RAIS John Magufuli ameagiza kwa taasisi zinazosimamia fedha na kodi, kuhakikisha kuwa serikali inakusanya kodi kwenye miamala ya fedha, inayofanywa na taasisi hizo na kampuni za simu na za madini.
Aidha, ameagiza kuwa Sh bilioni saba zilizolipwa kwa pensheni hewa, zirejeshwe mara moja huku akitoa ufafanuzi wa hatua ya serikali ya kusitisha kwa muda ajira serikalini.

Rais Magufuli alisema hayo Dar es Salaam jana katika kilele cha maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Maadhimisho hayo yalikwenda sambamba na uzinduzi wa sarafu maalumu yenye thamani ya Sh 50,000 na vitabu viwili, kikiwemo vinavyozungumzia masuala ya fedha na uchumi.
Uzinduzi huo uliofanyika katika ukumbi wa BoT jijini Dar es Salaam, ulikwenda pamoja na kongamano lililojadili mada kuhusu namna ya kupata fedha za miradi ya maendeleo zaidi ya misaada na mikopo nafuu na athari zake iliyowasilishwa na Profesa Justin Lin wa Chuo Kikuu cha Peiking, China.
Rais Magufuli alisema takwimu zinaonesha katika mwezi mmoja wa Machi, miamala iliyofanywa na kampuni za simu za mkononi ni ya zaidi ya Sh trilioni 5.5, lakini alihoji ni kasi gani cha kodi kimeingia serikalini.
Alisema pamoja na kusimamia makusanyo ya kodi za serikali, pia aliagiza BoT, Hazina na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), wajipange kuhakikisha mtambo wa kudhibiti makusanyo ya kodi, unafanya kazi na kufuatilia usalama wa huduma za fedha.
Mbali na hilo, aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha serikali inakusanya kodi zinazostahili kutoka kwenye kampuni za madini na kufuatilia kwa karibu, kwa kuwa kuna udanganyifu mkubwa unaofanywa na baadhi ya kampuni.
“Unakuta kampuni ipo nchini mwaka wa kwanza hadi wa 10, wanakwambia hawapati faida lakini wanaendelea kuchimba dhahabu. Sasa eneo hilo liangaliwe kwa karibu na kama kampuni inashindwa bora iondoke, ni heri tubaki na dhahabu yetu hata miaka 1000 ijayo, watakuja kuchimba wengine wakati sisi tumeshaoza. Visingizio vya kupata hasara kila mwaka, lakini wanaendelea kuwepo, haiwezekani,” alisema.
Aliwataka watendaji hao kutokuwa na kigugumizi katika kusimamia rasilimali kwa manufaa ya Taifa na kwamba serikali ina imani kubwa na BoT, hivyo wakisimamia vizuri uchumi utaimarika.
Pensheni hewa
Aidha, aliwataka viongozi wa taasisi hizo pia kushirikiana katika kudhibiti malipo kwa watumishi hewa, ambayo sasa imefikia kwenye utoaji wa pensheni hewa. Alisema anazo taarifa kuna wafanyakazi hewa 2,800, ambao wamelipwa pensheni hewa ya Sh bilioni saba kupitia Benki ya NMB, na kuagiza fedha hizo zifuatiliwe na benki hiyo izirejeshe mara moja.
“Wakati nazungumzia watumishi hewa ndani ya serikali wamefikia 12,446 na kwamba inawezekana idadi hiyo ikaongezeka na sasa watumishi hao wamelipwa pensheni shilingi bilioni saba,” alisema.
Rais Magufuli alisema wakati serikali inahakiki wafanyakazi hewa, Utumishi waliendelea kuajiri wapya, jambo ambalo kwa sasa amelisimamisha kwa miezi miwili ili kutoa nafasi ya kushughulikia changamoto hiyo.
