Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan
SERIKALI itahakikisha inalipa deni la Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) katika Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ili wagonjwa wapate dawa za saratani kwa gharama nafuu.
Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wakati alipotembelea taasisi hiyo pamoja na kumtembelea na kumjulia hali Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, Saleh Ramadhani Feruzi ambaye anapatiwa matibabu hospitalini hapo.

Alisema kwamba serikali itahakikisha inalipa deni hilo hata kama si lote ili kuwaondolea adha wagonjwa wa saratani ya kununua dawa katika maduka binafsi ambako ni ghali.
Akizungumza na baadhi ya wagonjwa ambao walimlalamikia gharama kubwa za dawa za matibabu aliahidi kuwa serikali itafanya jitihada zote ili wananchi hao wapate dawa hizo kwa gharama nafuu. “...Tutajitahidi serikali ilipe deni la MSD hata kama si lote lakini tupunguze ili wagonjwa wapate dawa kwa unafuu, kuliko kwenda kununua katika maduka binafsi basi wazipate hapa hospitali kwa bei ya unafuu,” alisema Samia.
Aidha, Samia alisema serikali itanunua mashine mbili za kisasa za mionzi kwa ajili ya taasisi hiyo ambazo zitasaidia utoaji wa matibabu kwa wagonjwa wanaofuata huduma katika taasisi hiyo.
Alisisitiza kuwa mkakati wa serikali uliopo unalenga kuhakikisha kuwa hali ya utoaji wa huduma za afya na dawa kote nchini unaimarika ili wananchi waweze kupata huduma hizo kwa ubora unaotakiwa.
Katika hatua nyingine alisema, amejionea tatizo la uhaba wa wahudumu na pia Mganga Mkuu wa taasisi hiyo amemuambia kuwa wameomba kibali cha kuajiri wahudumu wa afya 100, ambapo aliahidi kuwa serikali itahakikisha katika mwaka wa fedha 2016/2017 wahudumu wanapatikana wa kutosha.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa taasisi hiyo, Dk Diwani Msemo alisema serikali imetenga takribani Sh bilioni nane kwa ajili ya kupelekwa MSD kwa ajili ya vifaa tiba na dawa. Dk Msemo aliongeza kuwa kwa sasa, wanahudumia wagonjwa 160 kwa siku ambapo huanza kazi saa 12:00 asubuhi hadi saa 6 au 7:00 usiku.