Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amefanya uteuzi wa wakuu wa wilaya 139, huku sura mpya zikitawala, baada ya wengi wa zamani kuachwa.
Aidha, amefanya mabadiliko madogo katika safu ya wakuu wa mikoa kwa kuteua wakuu wa mikoa watatu, kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwa sababu mbalimbali, akiwemo Magesa Mulongo aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara, aliyeachwa kwenye uteuzi huo.

Ma-DC wapya
Taarifa ya Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi iliyotolewa Dar es Salaam jana, inaonesha wakuu wa wilaya wa zamani waliobakizwa ni 39 na wapya ni 78. Katika uteuzi huo uliozingatia vigezo kadhaa ikiwemo umri, kati ya wakuu wa wilaya wapya aliowateua, 22 walikuwa wakurugenzi watendaji wa halmashauri.
Taarifa ilisema wameteuliwa kushika nyadhifa hizo kutokana na utendaji wao mzuri. Kulingana na taarifa hiyo, kwa upande wa kigezo cha umri, wenye zaidi ya miaka 60, Rais Magufuli ameamua wastaafu.
“Aidha nafasi 78 za uteuzi wa wakuu wa wilaya zimejazwa na watanzania wengine ambao wameteuliwa kwa mara ya kwanza, wengi wao wakiwa ni vijana, wenye elimu ya kutosha na uzoefu katika maeneo mbalimbali,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo. Uteuzi huo umewezesha wilaya mpya kutambulika rasmi kutokana na kupangiwa wakuu wake.
Mathalani, mkoani Dar es Salaam, Wilaya ya Ubungo ambayo ni mpya, amepangiwa Humphrey Polepole aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Musoma na wilaya ya Kigamboni mkuu wake ni Hashim Mgandilwa.
Aidha, kama alivyofanya kwenye uteuzi uliopita wa wakuu wa mikoa, pia kwa upande wa wilaya, Rais Magufuli amezingatia nafasi ya wanajeshi katika uongozi wa maeneo ya pembezoni mwa nchi, hususani mikoa ya Kagera na Kigoma.
Katika Mkoa wa Kagera, wanajeshi walioteuliwa na wilaya zao kwenye mabano ni Shaban Lissu (Kyerwa), Michael Mtenjele (Ngara), Denis Mwila (Missenyi). Mkoani Kigoma walioteuliwa ni Martin Mkisi (Kasulu), Hosea Ndagala (Kakonko) na Elisha Gagisti (Buhigwe).
Katika tasnia ya habari, waandishi waandamizi walioteuliwa ni Daniel Chongolo anayekwenda Wilaya ya Longido mkoani Arusha na Godwin Gondwe anayekwenda Handeni, mkoani Tanga. Wakati wanataaluma hao wakipenya kwenye siasa kupitia wadhifa huo, wengine wanne waliokuwa wakuu wa wilaya, wameachwa.
Nao ni Betty Mkwassa (Mvomero), Lucy Mayenga (Uyui), Jackline Liana (Igunga), Muhingo Rweyemamu (Morogoro) na Novatus Makunga (Moshi). Wakuu wapya wa mikoa na wilaya walioteuliwa, wataapishwa kesho kutwa Ikulu Jijini Dar es Salaam na mara baada ya kuapishwa, watakula kiapo cha maadili ya uongozi.
Wakuu wa mikoa
Pamoja na hayo, Kijazi pia alisema kwa upande wa mabadiliko ya wakuu wa mikoa, Rais Magufuli alimteua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Zainab Telack kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.
Telack anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela ambaye uteuzi wake ulitenguliwa hivi karibuni. Rais Magufuli pia amemteua Dk Binilith Mahenge kuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mahenge anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu ambaye amehamishiwa Ofisi ya Waziri Mkuu, Dar es Salaam ambako atapangiwa majukumu mengine.
Aidha, Rais Magufuli amemteua Dk Charles Mlingwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mara. Dk Mlingwa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Magesa Mulongo ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
Walioteuliwa wakiri kazi kubwa inawakabili
Baadhi ya wakuu wa wilaya walioteuliwa, wamesema wanafahamu ukubwa wa kazi iliyo mbele yao ya kumsaidia Rais John Magufuli na kuahidi kutekeleza jukumu hilo kwa uaminifu.
Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo alisema amepokea uteuzi huo kwa kufahamu ukubwa wa kazi iliyopo mbele yake ya kumsaidia Rais John Magufuli katika kuitoa nchi kwenye uchumi wa chini kwenda wa kati.
“Hii ni changamoto kubwa kwangu na kwa wakuu wengine wa wilaya walioteuliwa. Ni lazima tutumie uwezo, ujuzi na maarifa yetu katika kuhakikisha kuwa lengo hilo la Rais linafanikiwa,” alisema.
