Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi wakijiandaa kwa kikao cha halmashauri ya chama hicho mjini Dodoma jana. (Picha na Fadhili Akida).
CHAMA Cha Mapinduzi kinatarajia kumpata Mwenyekiti mpya wa Taifa, Rais John Magufuli, katika Mkutano Mkuu wa chama hicho unaoanza leo mkoani hapa.
Tayari vikao vya Kamati Kuu (CC) na Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya CCM, vimeshapitisha kwa kauli moja jina la Rais Magufuli kugombea uenyekiti wa Taifa wa chama hicho.

Akizungumza na waandishi wa habari jana kuhusu kikao cha Nec katika Makao Makuu ya CCM jana, msemaji wa chama hicho, Christopher Ole Sendeka alisema kikao hicho baada ya kupokea jina la Rais Magufuli kutoka Kamati Kuu, kimeridhia lipelekwe katika Mkutano Mkuu.
“NEC kwa kauli moja imepokea pendekezo la Kamati Kuu na kutafakari na kupitisha jina la Rais John Magufuli, kugombea uenyekiti wa CCM na kesho (leo), jina hilo litawasilishwa kwenye Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM ili kuthibitishwa kwa kura za ‘Ndiyo”.
Katiba ya chama hicho ya mwaka 1997, inaeleza kuwa wakati wa uchaguzi unapofika, kazi mojawapo ya Nec ni kuteua jina la mwanachama atakayesimama katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa CCM na kupendekeza kwa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Katiba hiyo inasema pia kuwa unapofika wakati wa uchaguzi, kazi mojawapo ya Mkutano Mkuu wa Taifa ni kumchagua Mwenyekiti wa CCM.
Sendeka alifafanua kuwa kwa mujibu wa Katiba ya CCM, ili mtu aliyependekezwa kwa nafasi ya mwenyekiti wa CCM aweze kuchaguliwa, inabidi apate zaidi ya nusu ya kura za wajumbe wote wa Mkutano Mkuu wa Taifa.
Kampeni
Alisema kwa kuwa vikao vya juu vya Kamati Kuu na NEC ndivyo vilivyompendekeza Rais Magufuli kwenye nafasi ya uenyekiti na kwa kuwa yeye mwenyewe binafsi hakuomba, wala kujaza fomu ya nafasi hiyo, basi kazi ya kumpigia kampeni itafanywa na chama chenyewe.
“Yeye hakuomba wala kujaza fomu, bali amependekezwa na NEC hivyo chama kitamsemea. Kitapita kwa wajumbe mbalimbali na kumuombea kura,” alisema.
Sendeka alisema kwenye ukumbi wa mikutano, wajumbe wawili wa NEC ndiyo watakaomwelezea na kumuombea kura kwa wajumbe ukumbini.
Pongezi JK, aaga
Msemaji huyo wa CCM alisema NEC imempongeza Rais mstaafu, Jakaya Kikwete kwa kuongoza vizuri Taifa na chama katika kipindi chake chote na kuamua kwa hiari yake mwenyewe, kung’atuka leo kwenye uenyekiti wa chama, kumpisha Rais Magufuli ili aendeleze desturi ya CCM ya kuachiana kijiti.
Awali jana asubuhi Kikwete alipokuwa akifungua kikao cha NEC, alieleza kuwa jina la Rais Magufuli limependekezwa na Kamati Kuu iliyoketi juzi.
“Ajenda yetu leo ni moja tu. Mtapokea mapendekezo ya Kamati Kuu kuhusu Rais John Magufuli, kuwa Mwenyekiti mpya badala yangu. Ni matumaini yangu kuwa mtakubali, kama tulivyokubaliana katika Kamati Kuu na sitegemei wazo tofauti,” alisema Kikwete.
Aliwashukuru wajumbe wa NEC kwa kumpa msaada na ushirikiano mkubwa katika kipindi chote alichokuwa Mwenyekiti wa chama, baada ya kuchaguliwa kushika nafasi hiyo mwaka 2006.
“Naomba muendelee kumpa ushirikiano na msaada Mwenyekiti mpya Rais John Magufuli,” alisema Kikwete na kumdokeza mwenyekiti huyo mtarajiwa kuwa; “Ndugu Rais utakuwa Mwenyekiti. Kuna wakati kikao hiki cha Nec kinakuwa kigumu, lakini inabidi ukiendeshe tu”.
