RAIS John Magufuli amejitokeza hadharani na kuzungumzia sakata la wanafunzi wa Programu Maalumu, waliokuwa wakisoma katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na Chuo Kikuu cha St Joseph. Amesema kuwa wanafunzi hao, hawana sifa ya kupata elimu ya chuo kikuu.

Alisema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizindua Maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, inayojengwa kwa msaada wa Serikali ya China, inayoelezwa kuwa itakuwa bora zaidi barani Afrika.
Kuhusu wanafunzi hao waliofukuzwa vyuoni hivi karibuni na kuzua tafrani katika maeneo mbalimbali ikiwemo ndani ya Bunge, Rais Magufuli alisema wengi wa wanafunzi waliopata nafasi ya kusoma katika programu hiyo, walifeli mitihani ya Kidato cha Nne wakiwemo ambao walipata alama D katika masomo manne.
Akizungumzia namna programu hiyo ilivyoanza, Rais Magufuli alisema lengo lilikuwa ni kusajili wanafunzi 1,800 wenye sifa. Lakini, alisema katika mazingira ya kutatanisha walisajiliwa wanafunzi 7,802 na ambao hawana sifa, wakiwemo waliopata D nne katika mitihani ya Kidato cha Nne, jambo ambalo haliwezi kuvumiliwa.
“Walimaliza Form IV wakapata D nne wakaingia chuo kikuu. Unasajiliwa chuo kikuu na unapata mkopo wa serikali wakati umefeli! Haiwezekani… Haiwezekani… Haiwezekani,” alisema Rais Magufuli na kuongeza: “Hatuwezi kuwa na wanafunzi katika vyuo vikuu ambao wametoka Form IV wakati wapo wanafunzi waliohitimu Form Six wamekosa nafasi za kujiunga na vyuo vikuu kuchukua hata diploma halafu Form IV aliyefeli anasajiliwa!”
Alitumia fursa hiyo kumpongeza Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako kwa kuwafukuza wanafunzi hao vyuoni, Rais Magufuli alisema wanafunzi hao hawataruhusiwa kuendelea na elimu ya chuo kikuu kwa sababu walikuwa wanasoma elimu ambayo hawastahili.
Alisema kinyume cha madai ya wanasiasa kwamba wanafunzi hao ni wale walioamua kujiunga na progamu hiyo maalumu wakiwa wamefaulu kwa kupata Daraja la Kwanza na la Pili, ukweli ni kwamba wengi waliosajiliwa ni wale waliopata Daraja la Tatu na la Nne huku waliopata Daraja la Kwanza na la Pili wakiwa wachache.
“Hawa hawana hata sifa ya kusomea Diploma kwenye vyuo vikuu. Hatuna sababu ya kuwasajili huko wakati vyuo vyote 10 vya elimu havina wanafunzi wa kutosha. Serikali imeanza kuwachuja ili kuona wale wenye sifa za Divisheni 1 na 2 wanapata sehemu za kuendelea na masomo, lakini wale vilaza walioingia chuo kikuu wakati wamefeli wakatafute sehemu zinazowastahili si chuo kikuu,” alifafanua Rais Magufuli.
Akizungumzia namna serikali ilivyobaini kuwepo kwa wanafunzi hao hewa, alisema ni baada ya kutokea mgomo wa wanafunzi hao na kwamba baada ya kuchunguza alibaini uwepo wao Udom wakiwa hawana sifa.
“Nilipobaini uwepo wao nilisema hawa lazima waondoke, kama wanafunzi wa Udom nao wangeingia katika suala hili na wakagoma.. nao wangeondoka. Ni lazima tujenge misingi ya heshima ya nchi yetu. Ni lazima Watanzania tuanze kukubali ukweli, tutangulize maslahi ya Taifa letu ili lisonge mbele, tuache siasa,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu madai kwamba wanafunzi hao waliofukuzwa ni watoto wa masikini, Rais Magufuli alisema wengi wa watoto hao si watoto wa masikini, bali ni watoto wa viongozi waliotumia mbinu za kutumia mwanya huo kuingia vyuo vikuu na kupata mikopo ya serikali na kusababisha watoto wa masikini kukosa fursa hiyo. “Inashangaza wale wanasiasa failure (waliofeli) wameamua kuwatetea wanafunzi failure pia (waliofeli),” alisema Rais Magufuli.
Awali akimkaribisha Rais, Waziri Ndalichako alisema kutokana na Serikali ya Awamu ya Tano kutoa kipaumbele katika kuboresha kiwango cha elimu nchini, atafanya juu chini kusimamia lengo hilo la serikali kutokana na kukabidhiwa dhamana hiyo akiwa waziri katika sekta hiyo.
“Mheshimiwa Rais kwa vile kazi hii ya kuboresha kiwango cha elimu umenikabidhi mimi, nitaifanya kwa kiwango cha juu sana,” alisema Profesa Ndalichako ambaye mara zote akishangiliwa kwa nguvu na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Akizungumzia msaada wa Maktaba mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya China kwa msaada huo, ambao unafikia Dola za Marekani milioni 40, akizitaka nchi nyingine kujifunza kutoka China.
Alisema pamoja na kutoa msaada huo ambao utaifanya Udsm kuwa na maktaba kubwa na ya kisasa kuliko zote katika Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla, bado Serikali ya China imetoa msaada huo bila masharti yoyote.
Kuhusu changamoto za chuo hicho, Mkuu wa Chuo, Rais mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete na Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa Rwekaza Mukandala walisema changamoto kubwa ni ukosefu wa mabweni ya kuishi wanafunzi na kuomba serikali kuipatia ufumbuzi changamoto hiyo.
Akijibu Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh bilioni 10 za kuanzia ili majengo ya mabweni yajengwe ndani ya maeneo ya chuo hicho, huku akibatilisha matumizi ya Sh bilioni 1.2 zilizokuwa zinatokana na uwekezaji wa jengo maarufu la kibiashara ya Mlimani City, kuanza kuelekezwa kwenye ujenzi wa mabweni hayo.
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alieleza kushangazwa na hatua za mamlaka za Jiji la Dar es Salaam kushindwa kuwachukulia hatua kali watu wanaohujumu miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), na kuagiza watu hao kuchukuliwa hatua kali.
“Wapo ambao wamegeuza barabara zile sehemu za kujisaidia, wapo wengine ambao ingawa inakatazwa kupita wao wanapitisha magari yao, huku Mkuu wa Mkoa yupo, Mkuu wa Wilaya yupo na trafiki yupo. “Mtu kama huyu ilitakiwa kwanza gari lake likamatwe lipelekwe Polisi na akija kesho anakuta matairi yote hayapo, akiuliza mnamwambia lilikuja hivi hivi,” alisema Rais Magufuli.