RAIS John Magufuli amewataka polisi kujiongeza katika utendaji kazi wao bila kusubiri majambazi kufikia hatua ya kuwanyang’anya silaha katika vituo au kuvamia nyumba, watu na kuwanyang’anya mali zao.
Aidha, alisema umefikia wakati wa polisi sasa kugangamala na kutosita kuwanyang’anya majambazi silaha haraka na akiwataka kutumia mbinu za medani kwani wananchi wamechoka kutafuta mali zao huku watu wengine wakija kuchukua na kuahidi kuangalia namna ya kuwanunulia helikopta kwa ajili ya doria.

Magufuli alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua mpango wa usalama wa raia katika kuboresha utendaji kazi kwa kutumia Mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) awamu ya pili unaoanza kutekelezwa katika wilaya ya Kinondoni Julai mosi mwaka huu na baadaye kusambaa nchi nzima baada ya miaka mitatu na kupunguza uhalifu kwa asilimia 10 kila mwaka.
Uzinduzi huo pia ulihudhuriwa na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Katibu Mkuu Kiongozi John Kijazi. “Naomba niwe mkweli na muwazi kwa sababu sitaki kuwa mnafiki kwani yapo mambo yalikuwa yakinikereketa na kuniudhi unapoona jambazi anavamia kituo cha Polisi na kuua polisi kisha kuondoka na silaha au anakwenda kuiba mahali na ana silaha anaondoka hivi hivi hili limekuwa linanipa wasiwasi kidogo.
“Kama mnazo bunduki za kutosha kwa nini jambazi aondoke bila kunyang’aywa silaha anayotumia haraka haraka ,ninaposema haraka haraka mnanielewa, kwa nini jambazi aende mahali akafanye ujambazi na polisi mshindwe kumnyang’anya silaha yake haraka haraka,” alihoji.
Alisema polisi wanazo bunduki na risasi suala ni kumnyang’anya jambazi bunduki yake haraka kwa sababu kama ameenda mahali na bunduki hakwenda kwa ajili ya maonesho na kutoa wito kwa polisi nchini wakimuona jambazi ana silaha wahakikishe wanamnyang’anya bunduki yake haraka.
Rais Magufuli alisema na yule polisi atakayekuwa amejitoa mhanga kumnyang’anya bunduki jambazi asipelekwe mahakamani ila apewe cheo kwani hakuna polisi jamii kati ya jambazi na polisi. “Nasema kwa dhati kuwa mna mbinu nyingi za kuwanyang’anya silaha majambazi ,kwani wakati mwingine unaweza kumuita tu na akakubabidhi silaha ni vyema kutumia hizo mbinu na nyingine mnazoziita za medani MM na mkifanya hivi IGP mtanifurahisha,” alisema.
Magufuli alisema wananchi wamechoka kwani wanapata mali zao kwa kuhangaika lakini anakuja jambazi kuchukua na kutoa mfano jijini Dar es Salaam ambapo wanawake wamekuwa waathirika wa matukio ya kuporwa.
“ Unakuta mwanamke anatembea na pochi au simu anakuja mtu na bodaboda na kumburuta na kuchukua mkoba wake na polisi mpo”. Aliwahoji kwa nini polisi wasijifanye kuchukua ‘boda’ na kuwashika haraka haraka watu wanaofanya vitendo hivyo kwani wakiamua Tanzania iwe na amani itakuwa na amani.
Alitoa wito kwa wakubwa wa Jeshi la Polisi ambao ni IGP na makamanda wake kuwa vijana wao wanaweza kuwa na moyo wa kufanya kazi lakini wanawabana na kuwachelewesha kufanya kazi kwani wakienda kusaka majambazi polisi hupewa maelekezo wasiwanyang’anye silaha.
Alisema wao wanakuwa kwenye vituo vya mbali hivyo siku nyingine atawapeleka wakubwa hao wa Jeshi la Polisi watangulie kuwanyang’anya majambazi silaha. Rais Magufuli alisema jeshi hilo lina vijana wazuri na imara wanaopenda kazi zao na yeye kusisitiza kuwa ataendelea kusimamia maslahi ya polisi kwani tatizo ni uwezo lakini kadri wanavyoenda mambo yatakuwa mazuri.
“Ni vyema mtusaidie nchi iwe kama nyingine hata ukisahau pochi yako unaikuta kama nchi jirani ya Rwanda ukisahau hata pochi yako unaikuta hata kesho kwa nini hapa isiwe, polisi mkiamua mnaweza,” alisema.
Alieleza kuwa kwa mfumo huo ambao wameweka wa kufuatilia kila kitu wataangalia kwa upande wa serikali kama kuna mabaki watawaongezea lakini yatumike kama yalivyokusudiwa kwani nao polisi wanalalamikiwa kutumia fedha vibaya.
Alisema suala hilo nalo linatia dosari lakini yaliyopita basi yaangaliwe yaliyopo na yajayo kwa kwenda vizuri ili nchi iwe na amani kwani Watanzania wana imani na Jeshi la Polisi. Rais alisema asilimia kubwa ya maaskari ni wazuri lakini wale wachache wasio waaminifu ni vyema wakatolewa kwani licha ya mpango huo kuwa mzuri mtu anaweza kupiga simu kisha jambazi akaambiwa na mtoa taarifa akashughulikiwa au taarifa za wasamaria zikasambaa suala ambalo lipo Polisi.
