Rais Dk John Magufuli akimwapisha Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi jana.
RAIS John Magufuli amewaapisha mawaziri wawili aliowateua hivi karibuni kutokana na mabadiliko madogo aliyofanya kwenye Baraza la Mawaziri baada ya kutengua uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga.
Walioapishwa ni Mwigulu Nchemba aliyehamishwa kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani, ambaye ametangaza vita dhidi ya wauza dawa za kulevya nchini.

Mwingine ni Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambaye amesema atatumia uzoefu wake kushirikiana na wataalamu kuleta mapinduzi katika kilimo.
Uhalifu, dawa za kulevya Akizungumza baada ya kiapo cha utii mbele ya Rais, Ikulu Dar es Salaam, Mwigulu alisema atahakikisha ulinzi wa raia na mali zao, unapewa kipaumbele. Akimshukuru Rais Magufuli kumwamini kwa kumhamishia kwenye wizara hiyo, alisema atapambana vilivyo dhidi ya biashara ya dawa za kulevya ambazo zinaathiri kundi kubwa la vijana nchini.
“Natoa mwito kwa wale wote wanaojihusisha na biashara hii haramu ya dawa za kulevya, umefika wakati watafute shughuli nyingine ya kufanya kwani hatutavumilia kuona vijana wetu wakiangamia,” alisema Nchemba.
Mwigulu alisema katika vita dhidi ya uhalifu, wizara ilikwishaandaa mikakati mbalimbali ya kupambana nao. Alisema uhalifu unatishia amani ya raia na mali zao, hivyo ataendeleza na kuongeza nguvu matukio hayo yakome nchini.
“Najua kuwa wizara yangu ina jukumu la kuhakikisha wananchi wanalindwa na kuwa katika hali ya usalama, hivyo nina wajibu wa kusimamia na kuhakikisha hilo linafanyika nchini,” alisema. Waziri Mwigulu alisema anaingia katika wizara hiyo akiwa na taswira ya matukio ya mauaji ya hivi karibuni.
Aliahidi kufanyia kazi matukio hayo na kuhakikisha kuwa maisha ya watu hayawi hatarini. Tizeba na kilimo Kwa upande wake, Waziri Tizeba alisema yeye ni mhusika kamili wa sekta zote zilizo chini ya wizara yake kwani ni mkulima, mfugaji na mvuvi. Alisema atahakikisha anatumia uzoefu wake, kuwezesha mapinduzi katika sekta hizo tatu.
Alisema licha ya changamoto zilizopo katika sekta hizo tatu, kwa kushirikiana na watendaji wengine wa wizara, watahakikisha asilimia 75 hadi 80 ya Watanzania wanaotegemea kilimo, wanapata mafanikio makubwa.
“Naelewa kuwa kuna changamoto nyingi katika wizara, lakini naamini tutashirikiana vya kutosha katika kukabiliana nazo na kuhakikisha kuwa uchumi wa nchi unakua kupitia sekta hizi tatu,” alisema Tizeba.
Katika Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, Dk Tizeba alikuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi. Hafla ya kuapisha mawaziri hao ilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan,Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi.
Wengine ni Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali (IGP) Ernest Mangu na maofisa waandamizi wa Polisi, Magereza na Jeshi la Zimamoto. Mawaziri hao wawili waliteuliwa hivi karibuni kutokana na nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani kuwa wazi baada ya uteuzi wa Kitwanga kutenguliwa. Hii ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza lake la Mawaziri alilolitangaza Desemba 10, mwaka jana.