Akimkaribisha Kikwete, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema idadi ya wajumbe wa NEC waliotakiwa kuhudhuria kikao hicho ni 374, waliohudhuria ni 365 sawa na asilimia 97.5, hivyo akidi imetimia.
Kung’atuka leo
Kikwete alisema kikao hicho cha NEC ni cha kihistoria kwa namna mbili. Kwanza ni kikao chake cha mwisho kuhudhuria na kama atakuja kwenye kikao kingine, atakuwa amealikwa. “Nikija kwenye NEC mtakuwa mmenialika,” alisema.
Jambo la pili ni huko nyuma viongozi wa juu wastaafu, waliendelea kuhudhuria vikao vyote vya Kamati Kuu na NEC, wakiwa wajumbe wa kudumu. Hata hivyo, anasema miaka ya hivi karibuni, baadhi ya viongozi hao wastaafu, walisema wametumikia chama vya kutosha; hivyo wangependa kupumzika badala kuhangaika na kukaa kwenye vikao hivyo vya Kamati Kuu na NEC mara nyingine hadi saa 7:00 usiku.
Alimtaja mmojawapo wa waliotoa msimamo huo wa kutaka wazee wapumzike na waitwe pale inapobidi, kuwa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
“Lakini sisi tukasema hatutawaacha. Tukawaambia tutawaundia Baraza la Ushauri la Wazee,” alisema Kikwete na baadaye waliwaundia wazee hao Baraza la Ushauri. Baada ya hatua hiyo, Kikwete alisema yalizuka maneno mengi, ambapo baadhi ya watu walidai Kikwete hawataki wazee na ndiyo maana amewaengua katika vikao vya Kamati Kuu na NEC.
Alisema walijitahidi kueleza ukweli wa suala hilo na likaeleweka. “Kesho (leo) namaliza. Kesho (leo) ni mwisho kabisa. Nitahudhuria vikao pale nitakapohitajika kama wazee wengine wa CCM,” alisema.
Alifafanua kuwa wazee wastaafu wanahudhuria vikao pale wanapohitajika, kwa mfano kunapokuwa na masuala mazito yanayohusu chama na uhai wake; au kwa mfano vikao vya uchaguzi mkuu wa mwaka jana, ambapo chama kilipita katika msukosuko mkubwa.
Msukosuko
Kuhusu msukosuko wa mwaka jana, alisema kulikuwa na mijadala mikali katika vikao hivyo vya Kamati Kuu na NEC; na ilifikia mahali watu walikuwa wakiimba nyimbo wanazofahamu wao kwenye ukumbi huo wa NEC.
“Lakini maadam CCM haikuvunjika katika Uchaguzi Mkuu huo wa mwaka jana, kamwe haitavunjika tena. Katika uchaguzi huo wa mwaka jana, kuna mafisi yalikuwa yamekaa yanasubiri mkono udondoke yatafune, kwa bahati nzuri hilo halikutokea, kwani hakuna mkono uliodondoka na chama kilibaki imara na kinaendelea kuwa imara,” alisema.
Kikwete alisema kuna gazeti moja liliandika hivi karibuni eti CCM itaishia mwaka 2020, lakini alisisitiza kuwa CCM haitang’oka ng’o. Alifafanua kuwa CCM haitang’oka kwa kutumia nguvu, kwa sababu inafanya mambo yake kwa umakini mkubwa na kwa kuzingatia mahitaji na changamoto za wananchi.
Alisema Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, zina mipango mizuri na zinajitahidi kuitekeleza kwa ajili ya kuimarisha uchumi na maendeleo ya taifa.
Wafitini
Akieleza propaganda za wafitini, Kikwete alisema kuna gazeti lingine liliandika hivi karibuni kuwa “Uteuzi wa Magufuli kupingwa NEC”. Alisema habari hiyo ni potofu, kwa sababu hakuna kitu kama hicho na hakikutokea; na kwamba walioiandika, inaonesha wana mtambo wa kufyatua uongo.