Kusitishwa ajira
“Nilisema ajira mpya zisimame kwa mwezi mmoja na nusu lakini haitazidi miezi miwili, nawaomba watumishi msivunjike moyo kwa kuwa serikali imegundua kosa lazima lirekebishwe, lazima tujipange. Hata kupandisha vyeo tumesimamisha kwa muda huo baadae tutaendelea, tunataka kujenga nidhamu,” alisema.
Pia aliitaka BoT kufuatilia kwa karibu utendaji wa benki na kuchukua hatua kwa benki, ambazo hazifanyi kazi vizuri hata kama zinamilikiwa na serikali.
“Benki mojawapo ni Twiga Bancorp, haifanyi kazi vizuri, inajiendesha kwa hasara na serikali imekuwa ikiipatia fedha kila mwaka za uendeshaji. Hasara imefikia shilingi bilioni 18. Naomba Katibu Mkuu Hazina na BoT mfuatilie kama imeshindwa kujiendesha ifungwe.
“Katika utawala wangu sitabembeleza, nataka watu wafanye kazi kama benki haizalishi ni afadhali ikafungwa kuliko kuendelea kuitia hasara serikali. Kuna benki nyingine nayo ambapo inapigiwa debe na wanasiasa tena wa CCM lakini nayo haifanyi vizuri,” alisema.
Alisema kwa kuwa Gavana wa BoT, Profesa Benno Ndulu, sio mwanasiasa, anapaswa kufanya kazi yake bila kujali kama benki ni mali ya serikali au la, na kuwaacha wanasiasa waendelee na yao.
Aidha, aliagiza BoT kufuatilia suala la akaunti zilizolala kwenye benki kwa kuwa wakati mwingine fedha zinakaa mpaka watu wanapanga kuzitorosha. “Najua kwenye akaunti hizo kuna fedha nyingi, kuna akaunti moja ina Sh bilioni 23. Nataka mfuatilie na mimi nafuatilia kwa karibu,” alisema.
Pia aliwataka BoT kufuatilia kwa karibu maduka ya kubadilisha fedha ili wafanye biashara halali na yasitumike vibaya kutorosha fedha ama kutakatisha fedha haramu zikiwemo za wafanyabiashara wa dawa za kulevya.
Mfumuko wa bei
Alisema kwamba jukumu kubwa la BoT ni kudhibiti mfumuko wa bei na katika kipindi cha miaka ya 1990 hadi mwaka huu, Benki Kuu imefanya kazi kubwa ya kupunguza mfumuko wa bei kutoka asilimia 30 hadi asilimia 5.2.
Hata hivyo, alisema kupungua huko kunaonekana vizuri kwenye takwimu, lakini katika uhalisia wa maisha ya watu bado kuna changamoto kubwa; na wakati mwingine wananchi wanaona kama mfumuko wa bei umeongezeka hadi kufikia asilimia 70.
Kutokana na hali hiyo, aliwaagiza watendaji wa BoT wakiongozwa na Gavana Ndulu, kuhakikisha hiyo asilimia iliyopungua inaonekana kwenye maisha ya wananchi wa kawaida kwa maana ya bei za bidhaa kupungua.
Aliwapongeza wafanyakazi wa BoT chini ya uongozi wa Profesa Ndulu kwa mafanikio waliyoyapata katika kipindi cha miaka 50, ikiwemo kuongeza benki kutoka tatu hadi 54 ambazo zimeendelea kufanya kazi na kutoa mikopo.
Fedha vijijini
Hata hivyo, alisema kuna haja ya BoT kuhakikisha huduma za fedha zinafikishwa vijijini ambako kuna zaidi ya asilimia 70 ya Watanzania badala ya kubaki mijini, ambako kwa sehemu kubwa wanafanya biashara na serikali.
Alisema pia taasisi za fedha zimeendelea kutoa mikopo na kutoza riba kubwa, ambapo sehemu kubwa ya wakopaji wamejikuta wakishindwa kuendelea na wengine kufilisika kutokana kulipa fedha nyingi za riba kwenye mikopo.