Rais John Magufuli
SERIKALI imepewa mbinu kadhaa zitakazoiwezesha kushinda kesi za ufisadi zinazohusu watu wenye fedha nyingi, nyadhifa na nguvu ya kudhibiti au kupoteza ushahidi na kuonywa kuwa iwapo haitazitumia, rasilimali za Tanzania zitaendelea kutafunwa na wachache wenye ‘nafasi zao’.

Aidha, Rais John Magufuli amepongezwa kwa jitihada za kuanzisha mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi nchini, akitajwa kuwa kiongozi anayeweza kusimamia vita hiyo na kushinda kwa sababu ana sifa ya uadilifu na unyoofu ambayo kila Mtanzania anatakiwa kuwa nayo ikiwa nchi inataka kutokuwa na ufisadi.
Mbinu hizo zimetajwa kwa nyakati tofauti na wabunge mbalimbali na watoa mada kuu katika semina ya wabunge kuhusu ufisadi iliyofanyika Ukumbi wa Msekwa, ndani ya Viwanja vya Bunge mjini hapa, jana.
Semina hiyo iliandaliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ufisadi Tanzania (ACFE) na mada kuu mbili; Hali ya ufisadi nchini (Jitihada za kuuzuia, mbinu za kudhibiti mafisadi na changamoto katika kuukabili), masuala ya kisheria kwa ujumla kuhusu ufisadi. Ilitolewa na wakufunzi wa ACFE, Emmanuel Johannes na Dk Julius Mashamba.
Johannes alisema changamoto ya ufisadi ni kubwa zaidi kwenye mashirika ya umma kutokana na mfumo unaotumika kupata wakurugenzi wa bodi, watawala katika mashirika na kutokuwepo kwa uhuru kati ya bodi, wakaguzi wa ndani na watawala kutokana na njia walizopatikana.
Alisema kwa mtindo wa kupendekezana unaoendelea badala ya kutumia vigezo na sifa, taasisi na mashirika mengi ya umma yamejikuta yakishindwa kuendelea vizuri kwa ufanisi, hivyo kushauri mabadiliko kwa kuangalia uwezo, elimu na sifa nyingine muhimu.
Kwa maelezo yake, ikifanyika hivyo, mwanya wa kutokea ufisadi unakuwa ni finyu na hata mtendaji wa ngazi moja anakuwa huru kumwonya au kumkataza wa ngazi nyingine asiushiriki au kuwa tayari kutoa ushahidi katika kesi ya ufisadi pindi unapobainika katika taasisi.
Alisema kwa anayepata nafasi kwa kuzingatia vigezo hawezi kuwa na woga wa kusimamia utendaji mzuri wala upendeleo wala kuruhusu aliyempendekeza afanye ufisadi na kumfichia siri.
Dk Mashamba, Mhadhiri Mwandamizi wa Shule ya Sheria ya Dar es Salaam, alisema serikali inafungua kesi nyingi za rushwa na kushindwa kwa sababu sheria hazigusi baadhi ya vitendo viovu vinavyohusiana moja kwa moja na masuala ya rushwa.
Alisema; “Ikiwa serikali inataka kufanikiwa katika vita ya ufisadi kwa kushinda katika kesi inazozifikisha mahakamani, ni lazima sheria zinazotumika ziongezewe ‘nyama,’ ili ziguse maeneo mengine ya ufisadi ambayo kwa sasa haziyagusi.
“Pia inabidi irekebishe sheria zilizopo kuruhusu ufisadi mpya kama wa mtandao uweze kupelelezwa na kesi kuendeshwa mahakamani na kuamuliwa,” alisema na kuongeza kuwa, mambo mengine yanayopaswa kuangaliwa upya ni utitiri wa taasisi zinazoshughulikia mambo yanayofanana kama rushwa, ufisadi bila kuwa na mawasiliano. “Pia lazima serikali iweke kiwango cha chini cha elimu ya maofisa wanaopeleleza kesi za ufisadi chenye viwango vya kimataifa ili kuepusha kuwa na wasio na elimu kufanyia uchunguzi wenye elimu na ujanja wa kisheria, hivyo kushindwa kesi,” aliongeza Mashamba.
Alitaja mbinu nyingine ni kushirikisha Mahakama katika mafunzo ya kutambua ufisadi bila kuingilia uhuru wao wa kuendesha kesi na kuwasisitiza wanasheria kutotumika kupotosha ili kuficha ufisadi.
Hata hivyo, Mbunge wa Muleba Kusini (CCM), Anna Tibaijuka alisema endapo suala la uadilifu na unyoofu kwa wananchi na viongozi halitakuwepo, hata kukiwa na sheria za aina gani ufisadi hauwezi kwisha.
Alisema anampongeza Rais Magufuli kwa kupiga vita ufisadi na anaamini atafanikiwa ikiwa watu wake watakuwa wanyoofu na waadilifu kwa sababu hizo ndio sifa zake na anatembea katika njia ya uaminifu.