RAIS John Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya wapya watatu huku mmoja akiwa amebakiza muda mfupi kabla ya kula kiapo cha uadilifu, Ikulu, Dar es Salaam.
Imegundulika kuwa wawili waliteuliwa kimakosa na mmoja tayari ana wadhifa mwingine wa ubunge.

Akitoa ufafanuzi juu ya hatua hiyo Ikulu Dar es Salaam jana, wakati wa kuapisha wakuu wa mikoa wapya watatu na shughuli ya kula kiapo cha uadilifu kwa ma-DC wapya 139, Dk Magufuli alisema alitengua uteuzi wa Fikiri Avias Said kwa kuwa jina lake lilikosewa.
Alisema kwamba Mkuu wa Wilaya halali wa Ikungi mkoani Singida ni Miraji Mtaturu. Mtaturu alikuwa Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza.
Aidha, Dk Magufuli alisema ametengua uteuzi wa Fatma Toufiq kuwa Mkuu wa Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro kwa kuwa tayari mteule huyo ni Mbunge wa Viti Maalumu (CCM).
Badala yake, nafasi hiyo imezibwa na Agnes Hokororo aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kupitia chama hicho tawala. Katika Serikali ya Awamu ya Nne, Toufiq alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.
“Nilishasema katika utawala wangu, kila kazi itakuwa na mtu mmoja ili kuwe na ufanisi katika utendaji. Mtu mmoja, kazi moja,” alisisitiza Rais Magufuli akifafanua kuhusu Fatma Toufiq.
Mwingine ‘atumbuliwa’
Ikulu Kamishna wa Maadili ya Utumishi wa Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda alimtoa nje ya Ukumbi wa Ikulu kabla ya kiapo cha uadilifu mteule wa Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Emile Yotham Ntakamulenga baada ya kubainisha kuwa uteuzi wake ulikosewa na kwamba nafasi hiyo kihalali ni ya Nurdin Babu.
“Kwa heshima naomba Ntakamulenga utupishe ukumbini, haya mambo yanatokea sana, pole,” alisema Jaji Kaganda huku Ntakamulenga akitoka ukumbini hapo.
Babu alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji mkoani Pwani na amewahi kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi. Wakuu wa mikoa Wakuu wa mikoa walioapishwa ni Dk Binilith Mahenge wa mkoa wa Ruvuma, Dk Charles Mlingwa wa mkoa wa Mara na Zainab Telack wa mkoa wa Shinyanga.
JPM asema uteuzi mgumu
Aidha, Rais amesema pamoja na kwamba mchakato wa uteuzi wa wakuu wa wilaya ulikuwa mgumu, lakini amewataka viongozi hao wapya kufanya kazi bila woga na kuwaletea maendeleo wananchi.
Magufuli aliwataka wakuu hao wa wilaya katika utendaji wao, kuhakikisha kuwa wanapambana na vitendo vya rushwa, kusimamia mapato, kutatua kero za wananchi lakini pia kushirikiana na wananchi katika shughuli za maendeleo bila kutumia vibaya madaraka yao.
Alisema mchakato wa uteuzi wa wakuu wa wilaya ulikuwa mgumu kutokana na kazi kubwa ya kuwachuja, iliyozingatia sifa zao kuanzia historia, utendaji na uwajibikaji hali iliyosababisha kati ya ma-DC 139 waliokuwepo 101 kutemwa.
“Haikuwa kazi ndogo ndio maana leo mmeona ma-DC wapya ni wengi wako 100 na wengine wote 39 waliobaki ni wa zamani. Tulizingatia mengi katika uteuzi huu, niseme tu ukweli wengi tuliowaacha hawakufikia vigezo tulivyotaka,” alisisitiza Rais Magufuli.
Alisema katika uteuzi wa wakuu hao wa wilaya, w a k u r u g e n z i waliofanya vizuri pia walizingatiwa hali inayompa matumaini kwamba, timu hiyo ya ma- DC itafanya vizuri katika kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla.
Alisema kazi hiyo ni nafasi kubwa serikalini endapo itatumiwa vizuri kwa kuwajibika, kuchapa kazi, kusimamia shughuli za maendeleo, kuwa muadilifu na kupambana na rushwa kwani ndio njia nzuri ya kufikia uongozi wa juu.
