Mwanamuziki mashuhuri kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amekamatwa akiwa nyumbani kwake mjini Kinshasa.
Mwandishi wa BBC Poly Muzalia anasema mwanamuziki huyo amekamatwa kwa agizo la afisi ya mwendesha mashtaka.

Olomide alitimuliwa kutoka nchini Kenya baada ya video kuonekana kuonesha akimpiga teke mchezaji ngoma wa kike katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta mapema asubuhi baada yake kuwasili.
Alipangiwa kutumbuiza mashabiki wake Bomas of Kenya siku ya Jumamosi lakini tamasha hiyo ikaahirishwa.
Alikamatwa Ijumaa usiku na maafisa wa polisi wa Kenya na siku iliyofuata asubuhi akaingizwa kwenye ndege na kurejeshwa Kinshasa.
Waandalizi wa tamasha ambayo Olomide alipangiwa kutumbuiza nchini Zambia pia walitangaza kwamba wamefutilia mbali hafla hiyo kutokana na yaliyotokea Nairobi.
Mwanamuziki huyo, akiandika kwenye ukurasa wake wa Facebook Jumapili, aliomba radhi mashabiki wake na hasa “wanawake na watoto”.
“Najutia sana yaliyotokea… kilikuwa ni kipindi kifupi cha wenda wazimu,” aliambia kituo cha tevisheni cha taifa cha RTNC.
Baadaye, aliomba msamaha kutoka kwa raia wote wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao huenda alihisi kwamba tabia yake iliwakosea heshima.
Waziri wa masuala ya vijana na jinsia Kenya Bi Sicily Kariuki, katika taarifa kwa vyombo vya habari baada ya video iliyoonesha tukio hilo kusambaa, alipendekeza Olomide azuiwe daima kuzuru Kenya.
“Vitendo vyake ni matusi kwa Wakenya na Katiba yetu,” alisema kupitia taarifa.