Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu
MBUNGE wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) jana alijisalimisha Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na kauli za uchochezi alizozitoa, lakini akakosa dhamana.
Hatua ya Lissu kukosa dhamana na kulala rumande imekuja siku moja baada ya kuachiwa kwa dhamana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu anakokabiliwa na mashitaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi katika gazeti la Mawio.

Alifika kituoni hapo jana saa 7.38 mchana akiwa katika gari aina ya BMW lenye namba za usajili T549 BHH na kuhojiwa kwa saa tatu mfululizo juu ya kauli yake ya kumuita Rais John Magufuli kuwa ni dikteta ‘uchwara’, kuandika uchochezi katika mitandao ya kijamii na kutoa kauli za kuudhi.
Kwa mujibu wa Mwanasheria wa Lissu, John Mallya, kilichomfanya Lissu alale rumande ni kutokana na polisi kudai kuwa amefanya uchochezi na kutumia lugha ya kuudhi ya kusema kuna mtu anaitwa dikteta uchwara.
“Lissu amezungumza msingi wa kwa nini amesema dikteta uchwara kwenye mahojiano yake na amerekodiwa katika nyaraka za kipolisi na amehojiwa kwa saa tatu kuhusu jambo hilo, na kauli aliyosema jana kutoka mahakamani,” alisema Mallya.
Alisema wao kama wanasheria wataendelea kumpigania Lissu na kama atafikikishwa mahakamani leo watakuwepo kuhakikisha anapata haki zake zote za kisheria. Mallya alidai hakuna ujumbe wowote alioandika Lissu uliokuwa unasababisha uchochezi.
Awali, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye alikuwepo kituoni hapo, alidai hakuna jambo baya ambalo wanaona Lissu kalizungumza, bali alichokifanya ni kusema mtazamo wake kwa jinsi anavyoona.
Alisema chama hicho kitaendelea kuikosoa serikali pale kitakapoona mambo hayaendi sawa ili kuhakikisha serikali inasimama katika hali ambayo kila mmoja ataridhishwa nayo.
Juzi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Lissu aliachiwa kwa dhamana katika kesi ya inayomkabili ya mashitaka ya kuchapisha taarifa za uchochezi katika gazeti la Mawio, akijumuishwa kwenye kesi hiyo akiwa na washtakiwa wenzake ambao ni mwandishi wa habari hizo, Jabir Idrissa, Mhariri wa gazeti hilo, Simon Mkina na Mchapishaji wa Kampuni ya Jamana, Ismail Mehboob.