Alieleza kuwa wale vijana wanaokadiriwa 100 watakaofanya kazi kwa awamu ambao watakuwa wakipokea simu na taarifa za uhalifu utakaokuwa ukiendelea ni lazima wapewe posho maalumu na lazima wawe vijana wenye maadili kwa kuwachunguza pamoja na uangalizi maalumu.
Alitoa wito pia kwa wananchi wote kuendelea kuliamini Jeshi la Polisi na kushirikiana nalo huku wakitoa taarifa ili nchi iendelee kuwa salama kwani kwa ushirikiano wao ana uhakika wataweza kushinda masuala ya ujambazi na uhalifu unaotokea.
Rais Magufuli alisema hakuna sababu ya Dar es Salaam maduka kutofunguliwa usiku au kufanya biashara usiku lakini inawezekana wafanyabiashara wanahofia usalama wao hivyo mazingira yajengwe kuhakikisha kunakuwa na amani. Huku akitaka katika miji yote kufungwa kamera za CCTV kwani siyo vigumu wala vya gharama na vikiunganishwa katika mpango huo uhalifu utamalizika kwa haraka zaidi.
Alisema Kinondoni inasifika kwa matukio mengi ya uhalifu ambapo mwaka 2012 kulikuwa na matukio ya uhalifu 4,410 lakini mpaka kufikia mwaka 2015 vitendo vya uhalifu vilifikia 8,804.
Aliomba mpango huo uliozinduliwa Kinondoni kwa mwaka huu na miaka ijayo uhalifu ushuke na ndiyo itakuwa matokeo mazuri ya mpango huo lakini uhalifu ukipanda kutakuwa hakuna sababu ya kuwa na mpango huo.
Rais pia alimuagiza Katibu Mkuu Kiongozi kuwaagiza Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) ambao wana wajibu wa kushirikiana na polisi kwa mtu anapopiga simu katika namba 111 au 112 kusiwe na mtu wa chapa bali inapopigwa inakiliwe na kuchapwa moja kwa moja.
Alisema vyote ni vyombo vya serikali hakuna sababu ya TCRA kutofanya hiyo kazi na asiyetaka kufanya hivyo aondoke kwani atakuwa hataki kushirikiana na polisi kudhibiti uhalifu.
Kuhusu wanasiasa Alisema atafanya kazi bila kuwabagua watu kwa vyama vyao, maeneo wanayotoka makabila, dini kwani yeye kwake ni kazi tu kwani Watanzania wanahitaji maendeleo na vyama kuweka pembeni kwani wanataka kero zao kumalizwa na kuishi maisha mazuri.
Rais alisema yapo aliyoahidi kutekeleza kwa miaka mitano hivyo wamuache atekeleze kwa ajili ya Watanzania wote wakiwemo viongozi wengine wa vyama kama Diwani wa eneo hilo wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamuache atekeleze na CCM wasimsumbue kwani watamuuliza baada ya miaka mitano.
Alisema aliyoyaahidi hategemei mtu mmoja kumchelewesha kutekeleza hayo, kwani anataka baada ya miaka mitano kupimwa kwa aliyoyaahidi kwa hiyo polisi wasimamie watu wasiwacheleweshe kutekeleza aliyoyaahidi. “Najua mmenielewa ‘Message sent and Delivery’ kwani ndugu zangu hamtaki nitekeleze yale niliyoahidi?”
Alijibiwa na umati wa watu kuwa wanataka. Naye, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Ernest Mangu alisema mpango wa kuboresha jeshi hilo awamu ya kwanza ulikuwa kwa miaka 10 kuanzia 2006 hadi 2014 lakini kulikuwa na changamoto iliyoshirikisha Ofisi ya Rais na kutengeneza mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) awamu ya pili uliozinduliwa jana.
Alisema utekelezaji wake utaanza Julai Mosi, mwaka huu kwa kuanza na wilaya ya Kinondoni na baadaye kuenea nchi nzima kisha baada ya miaka mitatu kufika maeneo yote ya nchi ambapo kwa Jiji la Dar es Salaam zinahitajika Sh bilioni 27 ili kuwa na hali ya usalama kuliko majiji yote Afrika.
Rais Magufuli alisema katika mpango huo wataongeza ufanisi katika kushughulikia uhalifu kwa kuwa na mtandao wa vituo vya Polisi vikiwemo vya kuhamahama kwa kupeleka sehemu uhalifu ulipokithiri na kuwa na askari wa doria ambapo utaongozwa na GPS mpaka kituo kikubwa cha mawasiliano.
Alisema pia kuboresha huduma za kipolisi na kuboresha mawasiliano kwa kufungua kituo cha mawasiliano kwa kuwasiliana na polisi wa doria ili linapotokea tukio la uhalifu iwe rahisi kukabiliana nalo kwa haraka na kubuni vyanzo vya fedha.