Alisema katika kuhakikisha nchi inapiga hatua ya kasi katika kufikia uchumi wa kati, mtazamo mkubwa utakuwa ni kuhamasisha ujenzi wa uchumi utakaoegemea katika maendeleo ya viwanda, hatua ambayo pia itaongeza upatikanaji wa ajira kwa wananchi.
Kuhusu changamoto za uhaba wa madawati na chakula, ambazo rais aliapa kuwachukulia hatua wakuu wa wilaya na mikoa watakaoshindwa kukabiliana nazo, Chongolo alisema hayo ni maeneo ambayo ataelekeza nguvu kubwa katika kuyasimamia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Humphrey Polepole aliyehamishwa kutoka Wilaya ya Musoma, amepokea habari akiwa kwenye msiba wa baba yake aliyezikwa jana jijini Dar es Salaam.
Polepole ambaye katika uteuzi mpya amehamishiwa wilaya hiyo mpya, aliliambia gazeti hili kuwa yupo msibani kufuatia kifo cha baba yake mzazi, Mzee Hesron Polepole ambaye alifariki Juni 23 mwaka huu na kuzikwa jana katika makaburi ya Kinondoni.
Orodha kamili ya wakuu wa wilaya kulingana na mikoa ni:
ARUSHA
1. Arusha - Mrisho Mashaka Gambo
2. Arumeru - Alexander Pastory Mnyeti
3. Ngorongoro - Rashid Mfaume Taka
4. Longido - Daniel Geofrey Chongolo
5. Monduli - Idd Hassan Kimanta
6. Karatu - Therezia Jonathan Mahongo
DAR ES SALAAM
1. Kinondoni - Ally Hapi
2. Ilala - Sophia Mjema
3. Temeke - Felix Jackson Lyaviva
4. Kigamboni - Hashim Shaibu Mgandilwa
5. Ubungo - Hamphrey Polepole
DODOMA
1. Chamwino - Vumilia Justine Nyamoga
2. Dodoma - Christina Solomon Mndeme
3. Chemba - Simon Ezekiel Odunga
4. Kondoa - Sezeria Veneranda Makutta
5. Bahi - Elizabeth Simon
6. Mpwapwa - Jabir Mussa Shekimweli
7. Kongwa - John Ernest Palingo
GEITA 1. Bukombe - Josephat Maganga
2. Mbogwe - Matha John Mkupasi
3. Nyang’wale - Hamim Buzohera Gwiyama
4. Geita - Herman C. Kipufi
5. Chato - Shaaban Athuman Ntarambe
IRINGA
1. Mufindi - Jamhuri David William
2. Kilolo - Asia Juma Abdallah
3. Iringa - Richard Kasesela
KAGERA
1. Biharamulo - Saada Abraham Mallunde
2. Karagwe - Geofrey Muheluka Ayoub
3. Muleba - Richard Henry Ruyango
4. Kyerwa - Col. Shaban Ilangu Lissu
5. Bukoba - Deodatus Lucas Kinawilo
6. Ngara - Lt. Col. Michael M. Mtenjele
7. Missenyi - Lt. Col Denis F. Mwila
KATAVI
1. Mlele - Rachiel Stephano Kasanda
2. Mpanda - Lilian Charles Matinga
3. Tanganyika - Saleh Mbwana Mhando
KIGOMA
1. Kigoma - Samsoni Renard Anga
2. Kasulu - Col. Martin Elia Mkisi
3. Kakonko - Col. Hosea Malonda Ndagala
4. Uvinza - Mwanamvua Hoza Mlindoko
5. Buhigwe - Col. Elisha Marco Gagisti
6. Kibondo - Luis Peter Bura
KILIMANJARO
1. Siha - Onesmo Buswelu
2. Moshi - Kippi Warioba
3. Mwanga - Aaron Yeseya Mmbago
4. Rombo - Fatma Hassan Toufiq
5. Hai - Gelasius Byakanwa
6. Same - Rosemary Senyamule Sitaki
LINDI
1. Nachingwea - Rukia Akhibu Muwango
2. Ruangwa - Joseph Joseph Mkirikiti
3. Liwale - Sarah Vicent Chiwamba
4. Lindi - Shaibu Issa Ndemanga
5. Kilwa - Christopher Emil Ngubiagai
MANYARA
1. Babati - Raymond H. Mushi
2. Mbulu - Chelestion Simba M. Mofungu
3. Hanang’ - Sara Msafiri Ally
