Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jun 3, 2016

Wapinzani wabanwa posho bungeni

Naibu Spika, Dk Tulia Ackson
WABUNGE wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ambao wamekuwa wakiingia bungeni kusaini posho na kuondoka, wako hatarini kufutiwa posho kama wataendelea kususa vikao vya Bunge kama walivyotangaza.

Hali hiyo inatokana na hoja zaidi ya mbili zilizowasilishwa kwa Spika wa Bunge kwa njia ya Mwongozo huku moja ikiwasilishwa na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe, zikikusudia kutaka Bunge kufuta posho za wabunge hao.
Akizungumza jana bungeni baada ya kuruhusiwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, Dk Mwakyembe akitumia ibara za Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na Kanuni za Kudumu za Bunge, alitaka uongozi wa Bunge kutazama upya kama wabunge hao wanastahili kulipwa posho.
Dk Mwakyembe, kwanza alitumia Ibara ya 26 ibara ndogo ya kwanza na ibara ndogo ya pili ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo aliinukuu; “Kila mtu ana wajibu wa kufuata na kutii Katiba hii na sheria za Jamhuri ya Muungano. Kila mtu ana haki, kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria, kuchukua hatua za kisheria kuhakikisha hifadhi ya Katiba na sheria za nchi.”
Baada ya hapo alinukuu tena Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 23, ibara ndogo ya kwanza na ya pili; “Kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake, na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo wao watapata malipo kulingana na kiasi na sifa za kazi wanayoifanya. Kila mtu anayefanya kazi anastahili kupata malipo ya haki.”
Kwa kuzingatia ibara hizo za Katiba, alisema kwa kutumia nafasi yake ya raia wa Tanzania na Waziri mwenye dhamana ya Katiba na Sheria, alihoji kama haki inatendeka, kulipa posho na stahiki wabunge ambao hawakuingia bungeni wala hawakuwa katika shughuli inayotambuliwa na Bunge, sawa na waliokuwa wakifanya kazi bungeni.
Alitaka Bunge lifafanue kwa kuzingatia ibara hizo za katiba kama ni haki kulipa wabunge hao wa Ukawa, wanaoingia bungeni na kusaini ili walipwe posho, kwa kubonyeza vitufe vya kielektroniki na kuingia bungeni kwa sekunde chache na kutoka kwenda kupumzika. Kuhusu wabunge waliosimamishwa kazi na Bunge, Dk Mwakyembe alihoji kama Bunge linazingatia Kanuni ya 75, ama la.
Kanuni hiyo inasema: “Mbunge aliyesimamishwa kazi atatoka katika Bunge na hataingia tena katika sehemu yoyote ya Ukumbi wa Bunge na maeneo ya Bunge kwa muda wote atakapokuwa amesimamishwa, na atalipwa nusu mshahara na nusu posho zinazoambatana na mshahara huo.”
Kabla ya Mwongozo wa Dk Mwakyembe, juzi usiku Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM) aliomba Mwongozo na aliporuhusiwa alimtaka Naibu Spika aeleze kama kitendo cha wabunge hao wa Upinzani kuingia na kukaa muda mfupi na kutoka bungeni, kinatofautiana na tatizo la wafanyakazi hewa ambao wanapigwa vita na serikali.
“Kweli Mheshimiwa Naibu Spika, serikali inawaona na wewe unawaona, hii si kuiibia serikali? Au na sisi tuanze?” Alihoji Keissy.
Mbali na Keissy, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) aliomba Mwongozo jana na kumtaka Naibu Spika kuzingatia Mwongozo wa Dk Mwakyembe na Keissy, akieleza kuwa kama si dharau kwa Bunge, kumsimamisha mtu kazi, halafu anaruhusiwa kuitisha mikutano ya kibunge jimboni.
Alimtaka Naibu Spika ambaye ni mwalimu wa sheria, akubali iletwe hoja ya kurekebisha Kanuni za Bunge ili adhabu inayotolewa kwa mbunge, imdhibiti asifanye shughuli zozote ikiwemo mikutano ya hadhara wakati wa adhabu.
Akipokea miongozo hiyo, Naibu Spika aliahidi kutolea uamuzi baadaye baada ya kufanya mashauriano huku suala la adhabu likirejeshwa kwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge.
Wabunge wa Ukawa kuanzia mwanzoni mwa wiki hii waliazimia kususa kuingia bungeni katika vipindi vyote vitakavyoongozwa na Naibu Spika, kwa madai kuwa anawaongoza kibabe kama wanafunzi na kuwa hajui uchungu wa kampeni katika majimbo.
Hata hivyo, juzi Dk aliwataka Watanzania wasikubali kupotoshwa na Kambi Rasmi ya Upinzani, iliyoamua kususa vikao anavyoviongoza, kwa kuwa kama wanaona amekosea, kuna fursa ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi wake.
Kwa upande wao, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imewasilisha kwa Ofisi ya Spika wa Bunge kusudio la kumwondoa madarakani Naibu Spika wanayemtuhumu kwa mambo sita ikiwemo upendeleo, ubabe na kufanya kazi kwa maslahi ya Serikali, badala ya umma.
Kusudio hilo la maandishi lilipelekwa katika ofisi hiyo jana na kupokelewa na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashilillah kwa niaba ya Spika, Job Ndugai ambaye hakuwepo ofisini wakati huo.
Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema) ndiye aliyewasilisha kusudio hilo kwa niaba ya kambi hiyo ya upinzani na kuzungumza na wanahabari kuhusu hatua hiyo, katika mkutano na vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Millya, mambo mengine yaliyowasukuma kuona umuhimu wa kuleta kusudio hilo kwa Spika ni unyanyasaji ambao Naibu Spika huyo anawafanyia wabunge wa kambi ya upinzani, kusimamia fedha za Mfuko wa Bunge zirudishwe kwa Rais pamoja na kukataa miongozo yao kila wakati bila sababu za msingi.
Alisema pia kuwa wameona hafai kuwepo katika kiti hicho pia kwa sababu si mwanasiasa na kwamba hana uzoefu wa kuendesha vikao vya Bunge.
Alisema, “Pamoja na kususia vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika huyo, tumekubaliana kuwasilisha kusudio hilo kwa Spika ili suala hilo lipelekwe bungeni na kujadiliwa,” alisema na kueleza kuwa wafanye hilo kwa kuzingatia Ibara ya 85 (c) Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayozungumzia hatua za kumwondoa madarakani Naibu Spika wa Bunge ikiwa kunakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
Ibara ya 85 (4) (c ) ya Katiba inasema “ Naibu Spika atakoma kuwa Naibu Spika na ataacha kiti cha Naibu Spika, litokeapo lolote kati ya mambo yafuatayo, ikiwa mtu huyo ataondolewa kwenye madaraka ya Naibu Spika kwa Azimio la Bunge”.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa ili hoja hiyo ijadiliwe bungeni, italazimika kujadiliwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
Imeandikwa na Joseph Lugendo na Namsembaeli Mduma, Dodoma
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP