Rais John Magufuli
WAKUU wa wilaya wateule, wameahidi kuchapa kazi kwa uadilifu, kuzingatia haki na maadili ikiwa ni pamoja na kutekeleza maagizo yote waliyopatiwa na Rais John Magufuli.
Waliyasema hayo Ikulu Dar es Salaam juzi wakati wa hafla ya kuapishwa wakuu wa mikoa wapya watatu na shughuli ya kula kiapo cha uadilifu wakuu wa wilaya wapya 139.

Mkuu wa Wilaya mteule wa Kasulu, Kanali Martin Mkisi aliahidi kufanya kazi kadri ya uwezo wake na kuzingatia uadilifu ili kuwaletea maendeleo wananchi wa Kasulu iliyopo mpakani kwa Tanzania na Burundi inayokabiliwa na matatizo ya wakimbizi, uhamiaji haramu na ujambazi.
Alisema katika utendaji wake, atatoa kipaumbele katika suala la ulinzi na usalama kwa kushirikiana na Kamati ya Ulinzi na Usalama.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Salum Happi pamoja na kushukuru kwa kuaminiwa tena kwa mara ya pili na kutakiwa kuendelea katika nafasi yake hiyo, pia ameahidi kuendelea kuzifanyia kazi changamoto zinazoikabili wilaya hiyo ambayo awali alikabidhiwa kuiongoza miezi miwili iliyopita.
Sarah Chiwamba, Mkuu wa Wilaya mteule wa Liwale, amemshukuru Rais kwa kumuamini na kumteua kuwa mwakilishi wake katika wilaya hiyo iliyopo mkoani Lindi na kuahidi kuitumikia nafasi yake ya ukuu wa wilaya kwa uadilifu.
Mkuu wa Wilaya mteule wa Handeni, Godwin Gondwe alianza kwa kuwashukuru na kuwapongeza wanahabari wote nchini kwa uteuzi wake na kusisitiza kuwa, kuaminiwa kwake na Rais Magufuli ni ishara tosha kuwa kiongozi huyo wa nchi, anaikubali na kuiamini tasnia ya habari.
Alisema anafahamu kuwa Serikali ya Awamu ya Tano imejikita katika kuinua maisha ya mwananchi wa chini, jambo ambalo atalitekeleza kwa vitendo huku akiahidi kutomuangusha Rais wala wanahabari wenzake.
Kwa upande wake, Mkuu wa wilaya mteule wa Kaliua, Busalama Yeji alisema kwa kuwa maagizo na maelekezo mengi yanalenga Ilani ya CCM na ahadi zilizotolewa katika kampeni za uchaguzi mwaka jana, atahakikisha anatekeleza wajibu wake kama anavyotakiwa.
Naye Mkuu wa Wilaya mteule wa Kilolo, Asia Abdallah alimshukuru Rais Magufuli kwa kumteua, lakini pia kumpeleka katika wilaya hiyo ya Kilolo aliyobainisha kuwa maisha ya huko ni sawa kabisa na maisha aliyoishi.
Mwishoni mwa wiki, Dk Magufuli aliwateua wakuu wa wilaya wapya 139, kati yao 78 wakiwa ni wapya kabisa, 39 wanaoendelea na 22 waliokuwa wakurugenzi katika halmashauri mbalimbali waliofanya vizuri.
Tayari wakuu hao wa wilaya wamekula kiapo cha uadilifu kupitia Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma juzi ambapo pia wakuu wa mikoa watatu ambao ni Dk Binilith Mahenge (Ruvuma), Dk Charles Mlingwa (Mara) na Zainab Telack (Shinyanga).