Mohammed Dewji.
LICHA ya kuongoza kwa kutoa ajira katika sekta binafsi nchini, bilionea kijana zaidi Afrika, Mohammed `Mo’ Dewji ameahidi kumwaga ajira zaidi na kufikia 100,000 ili kumuunga mkono Rais John Magufuli la kukabili tatizo la ajira.
Kwa sasa, Dewji anayemiliki mtandao wa kampuni zilizopo chini ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), ameajiri Watanzania 28,000 katika kampuni zake zaidi ya 31. Ni mwajiri mkubwa wa pili nchini baada ya Serikali.

Alikaririwa na jarida maarufu la uchumi duniani, Forbes la Marekani toleo la wiki hii akisema ameguswa na uchapakazi wa Rais Magufuli, hivyo anajiona ana jukumu la kufanya katika kuisaidia Serikali ya Awamu ya Tano baada ya Rais kuonesha dhamira ya dhati ya kuinua uchumi wa nchi.
Alisema anakusudia kuajiri Watanzania 100,000 ndani ya miaka minne, ili aweze kutimiza ndoto yake ya kurudisha kwa wananchi sehemu kubwa ya faida katika biashara zake, lakini pia kuwakwamua vijana na Watanzania waweze kujitegemea na kupiga hatua kimaendeleo, hali itakayosaidia kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.
Aliyasema hayo ikiwa ni takribani wiki moja tangu kampuni tanzu ya MeTL Group ilipong’ara katika Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa Mwaka 2015 na kutwaa tuzo tatu katika hafla iliyofanyika Dar es Salaam.
Katika tuzo hizo zilizoandaliwa na Shirikisho la Wenye Viwanda Nchini (CTI) na kuhudhuriwa na Rais Magufuli, kampuni zilizo chini ya MeTL, Star Oils (T) Ltd inayohusisha na bidhaa za petroli, East Coast Foods & Fats inayozalisha bidhaa za mafuta na sabuni na kiwanda cha nguo cha 21st Century cha Morogoro zilitwaa tuzo.
“Ninakusudia kuongeza dola milioni 500 zaidi (shilingi trilioni moja) katika biashara zangu ndani ya miaka minne niweze kuajiri zaidi ya watu 100,000, wengi wakiwa Watanzania,” alisema bilionea huyo mwenye umri wa miaka 41 ambaye yumo katika orodha ya mabilionea 24 wakubwa zaidi Afrika, lakini akiwa namba moja kwa upande wa vijana.
Alisema miongoni mwa maeneo yatakayozalisha ajira mpya ni pamoja na kiwanda kipya cha sukari anachokusudia kukianzisha, akisema si kwamba kitazalisha sukari pekee, bali pia uzalishaji wa nishati ya umeme.
Rais Magufuli, akizungumza wakati wa Tuzo za Rais za Mzalishaji Bora wa mwaka 2015, alisema serikali yake imejipanga kuwasaidia na kuwaunga mkono wawekezaji wote wa ndani, watakaoanzisha viwanda nchini ikiwa ni pamoja na kuwahakikishia ulinzi wa viwanda vyao.
MeTL Group yenye utajiri wa zaidi ya dola bilioni 1 (sh trilioni 2.2) ilianzishwa mwanzoni mwa miaka ya 1970 na imejikita katika sekta za biashara, kilimo, uzalishaji, nishati na petroli, huduma za fedha, huduma za simu, usafirishaji, usambazaji, majengo na miundombinu.