Majaliwa awa mfano
“Mnamuona Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa yule ni DC mstaafu. Alitimiza wajibu wake ndio maana leo yupo hapo, nina imani kubwa na kwenu natumaini hamtoniangusha,” alisema Rais Magufuli.
Alisema amewateua kwa sababu anaamini watamwakilisha vyema kupitia utendaji wao kwa kukabiliana kikamilifu na changamoto na mateso yanayowakabili Watanzania wengi kwa sasa.
Alisema anaamini kuwa kazi ya kiongozi ni kuongoza ndio maana amewateua viongozi hao kwa kuwa anaamini wana uwezo wa kutosha huku akiwataka wajione ni wenye bahati kwani kati ya Watanzania milioni 50, wao kwa uwezo wa Mungu, ndio waliochaguliwa kushika wadhifa huo.
Alieleza kuwa pindi watakapokwenda kwenye maeneo yao, watakabiliana na matatizo mengi ya wananchi, hivyo hategemei wala kufikiria kuwa ma-DC hao ndio watakaokuwa chanzo cha matatizo katika maeneo yao.
Alisema siri kubwa ya utendaji ni kwa kumtegemea Mungu, hivyo aliwataka kumuweka kwanza Mungu mbele na kuchapaka kazi kwa kupambana na rushwa, kuzingatia maadili, haki na kuwatumikia wananchi bila kujali dini, rangi, vyama vyao au itikadi.
Kusimamia Ilani ya CCM
“Simamieni ahadi za Chama Cha Mapinduzi (CCM), tulipokuwa kwenye kampeni kuomba kura tuliahidi yale yaliyopo kwenye Ilani ya CCM. Katekelezeni haya kwa nguvu zote asitokee mtu akawakwamisha,” alisisitiza.
Alisema kisheria wakuu wa wilaya, wanayo mamlaka makubwa katika kusimamia maendeleo ikiwemo uwezo wa kumuweka ndani mtu yeyote anayewakwamisha kwa saa 24.
“Ikifikia huko wawekeni ndani ili waonje machungu ya jela lakini nawaomba msimuonee mtu, kikubwa chapeni kazi, tatueni changamoto zilizopo,” alisema.
Alisema Serikali ya Awamu ya Tano imejipanga kuwa na Tanzania mpya yenye maendeleo hivyo ni wakati wa wakuu hao wa wilaya kutumia ujuzi na uzoefu wao, kuisaidia serikali na wananchi, kutumia utajiri uliopo wa Tanzania na kuipaisha nchi kiuchumi na hivyo kuwakwamua wananchi katika lindi la umasikini.
Aidha, aliwataka ma-DC hao kuhakikisha katika maeneo yao wanawakumbusha wananchi kufanya kazi kwani kwa sasa watanzania wengi wamezoea kulalamika na kusubiri kupewa kila kitu bila kuwajibika kwa kufanya kazi.
Dk Magufuli aliwataka viongozi hao kuwa mstari wa mbele kusimamia fedha za maendeleo bila woga wala kutishiwa na wakurugenzi ambao mara nyingi huona kama fedha hizo ni zao.
“Nawaambieni hapa fedha zile ni za Serikali, zisimamieni bila woga, h a k i k i s h e n i kweli miradi inayotekelezwa inalingana na thamani ya fedha,” “Nilikuwa namuona DC wa Iringa (Richard Kasesela) alivyokuwa anabeba watoto, watu wakamsema lakini mimi nikasema huyu anabaki hapohapo. Katika kazi hii mtasemwa, mtakajeliwa, watawadhihaki lakini nawaomba mfanye kazi kwa kumtanguliza Mungu, watakaowachezea tumieni madaraka yenu,” alisema.
Kusimamia mapato
A l i s e m a kwa kuwa wao ndio wanaomwakilisha Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu, ni lazima wafanye kazi bila woga wala kusumbuliwa na mtu.” Nasema hivi tangulizeni vifua mbele na ikiwezekana hata na kichwa kitangulizeni mbele,” aliwaeleza.
Pia Magufuli aliwataka wakasimamie vyema mapato katika maeneo yao kwani kumekuwepo na baadhi ya watu wajanja wanaotumia vibaya taasisi za Serikali ikiwemo Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kujinufaisha wenyewe na kuliingizia taifa hasara.
