JESHI la Polisi Kikosi cha viwanja vya ndege, Dar es Salaam linamshikilia raia wa Nigeria, Bede Eke (45) kwa tuhuma za kusafirisha unga unaosadikiwa kuwa ni dawa za kulevya.

Akizungumza na gazeti hili, Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Martin Otieno alisema mtu huyo alikamatwa usiku wa kuamkia jana akiwa safarini kwenda Lagos, Nigeria.
“Juni 26, mwaka huu majira ya saa 7:25 usiku katika eneo la ukaguzi wa mashine ya chini, askari Polisi kwa ushirikiano na askari wa uwanja wa ndege Terminal II walifanikiwa kumkamata Bede Eke akiwa na begi walilolitilia shaka na katika upekuzi walibaini kuwa na unga,”alisema Otieno.
Kamanda Otieno alisema Eke alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akisafiri kwa Ndege ya Ethiopian Airline kwenda Lagos, Nigeria kupitia Ethiopia, ambapo baada ya kutiliwa shaka katika begi hilo waliamriwa kulifungua na ndani palikuwa na begi dogo la mgongoni, ambalo lilishonwa vizuri na kufungwa na gundi ya nailoni.
Alisema ndani ya begi hilo dogo la mgongoni jeusi, mlikuwa na kifurushi chenye uzito wa kilo tano na kilipofunguliwa palikuwa na unga unaodhaniwa kuwa ni dawa za kulevya.
“Tumepeleka sampuli ya unga huo kwa mkemia mkuu wa serikali ili kuweza kutambua ni aina gani ya dawa za kulevya, lakini bado tunaendelea na mahojiano naye ili kubaini ni wapi amechukua unga huo,” alisema Otieno.
Kamanda Otieno alisema kuwa kukamatwa kwa mtuhumuwa huyo kunatokana na kuongezeka kwa udhibiti na kupata mashine za kisasa za utambuzi, ikiwa ni pamoja na ari ya kazi. Tukio hilo limetokea wakati taifa na dunia, inaadhimisha upigaji vita wa dawa za kulevya. Tukio hilo ni la kwanza kwa mwaka huu katika uwanja huo.