Waziri Mkuu, Majaliwa Kassim Majaliwa.
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa onyo kuwa Serikali itamchukulia hatua kiongozi yeyote, atakayedokoa fedha za michango ya madawati zinazotolewa na wadau wa maendeleo.
Amewataka watendaji wa mikoa na wilaya, kuhakikisha fedha zinazotolewa kwa ununuzi wa madawati nchini zinatumika ilivyokusudiwa. Amesema watendaji na viongozi katika ngazi mbalimbali mikoani, watapimwa kwa jinsi watakavyotekeleza maagizo haya ya kuondoa changamoto ya uhaba wa madawati nchini.

Waziri Mkuu alisema hayo jana wakati wa Matembezi ya Hisani ya kukusanya fedha kwa ajili ya ununuzi wa madawati, ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ambapo walimkabidhi mfano wa hundi ya zaidi ya Sh milioni 263, Sh milioni 10 zikiwa bado ahadi na kufanya jumla ya makusanyo kuwa zaidi ya Sh milioni 273 kwa ajili ya ununuzi wa madawati.
Alisema michango inayoenda katika mikoa, lazima ifanye kazi iliyokusudiwa watakapokabidhiwa, kwa kuwa wakuu wa mikoa na wilaya ndio wamekabidhiwa kazi ya kuhakikisha madawati yanatengenezwa na kupelekwa katika shule zenye msongamano.
“Fedha zinazotolewa na watu mbalimbali kama nilivyoona kwa msanii Diamond kuchangia madawati 600 na nyingine zimetolewa na benki leo na wengine na taasisi nyingine za fedha, zitumike kutengeneza madawati na yeyote atakayekuwa anadonoadonoa tutamfikisha katika vyombo vya sheria,” alisema.
Aliwaagiza watendaji katika shule yaani walimu wakuu na walimu wote, kuhakikisha madawati yanayotengenezwa na kupelekwa shuleni yanatumika vizuri na yale yatakayokuwa yanaharibika yatengenezwe.
Alisema kuna madawati mengi hayatunzwi vizuri na hata yakiharibika kwa kuchomoka msumari, yanatupwa na kuwataka waandae mikakati ya kutengeneza ili yatumike tena wakati wadau wengine wakiendelea kuchangia.
“Nawaagiza wakurugenzi kufanya sensa ya madawati mabovu ili kujua idadi yake kisha kutafuta mikakati ya kuyatengeneza na yatumike na siyo kuyaacha yasitumike, kama nilivyosisitiza kila wilaya kuanzisha mikakati endelevu ya kuhakikisha tatizo la madawati linakwisha kabisa,” alisema.
Alisema tatizo madawati hadi kufikia Machi 30, mwaka huu, kulikuwa na upungufu wa madawati milioni tatu, ambapo katika shule za msingi upungufu ulikuwa madawati milioni 2.8 kutokana na serikali kuanzisha sera ya elimu bure, huku sekondari kukiwa na upungufu wa madawati zaidi ya 200,000.
Alipongeza wafanyakazi wa BoT kwa kutoa fedha mifukoni mwao kwa ajili ya kuchangia madawati, kitendo ambacho alikieleza kuwa ni cha kizalendo na kinachofaa kuigwa na jamii yote kwa maana ya mtu mmoja mmoja au taasisi au kikundi chochote ili kuondoa tatizo la watoto kukaa chini.
Akizungumza katika matembezi hayo Gavana wa BoT, Professa Benno Ndullu alisema fedha hizo ni mchango uliotolewa na kila mfanyakazi wa benki hiyo nchini kwa hiari yao wenyewe, walitoa mchango wa kujidhamini wenyewe kwenye matembezi hayo.
Alisema mpaka sasa zilikuwa zimekusanywa Sh 273,089,338 kwa ajili ya ununuzi wa madawati ya kupeleka katika shule zenye upungufu au zisizo na madawati Dar es Salaam na mikoa ambayo benki hiyo ina matawi, ambayo ni Mbeya, Mwanza, Zanzibar, Arusha, Dodoma na Mtwara na Chuo cha Benki hiyo cha Mwanza.
Alisema katika fedha hizo, Benki hiyo imetoa Sh milioni 167 kama mchango wao kwa jamii, wafanyakazi wametoa milioni 29.8, taasisi za fedha milioni 22 na kampuni za simu milioni 54.3.
Profesa Ndullu alisema kwa Zanzibar fedha zitakazotolewa, watapeleka katika kukabiliana na matatizo ya magodoro na mashuka kwenye baadhi ya hospitali na zahanati, kwani ndiyo changamoto kubwa kuliko madawati.