“Tulikuwa tunafuatilia mashine za EFDs zinazokusanya mapato, yupo mtu mmoja alitengeneza kampuni nyingi zilizokuwa zikimlipa asilimia tano ya VAT na yeye anacheza na TRA halipi asilimia 18 ya kodi hiyo. Alikuwa anaingiza kati ya shilingi milioni saba mpaka nane kwa dakika. Serikali ilipoteza matrilioni ya fedha. Huyu mtu yupo kwenye mikono salama kwa sasa.”
Majaliwa, Samia wanena
Naye Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema kati ya wakuu wa wilaya walioteuliwa, wako mchanganyiko kwa maana ya vijana, wazoefu na wenye taaluma mbalimbali hali inayoashirikia utendaji mzuri.
Lakini aliwasisitizia kuwa kazi ya ukuu wa wilaya haina ujuzi wala usomi na kuwataka wote kufanya kazi kwa kusoma alama za nyakati kwani katika nafasi walizonazo kulikuwepo wateule wengine ambao wameachwa kwa kushindwa kufanya vizuri.
“Hakikisheni mnamalizia kazi ya madawati kuna mikoa imefanya vizuri lakini pia ipo iliyofanya vibaya. Nasisitiza hatutaki kusikia eneo wananchi wake wanalia njaani jukumu la DC kuhakikisha eneo lake linazalisha chakula cha kutosha,” alisema Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka viongozi hao, kabla ya kuanza kazi wahakikishe wajiridhishe kwanza kwa kuyatambua maeneo yao, kuwa karibu na Kamati za Ulinzi na Usalama na kutekeleza ipasavyo maagizo ya Rais Magufuli aliyoyatoa katika hotuba yake wakati akifungua Bunge Novemba, mwaka jana.
Aidha, alisema jukumu lake alilopewa na Rais ni kuwasimamia ma-DC hao na hivyo aliwataka kutotulia maofisini na badala yake wafanye ziara mbalimbali katika maeneo yao ili kujua vyema kero za wananchi na kuzitatua.
“Nyie si desk officers, nyie ni field officers,” alifafanua. Waonywa ulevi, ugomvi Kabla ya kuwaapisha kiapo cha uadilifu, Kamishna wa Maadili ya Utumishi wa Umma katika Sekretarieti ya Maadili ya Umma, Jaji mstaafu Salome Kaganda aliwataka viongozi hao katika kuwajibika kwao wazingatie maadili na kujiepusha na vitendo vitakavyowaharibia na kuwatia aibu kama viongozi.
Alisema uzoefu wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, unaonesha kuwa kumekuwa na matumizi mabaya ya madaraka hasa kwa viongozi wa wilaya.
“Sheria kweli inakupa mamlaka kumuweka mtu ndani, lakini sio uende ukalewe baa upigane au ugombane na watendaji wako na kumuweka mtu ndani hayo ni matumizi mabaya ya madaraka,” alisema Jaji Kaganda.
Kuhusu zawadi, alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma inatambua zawadi za kimila na imebainisha wazi kuwa zawadi inayozidi kiwango cha Sh 200,000 lazima aripoti kwa ofisa masuhuli.
“Tena hili nitalifuatilia wapo viongozi wamepewa zaidi wanakaribia kujaza mazizi lakini hawajaziripoti. Hii si zawadi hii ni rushwa ya kuwekeza,” aliwaeleza wakuu hao wa wilaya wapya.
Wakati huo huo, Rais John Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti Mwenza wa Taasisi ya Bill and Melinda Gates ya Marekani, Melinda Gates.
Rais Magufuli amemhakikishia mwenyekiti mwenza huyo kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano wake na taasisi hiyo ambayo imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya afya, uongozi na kilimo.
Kwa upande wake, Melinda Gates amempongeza Rais Magufuli kwa kazi kubwa anayoifanya katika kukabiliana na rushwa na kuongeza ukusanyaji wa mapato ya serikali, na pia kwa nia yake thabiti ya kuinua sekta ya kilimo inayotegemewa na idadi kubwa ya Watanzania na ameahidi kuwa Taasisi ya Bill and Melinda Gates itaendelea kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Tano katika kuongeza tija ya uzalishaji wa mazao ya kilimo.