Waziri wa Sheria na Katiba, Dk arison Mwakyembe.
KATIKA kukabiliana na suala la rushwa na ufisadi, serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 2.5 ili kuwezesha uanzishwaji wa Mahakama ya Mafisadi. Aidha, serikali imetenga jumla ya Sh bilioni 72.3 katika bajeti ya mwaka 2016/17 kwa ajili ya shughuli mbalimbali za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) ili kuiwezesha taasisi hii kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Hayo yamo katika Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17, iliyowasilishwa bungeni mjini Dodoma jana na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango. Katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), iliweka wazi kwamba itaanzisha mahakama maalumu ya kukabiliana na mafisadi na wahujumu wa uchumi, na hivi karibuni Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitangaza kwamba mahakama hiyo itaanza Julai mosi, mwaka huu.
Dk Mpango alisema vile vile katika bajeti ya mwaka 2016/17, serikali imetenga Sh bilioni 44.7 kwa ajili ya kuiwezesha Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi (NAO) kutekeleza majukumu yake ya msingi ya kukagua na kudhibiti matumizi ya fedha za umma.