4. Kiteto - Tumaini Benson Magessa
5. Simanjiro - Zephania Adriano Chaula
MARA
1. Rorya - Simon K. Chacha
2. Serengeti - Emile Yotham Ntakamulenga
3. Bunda - Lydia Simeon Bupilipili
4. Butiama - Anarose Nyamubi
5. Tarime - Glodious Benard Luoga
6. Musoma - Dk Vicent Anney Naano
MBEYA
1. Chunya - Rehema Manase Madusa
2. Kyela - Claudia Undalusyege Kitta
3. Mbeya - William Ntinika Paul
4. Rungwe - Chalya Julius Nyangidu
5. Mbarali - Reuben Ndiza Mfune
MOROGORO
1. Gairo - Siriel Shaid Mchembe
2. Kilombero - James Mugendi Ihunyo
3. Mvomero - Mohamed Mussa Utali
4. Morogoro - Regina Reginald Chonjo
5. Ulanga - Kassema Jacob Joseph
6. Kilosa - Adam Idd Mgoyi
7. Malinyi - Majula Mateko Kasika
MTWARA
1. Newala - Aziza Ally Mangosongo
2. Nanyumbu - Joakim Wangabo
3. Mtwara - Dk Khatibu Malimi Kazungu
4. Masasi - Seleman Mzee Seleman
5. Tandahimba - Sebastian M. Walyuba
MWANZA
1. Ilemela - Dk Leonald Moses Massale
2. Kwimba - Mhandisi Mtemi Simeon
3. Sengerema - Emmanuel Enock Kipole
4. Nyamagana - Mary Tesha Onesmo
5. Magu - Hadija Rashid Nyembo
6. Ukerewe - Estomihn Fransis Chang’ah
7. Misungwi - Juma Sweda
NJOMBE
1. Njombe - Ruth Blasio Msafiri
2. Ludewa - Andrea Axwesso Tsere
3. Wanging’ombe- Ally Mohamed Kassige
4. Makete - Veronica Kessy
PWANI
1. Bagamoyo - Alhaji Majid Hemed Mwanga
2. Mkuranga - Filberto H. Sanga
3. Rufiji - Juma Abdallah Njwayo
4. Mafia - Shaibu Ahamed Nunduma
5. Kibaha - Asumpter Nsunju Mshama
6. Kisarawe - Happyness Seneda William
7. Kibiti - Gulamu Hussein Shaban Kifu
RUKWA
1. Sumbawanga - Dkt. Khalfan Boniface Haule
2. Nkasi - Said Mohamed Mtanda
3. Kalambo - Julieth Nkembanyi Binyura
RUVUMA
1. Namtumbo - Luckness Adrian Amlima
2. Mbinga - Cosmas Nyano Nshenye
3. Nyasa - Isabera Octava Chilumba
4. Tunduru - Juma Homela
5. Songea - Polet Kamando Mgema
SHINYANGA
1. Kishapu - Nyambonga Daudi Taraba
2. Kahama - Fadhili Nkulu
3. Shinyanga - Josephine Rabby Matiro
SIMIYU
1. Busega - Tano Seif Mwera
2. Maswa - Sefu Abdallah Shekalaghe
3. Bariadi - Festo Sheimu Kiswaga
4. Meatu - Dk Joseph Elieza Chilongani
5. Itilima - Benson Salehe Kilangi
SINGIDA
1. Mkalama - Jackson Jonas Masako
2. Manyoni - Mwembe Idephonce Geofrey
3. Singida - Elias Choro John Tarimo
4. Ikungi - Fikiri Avias Said
5. Iramba - Emmanuel Jumanne Luhahula
SONGWE
1. Songwe - Samwel Jeremiah
2. Ileje - Joseph Modest Mkude
3. Mbozi - Ally Masoud Maswanya
4. Momba - Juma Said Irando
TABORA
1. Nzega - Geofrey William Ngudula
2. Kaliua - Busalama Abel Yeji
3. Igunga - Mwaipopo John Gabriel
4. Sikonge - Peres Boniphace Magiri
5. Tabora - Queen Mwashinga Mlozi
6. Urambo - Angelina John Kwingwa
7. Uyui - Gabriel Simon Mnyele
TANGA
1. Tanga - Thobias Mwilapwa
2. Muheza - Mhandisi Mwanaisha Tumbo
3. Mkinga - Yona Lucas Maki
4. Pangani - Zainab Abdallah Issa
5. Handeni - Godwin Crydon Gondwe
6. Korogwe - Robert Gabriel
7. Kilindi - Sauda Salum Mtondoo
8. Lushoto - Januari Sigareti Lugangika
Habari hii imeandikwa na Halima Mlacha, Oscar Mbuza na Mroki Mroki.