Waziri Mteule wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba.
RAIS John Magufuli amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kumteua Mwigulu Nchemba kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano, Ikulu kwa vyombo vya habari, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli amefanya mabadiliko hayo madogo jana na kumteua pia Mbunge wa Buchosa, Dk Charles Tizeba kuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Tibeza anachukua nafasi ya Nchemba, ambaye alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi. Taarifa hiyo ilisema Nchemba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga ambaye uteuzi wake ulitenguliwa na Rais Magufuli. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mawaziri walioteuliwa katika mabadiliko hayo, wataapishwa kesho saa 3:00 asubuhi Ikulu jijini Dar es Salaam.
Uteuzi wa Kitwanga ulitenguliwa Mei 20, mwaka huu, kufuatia kitendo chake cha kuingia bungeni na kujibu swali linalohusu wizara yake akiwa amelewa. Taarifa ya Ikulu, iliyotolewa siku hiyo na Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa ilisema “ Rais John Magufuli ametengua uteuzi wa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Charles Kitwanga kuanzia leo tarehe 20 Mei 2016.
Rais ametengua uteuzi huo kufuatia kitendo cha Mheshimiwa Charles Kitwanga kuingia bungeni na kujibu swali linaloihusu Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa amelewa”.
Wasifu wa Mwigulu Nchemba Mwanasiasa huyu aliyebobea katika masuala ya uchumi, alizaliwa Januari 7, 1975 huko Makunda wilayani Iramba mkoani Singida. Ndiye Mbunge wa Jimbo la Iramba Magharibi mkoa wa Singida kwa tiketi ya CCM tangu mwaka 2010.
Alichaguliwa mara ya pili mwaka 2015. Aliwahi kufanya kazi kama Mchumi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kati ya mwaka 2006 hadi 2010. Historia yake kielimu Mwigulu alipata elimu ya msingi katika shule ya msingi Makunda iliyopo kata ya Kyengege tarafa ya Kinampanda wilayani Iramba (1987 – 1993), na elimu ya sekondari alipata katika shule za Ilboru, Arusha alikohitimu kidato cha nne mwaka 1997 na Mazengo mkoani Dodoma alikohitimu kidato cha sita mwaka 2000.
Alipata elimu ya juu kuanzia ngazi ya Cheti katika Taasisi ya Uongozi ya The East African katika kozi ya Utawala, na Shahada zake mbili za Uchumi alisoma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), ya Pili akihitimu mwaka 2006.
Uzoefu katika uongozi Anakabidhiwa jukumu la kuiongoza Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi akiwa ameshakomaa kiuongozi, kwani mbali ya kuwa Mbunge tangu mwaka 2010, amehamishiwa Mambo ya Ndani akitokea Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvivu.
Lakini kufikia wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, alikuwa Naibu Waziri wa Fedha na Uchumi. Kabla ya kuamua kuzama katika siasa, alikuwa Msimamizi wa Sera za Kiuchumi katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
Katika siasa, alishika nyadhifa mbalimbali kuanzia ngazi za chini, lakini kitaifa, alikuwa Mweka Hazina wa CCM mwaka 2011 hadi 2012 na baadaye aliteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM upande wa Tanzania Bara kati ya mwaka 2012 na 2015.
Katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana, Mwigulu ambaye ni baba wa watoto watatu aliobarikiwa na mkewe Neema, alijitosa kuwania kuteuliwa na CCM kuwania Urais wa Tanzania Bara uliovutia zaidi ya wanaCCM 42. Hata hivyo kura zake hazikutosha, kwani Rais wa sasa, Dk John Magufuli ndiye aliyeteuliwa kupeperusha bendera ya chama hicho.
Dk Charles Tizeba ni nani? Huyu ni Mbunge wa Buchosa mkoani Mwanza tangu mwaka 2010, aliyeingia madarakani baada ya kumng’oa aliyekuwa mshindani wake ndani ya CCM, Samuel Chitalilo. Alichaguliwa mara ya pili mwaka 2015. Dk Tizeba alizaliwa Buchosa na amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Sikonge, Tabora kwa miaka minne kati ya 2006 na 2010.
Alisoma uhandisi katika Chuo cha Ufundi Dar es Salaam (Dar Technical College, sasa Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT). Shahada ya Uzamili aliipata katika Chuo Kikuu cha Kalinin Polytechnical kilichopo Urusi ambako pia alisoma Shahada ya Uzamivu (PhD) katika Chuo Kikuu cha Ufundi Tver.
Aliingia katika Baraza la Mawaziri Mei 7, mwaka 2012 alipoteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Uchukuzi akiwa chini ya Dk Harrison Mwakyembe. Uteuzi wa Dk Tizeba (55) ulikuja baada ya Rais Jakaya Kikwete kufanya mabadiliko katika baraza lake, baada ya kuwaondoa mawaziri sita kutokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kubaini kuwa walikiuka maadili ya utumishi wa umma na kushindwa kuwajibika kisiasa kusimamia mali za umma.
Walioondolewa walikuwa Mustafa Mkulo (Fedha), William Ngeleja (Nishati na Madini), Dk Haji Mponda (Afya na Ustawi wa Jamii), Ezekiel Maige (Maliasili na Utalii), Omar Nundu (Uchukuzi) na Dk Cyril Chami (Viwanda na Biashara).
Wengine waliotemwa ni Dk Athuman Mfutakamba (Naibu Waziri wa Uchukuzi) na Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Lucy Nkya. Hivyo, Dk Tizeba alichukua nafasi ya Dk Mfutakamba, na aliendelea kushika nafasi hiyo hadi anakwenda kutetea ubunge wake katika Jimbo la Buchosa Oktoba mwaka jana.