“Kuna watu wana viwanda na mitambo ya kufyatua uongo. Hawa wanazalisha bidhaa mpya zenye uongo na uzushi kila siku,” alisema.
Aidha, alisema wapo watu hawalali na wana taabu mno, wanapoona CCM ina nguvu na inaendelea kuwa imara. Alisisitiza kuwa CCM haibabaishwi na uongo na uzushi wa watu hao; kwani mara zote kama kuna jambo ndani ya CCM, hupelekwa katika vikao husika, kisha hujadiliwa na kufikia maafikiano.
Rais Magufuli anakuwa Mwenyekiti wa Tano wa Taifa wa Chama, ambapo wa kwanza alikuwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliyefuatiwa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Kikwete.
Wajumbe karibu wote wa Mkutano Mkuu huo maalumu, wameshawasili mjini hapa pamoja na wageni waalikwa.
MAGUFULI NI NANI?
Dk Magufuli alizaliwa tarehe 29 Oktoba 1959 wilayani Chato mkoani Kagera (sasa Mkoa mpya wa Geita). Alianza elimu ya msingi katika Shule ya Msingi Chato wilayani Chato mwaka 1967 na kuhitimu mwaka 1974. Alijiunga na Shule ya Seminari Katoke wilayani Biharamulo, ambako alisoma Kidato cha Kwanza na cha Pili mwaka 1975 – 1977.
Alihamishiwa Shule ya Sekondari Lake mkoani Mwanza, ambako alisoma kidato cha Tatu na Nne mwaka 1977 - 1978. Masomo ya Kidato cha Tano na Sita alipata Shule ya Sekondari Mkwawa mkoani Iringa kati ya mwaka 1979 na 1981.
Baadaye alirudi Chuo cha Ualimu Mkwawa kusomea Stashahada ya Elimu ya Sayansi katika masomo ya Kemia, Hisabati na Elimu. Alisoma hapo mwaka 1981 – 1982. Baada ya kuhitimu hapo, alianza kazi ya ualimu katika Shule ya Sekondari Sengerema mkoani Geita, akifundisha masomo ya Kemia na Hisabati kati ya mwaka 1982 na 1983.
Baadaye alijiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria akianzia Makutupora, Dodoma (Julai - Desemba 1983), kisha kambi ya Makuyuni mkoani Arusha (Januari hadi Machi 1984) na akamalizia kambi ya Mpwapwa mkoani Dodoma (Machi – Juni 1984).
Mwaka 1985 alijiunga Chuo Kikuu cha Dar es Salaam akisomea Shahada ya Sayansi ya Elimu akibobea kwenye masomo ya Kemia na Hisabati na alihitimu mwaka 1988. Mwaka 1989 - 1995 alifanya kazi katika Kiwanda cha Nyanza Co-operative Union (Ltd.) akiwa Mkemia na wakati huohuo alianza masomo ya Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Chuo Kikuu cha Salford nchini Uingereza, kikishirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ambako alisoma kati ya mwaka 1991 na 1994.
Magufuli aliendelea na elimu ya juu zaidi kwa maana ya Shahada ya Uzamivu ya Kemia kuanzia mwaka 2000 hadi 2009, ambayo aliihitimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na kuwa mhitimu wa Shahada ya Udaktari. Dk Magufuli ana mke na watoto kadhaa.
Dk Magufuli alichaguliwa kuwa mbunge wa Chato mwaka 1995, na aliposhinda Rais Benjamin Mkapa alimteua kuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Miundombinu. Katika uchaguzi wa mwaka 2000, Dk Magufuli aligombea na kushinda kwa mara ya pili. Rais Mkapa alimteua kuwa Waziri wa Miundombinu .
Mwaka 2005 alichaguliwa kuwa mbunge kwa kipindi cha tatu na Rais Jakaya Kikwete alimteua kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hadi mwaka 2008, alipohamishiwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, ambayo aliiongoza hadi mwaka 2010.
Mwaka 2010 alifanikiwa kuchaguliwa kuwa mbunge kwa mara ya nne na Rais Kikwete alimrudisha katika Wizara ya Ujenzi, ambayo aliiongoza hadi 2015. Oktoba mwaka 2015 alichaguliwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano.