Rais John Magufuli
RAIS John Magufuli amewaalika wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu la nchini China kuungana na Tanzania katika utekelezaji wa mpango wa ujenzi wa viwanda na ujenzi wa miundombinu.
Alitoa mwaliko huo Ikulu jijini Dar es Salaam jana, alipokutana na kufanya mazungumzo na Kiongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa Jimbo la Jiangsu, Luo Zhijun ambaye yupo hapa nchini akiwa na viongozi wengine wa serikali wa jimbo hilo kwa ziara ya kikazi.

Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, kwa vyombo vya habari jana, ilisema Rais Magufuli amewaalika wawekezaji hao kuja kuwekeza kwenye ujenzi wa viwanda na miundombinu na hasa reli na kuwahakikishia kuwa serikali yake ya Awamu ya Tano itatoa ushirikiano wa karibu kufanikisha uwekezaji huo.
Rais Magufuli alimweleza Zhijun kuwa serikali yake ya Awamu ya Tano, imedhamiria kuhakikisha asilimia 40 ya watanzania wanapata ajira kupitia viwanda ifikapo mwaka 2020, na ili jitihada hizo zifanikiwe inawakaribisha wafanyabiashara wa Jiangsu, kuanzisha viwanda vitakavyosindika na kuzalisha bidhaa za mazao ya kilimo na ufugaji, yakiwemo pamba, kahawa, korosho, samaki na nyama kwa kuwa malighafi zipo na pia fursa za kupanua uzalishaji wa malighafi hizo zipo.
Alimhakikishia kiongozi huyo wa Jimbo la Jiangsu ambalo lina viwanda vingi nchini China, kuwa licha ya uwekezaji wa viwanda kuinufaisha Tanzania kwa wananchi wake kupata ajira na serikali kukusanya mapato, wawekezaji wa China watanufaika na fursa ya soko kubwa la ndani ya Tanzania na nchi saba zinazoizunguka Tanzania, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zenye watu zaidi ya milioni 650.
“Mheshimiwa Luo Zhijun naomba uwaeleze wafanyabiashara wa Jimbo lako la Jiangsu kwamba ninawakaribisha kwa mikono miwili, waje hata kesho waseme wanataka kuanzisha kiwanda gani na sisi tutawapa ushirikiano,” alisema.
Rais Magufuli aliongeza kuwa, “tunayo maeneo ya kutosha ya kuanzisha viwanda kwa Pwani na Dar es Salaam tuna eneo la Bagamoyo tunaloweza kuweka viwanda zaidi ya 1,000 hali kadhalika Kigamboni na maeneo mengine mengi katika mikoa mbalimbali nchini nzima.”
Taarifa hiyo ilisema kuwa Rais Magufuli, pia alimueleza kiongozi huyo kuwa serikali yake inayakaribisha makampuni ya Jiangsu kuungana na Tanzania katika ujenzi wa miundombinu, ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kati, ambayo tayari Tanzania imetenga Sh trilioni moja kwa ajili ya kuanza ujenzi kwa kiwango cha kisasa (standard gauge) katika bajeti ijayo, ujenzi wa kilometa 1,200 za barabara ya njia sita kutoka Dar es Salaam hadi Chalinze na miradi mingine. Kwa upande wake, Kiongozi huyo wa CPC, Zhijun alimshukuru Rais Magufuli kwa utayari wake wa kuwapokea wawekezaji kutoka Jimbo la Jiangsu.
Aliahidi kuwa pamoja na kwamba Jimbo hilo tayari limewekeza hapa nchini kiasi cha dola za Marekani bilioni moja (sawa na Sh trilion 2.2), atahakikisha anawashawishi wawekezaji wengi zaidi wa viwanda katika jimbo lake kuja Tanzania haraka iwezekanavyo, kufanikisha mpango wa kujenga viwanda na kuzalisha ajira.
Balozi wa China nchini, Dk Lu Youqing aliyefuatana na Zhijun alimweleza Rais Magufuli kuwa pamoja na kuwekeza Dola bilioni moja kati ya Dola bilioni 6.62 zilizowekezwa na China hapa nchini kwa mwaka 2014/2015, wawekezaji wa jimbo la Jiangsu wanatarajia kuwekeza Dola za Marekani bilioni tano (sawa na Shilingi trilioni 11) nchini Tanzania katika miaka mitano ijayo.
Mazungumzo hayo yalihudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye juzi ametia saini makubaliano ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Mkoa wa Dar es Salaam na Jimbo la Jiangsu, ambapo jimbo hilo limeahidi kuwekeza katika miradi mbalimbali ya viwanda vya mazao ya kilimo, ujenzi na huduma za kijamii.