SERIKALI imesitisha utaratibu mpya uliotangazwa wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wa kutoa chakula kwa wagonjwa wote waliolazwa katika Hospitali hiyo kuanzia Julai Mosi, mwaka huu.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu (pichani) jana aliagiza hospitali kusitisha utaratibu mpya uliopendekezwa wa huduma ya chakula kwa wagonjwa.

Alitoa agizo hilo jana alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kusema kuwa Wizara imeamua kusitisha huduma hiyo mpaka pale itakapopata taarifa za kutosha kuhusu faida na hasara za utaratibu huo mpya uliopendekezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Jumanne, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano ya Umma wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema hospitali hiyo imeboresha huduma zake na kwamba imeingia ubia na wazabuni ili kutoa huduma hiyo kwa wagonjwa kuanzia Julai Mosi.
Hata hivyo Waziri Ummy alisema wizara imepokea maoni mengi kutoka kwa wananchi kuhusiana na hatua iliyochukuliwa na Muhimbili baada ya kuwataka wananchi kuchangia gharama za chakula ili hospitali hiyo iweze kutoa kwa wagonjwa.
“Kufuatia hali hii kuleta wasiwasi kwa wananchi na wagonjwa, nimeagiza Hospitali ya Muhimbili kusitisha utaratibu huo mpya mpaka hapo tutakapopata taarifa za kutosha kuhusu faida na hasara za utaratibu mpya unaopendekezwa,” alisema Ummy.
Alisema hiyo ni moja ya juhudi zilizofanywa na uongozi wa hospitali hiyo katika kuboresha huduma kwa wagonjwa ikiwemo kuboresha upatikanaji wa dawa na chakula. “Hata hivyo inaonekana hakukuwa na ushirikishwaji wa kutosha wa wananchi katika suala hili, sasa tutaboresha kwa maoni ambayo tutapokea,” alisema waziri huyo.
Wiki iliyopita Hospitali ya Muhimbili ilitangaza kuwa chakula kitaandaliwa hospitalini hapo na ili kutoa huduma hiyo mgonjwa atatakiwa kuchangia kidogo na kulazimika kutoa Sh 10,000 kwa kulazwa, kumuona daktari Sh 10,000 na Sh 30, 000 kwa chakula. Gharama hizo ni kwa siku tano ambazo kwa ujumla ni Sh 50,000.