda sana.
“Ndio maana kuna siku moja, ulizungumza kuhusu shida ya barabara yako ikabidi nitafute mbinu za namna gani tunaweza kuishughulikia kwa utaratibu ulio wazi, nikamtuma Meneja wa Barabara wa Mkoa wa Dar es Salaam, akaja, akaipitia na akafahamu changamoto zilizopo, akafanya upembuzi yakinifu na usanifu, nataka kukuthibitishia kuwa fedha za kutengenezea barabara hii zipo,” alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na waumini.
Kwa upande wake, Mchungaji Lusekelo alimshukuru Rais Magufuli kwa kulitembelea kanisa hilo, na amemuombea heri katika uongozi wake ili afanikishe azma ya kuliletea taifa maendeleo ikiwemo mpango wa kuanzisha viwanda.
Kabla ya kwenda kutembelea Kanisa la Maombezi jana, Rais Magufuli alishiriki katika Ibada ya asubuhi kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu Petro, Oysterbay ambako yeye ni muumini wake.
Wakati wa Pasaka mwaka huu, Rais Magufuli alishiriki katika ibada ya sikukuu hiyo kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Azania Front, Dar es Salaam.
Alikwenda hapo bila kutarajiwa na wakati anazungumza na waumini, alisema, “Ni kweli sikuomba ruhusa ya kuja hapa, naomba unisamehe sana (akimaanisha Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk Alex Malasusa), nilisema nataka Pasaka hii nisali Azania Front, sasa wasaidizi wangu waliniambia lazima wakuambie wewe Baba Askofu nikawaambia wasikueleze kwa sababu mimi sipo tofauti na nyinyi, mimi ni Mkristo wa kawaida.”