Ndege ya Air Tanzania.
SERIKALI imetangaza kutenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa meli mpya katika maziwa nchini, ununuzi wa ndege tatu mpya, ujenzi wa reli ya kisasa na kulipa deni la Bohari ya Madawa (MSD).
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 bungeni jana, alisema serikali itaendelea kukabiliana na kero zinazotokana na uchakavu wa miundombinu ya reli, barabara, bandari na viwanja vya ndege.

“Katika mwaka 2016/17, serikali imetenga shilingi trilioni 5.47 sawa na asilimia 25.4 ya bajeti yote ukiondoa Deni la Taifa, kwa ajili ya miradi ya ujenzi na uchukuzi,” alieleza Dk Mpango.
Aliyataja baadhi ya maeneo yanayohusika ni ujenzi wa miundombinu ya barabara – kiasi cha Sh trilioni 2.18 kimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hasa zenye kufungua fursa za kiuchumi na kukarabati barabara zilizopo, kiasi cha Sh trilioni 2.49 kimetengwa kwa ajili ya kuanza kujenga Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge, ununuzi wa ndege mpya tatu za abiria na ununuzi wa meli mpya Ziwa Victoria.
Nyingine ni ukarabati wa meli katika Ziwa Victoria na Ziwa Tanganyika; uboreshaji wa miundombinu ya bandari; na ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege. Aidha, kiasi cha Sh bilioni 161.4 kimetengwa katika Mfuko wa Reli kwa ajili ya ununuzi wa mabehewa na vichwa vya treni pamoja na ukarabati wa reli.
Aidha, alisema serikali imetenga jumla ya Sh trilioni 1.13 sawa na asilimia 5.3 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa ili kugharimia upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa ajili ya matumizi ya majumbani na viwandani.
Kuhusu upatikanaji duni wa huduma za afya, maji na elimu, alisema sekta ya elimu imetengewa jumla ya Sh trilioni 4.77 sawa na asilimia 22.1 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa.
Alisema fedha hizi zimetengwa kwa ajili ya kugharimia shughuli mbalimbali za elimu zikiwemo: Elimu Msingi bila malipo; gharama za uendeshaji wa shule ikiwemo chakula, ununuzi wa vitabu, na mitihani; mikopo na ruzuku kwa wanafunzi wa elimu ya juu; na ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya elimu katika ngazi zote.
Kuhusu afya, alisema kwa kutambua umuhimu wa huduma bora za afya kwa wananchi, serikali imetenga jumla ya Sh trilioni 1.99 sawa na asilimia 9.2 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa kwa ajili ya sekta ya afya.
“Baadhi ya maeneo yanayohusika ni pamoja na ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi (reagents) ambayo yametengewa shilingi bilioni 180.5; ulipaji wa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD) shilingi bilioni 71.0; na uboreshaji wa miundombinu ya kutolea huduma za afya katika ngazi zote,” alisema.
Akizungumzia maji, alisema serikali imetenga kiasi cha Sh trilioni 1.02 sawa na asilimia 4.8 ya bajeti yote bila kujumuisha Deni la Taifa, kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama nchini.