Rais John Magufuli akiwapungia mkono wakazi wa Igunga mkoani Tabora, mara baada ya kuwahutubia wilayani hapo jana. (Picha na Ikulu).
MRADI wa kusambaza maji ya kutoka Ziwa Victoria mpaka katika miji ya mkoa wa Tabora, umepata fedha dola za Kimarekani milioni 268.35, zaidi ya Sh bilioni 500.
Rais John Magufuli, amesema hayo jana alipokuwa akizungumza na wananchi katika ziara yake katika mkoa wa Tabora, akitokea mkoa wa Singida.

Alisema fedha hizo ni mkopo kutoka nchini India na zitatumika kusambaza maji hayo katika miji ya Tabora, Igunga, Nzega, Sikonge na Uyui pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu kuanzia mwaka huu, ambapo watu zaidi ya milioni moja watanufaika.
Kabla ya kuingia mkoani Tabora, Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa mji wa Misigiri katika wilaya ya Iramba, ambapo amemuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara katika Mkoa wa Singida, kuhakikisha mkandarasi anayejenga daraja la Sibiti anarejea kazini mara moja kukamilisha ujenzi wa daraja hilo.
Rais Magufuli amesema serikali yake imejipanga kumlipa fedha mkandarasi huyo na hivyo hakuna sababu ya kuendelea kusimamisha ujenzi huo.
Mkoani Tabora, Rais Magufuli amezungumza na wananchi waliosimamisha msafara wake katika vijiji vya Nanga na Ziba na amefanya mikutano ya hadhara katika miji ya Igunga na Nzega ambako amewahakikishia wananchi kuwa serikali yake itahakikisha inatekeleza ahadi zilizopo katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya Mwaka 2015.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika Igunga, Rais Magufuli amepokea malalamiko ya wananchi kuhusu kutoanza kutumika kwa kituo cha mabasi na soko na amewaagiza viongozi wa mkoa wa Tabora, kuhakikisha kituo cha mabasi cha Igunga na soko la Igunga vinaanza kutumika kuanzia Jumatatu ijayo ya Agosti mosi, 2016.
Dk Magufuli alisema Serikali pia imefanya usanifu na upembuzi yakinifu kwa ajili ya kutekeleza mradi wa kusambaza maji ya kutoka Mto Malagarasi kwa ajili ya miji ya Urambo, Kaliua na Nguruka pamoja na vijiji vilivyopo kandokando mwa bomba kuu ambako watu laki sita watanufaika.
Aidha, Rais Magufuli amepiga marufuku wakulima wadogo kutozwa ushuru wa mazao watokapo na mazao mashambani.
“Ninapenda tukusanye kodi, lakini sio kukusanya kodi kutoka kwa watu masikini, mtu ametoka shambani na magunia yake mawili au hata matano halafu ninyi mnamtoza kodi. “Mimi sipendi kuwanyanyasa hawa watu wanyonge, mtu akiwa na mazao lori zima hapo sawa lakini sio kwa mtu mnyonge mwenye gunia moja,” alisema Rais Magufuli.
Kuhusu maombi ya mkoa wa Tabora kutaka kuanzishwa mkoa mwingine kutokana na ukubwa wa baadhi ya wilaya, Rais Magufuli alisema haoni umuhimu wa kuanzisha mikoa mipya hapa nchini kwa sasa na badala yake fedha zitaelekezwa katika huduma kwa wananchi kama vile maji, barabara, miundombinu na huduma za afya.