Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi MwombejiKamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji.
Na Stephano Mango, RISASI MCHANGANYIKO
RUVUMA: Mwalimu wa shule ya msingi Lupapila iliyopo kata ya Subira, Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Christopher Ndimbo (29) wiki iliyopita aliporwa pikipiki yake na baadaye kuuawa kwa kukatwakatwa na mapanga na watu wanaodhaniwa kuwa majambazi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Zuberi Mwombeji, mwili wa marehemu ulikutwa katika Mtaa wa Making’inda, Kata ya Msamala mkoani hapa saa 12 jioni, Juni 14, mwaka huu ukiwa umekatwakatwa na kitu chenye ncha kali, baada ya kuwa ametoweka nyumbani kwake, Mtaa wa Mji Mwema, tangu Juni 11, mwaka huu.
Kamanda Mwombeji alisema marehemu ambaye pia alikuwa akijishughulisha na biashara ya bodaboda, alikuwa na pikipiki yake aina ya Sanlg, yenye namba za usajili MC 762 ACK  ambayo imetoweka.
“Mara ya mwisho marehemu alionekana akiwa katika maeneo ya Uhuru Pub iliyopo kandokando ya uwanja wa michezo wa Majimaji majira ya saa 2 usiku akisubiri abiria na baada ya kumpata, aliondoka kuelekea kusikojulikana,” alisema.
Kamanda alisema walianza kumtafuta marehemu baada ya mkewe, Jeska Kiswaga (22) kutoa taarifa Kituo Kikuu cha Polisi cha Songea juu ya kutoonekana kwa mumewe ndipo jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi walipofanikiwa kumkuta akiwa na majeraha makubwa kichwani na sehemu zingine za mwili.