Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameanzisha majadiliano kuhusu umuhimu wa kumwezesha mwanamke kiuchumi kwa viongozi wa nchi za Afrika, Caribbean na Pacific (ACP) wakati wa Mkutano wa Nane wa Wakuu wa Nchi hizo uliofanyika Port Moresby nchini Papua New Guinea.

Katika mkutano huo wa siku mbili uliomalizika jana, Samia alikuwa mtoa mada mkuu katika majadiliano ya kumwezesha mwanamke kiuchumi yaliyofanyika sambamba na Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.
Alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Jopo la Ngazi ya Juu la Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Kimoon lililoundwa kusaidia kufanya uchambuzi na kutoa mapendekezo ya namna ya kuchagiza kasi ya kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia Ajenda ya mwaka 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.
Jopo hilo linakusanya maoni, uzoefu na miongozo kutoka kwa wadau duniani kote kupitia majadiliano.
Aliuambia mkutano huo kuwa uwezo mkubwa walionao wanawake kama wazalishaji wakuu bado haujatumika kikamilifu kwa miongo yote katika kuchangia maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao licha ya kwamba wao ni takribani nusu ya nguvu kazi ya dunia na kama wakiwezeshwa mchango wao unaweza kufikia zaidi ya trilioni 20 ya pato la dunia.
Pia alielezea matumaini yake kwamba uchumi imara ambao unaonekana katika nchi za ACP katika miaka ya hivi karibuni utaendelea kukua na kusisitiza umuhimu wa kuondoa tofauti za kiuchumi baina ya wanawake na wanaume ili kujenga uchumi imara.
Matokeo ya majadiliano katika mkutano huo yatasaidia kushawishi kazi ya jopo hilo na kuhakikisha mtazamo wa kikanda unaingizwa katika ripoti ya kwanza itakayowasilishwa na jopo hilo kwa Katibu Mkuu wa UN, Septemba 2016.