Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika
MATUSI na kusema uongo bungeni kumesababisha wabunge watatu wa Chadema kufungiwa kuhudhuria vikao 20 vya Bunge.
Wabunge waliofungiwa kuhudhuria vikao hivyo ni Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi maarufu Sugu, Mbunge wa Ubungo, Said Kubenea na wa Simanjiro, James Millya.

Wakati Mbilinyi amefungiwa vikao 10 kwa kuonesha ishara ya matusi, Millya na Kubenea wamefungiwa vikao vitano kila mmoja kwa kusema uongo.
Akizungumzia shauri la Mbilinyi, Mwenyekiti wa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, George Mkuchika alisema kitendo cha Mbilinyi cha kuonesha kidole chake cha kati cha mkono wa kulia juu huku akiwa amekunja vidole vingine, kumefedhehesha Bunge, wabunge na wananchi kwa ujumla.
Aidha, alisema Mbilinyi akiwa mbunge mzoefu, kitendo chake hicho kinatafsiriwa kuwa ni kudharau mamlaka ya Spika.
Mkuchika alisema baada ya kamati yake kupokea malalamiko ya kutoka Spika, kufuatia miongozo iliyoombwa na Mbunge Jacqueline Msongozi na Sixtus Mapunda kwamba Mbilinyi alitoa ishara ya matusi bungeni, iliketi Juni 19, mwaka huu na kufanya uchunguzi washauri hilo.
Baada ya kuita mashahidi katika shauri hilo, kuangalia mikanda ya video bungeni na kumhoji Mbilinyi, kamati ilibaini kwamba Mbilinyi alikuwa amekiuka masharti ya kifungu cha 24 (d) na (e) cha sheria ya Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge na Kanuni ya 74 (1) (a) na (b).
Mkuchika alisema kwamba Mbilinyi alipohojiwa, alikiri kuonesha kidole cha kati cha mkono wake wa kulia, akielekeza kwa juu huku vidole vingine akiwa amekunja kutokana na hasira ya kile alichodai iliyotokana na kuudhiwa na matusi, aliyorushiwa na mtu asiyemfahamu wakati akitoka bungeni.
Mbilinyi alidai kuwa mtu huyo alimtusi mama yake, matusi ya nguoni, jambo lililomkasirisha na kutoa ishara hiyo.
Hata hivyo, alisema hamjui aliyemtusi. Mkuchika alisema katika kukata shauri hilo, pia walijihoji kama ishara hiyo ina maana gani na hivyo pamoja na kuangalia maana katika utamaduni wa Tanzania, pia walipitia kitabu cha The Definitive Book of Body Language kilichoandikwa na Allan and Barbana Peace na kubaini kwamba ishara hiyo ni ya matusi.
Mbilinyi anadaiwa kutoa ishara hiyo ya matusi Juni 6, 2016 wakati akitoka nje ya Bunge baada ya kuwasilisha taarifa ya kambi ya upinzani bungeni kuhusu Azimio la Bunge la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Udhibiti wa Matumizi ya Dawa na Mbinu za Kuongeza Nguvu Michezoni.
Kitendo chake hicho, kilionwa na wabunge Msongozi na Mapunda ambao waliomba mwongozo wa spika.
Naye Naibu Spika Tulia Ackson akizungumzia mashauri ya Kubenea na Millya alisema Kamati ya Maadili imewaona watu hao kuwa na makosa ya kusema uongo bungeni baada ya wao kushindwa kuthibitisha madai yao, waliyoyatoa dhidi ya mawaziri Dk Hussein Ali Mwinyi na Jenista Mhagama.
Ilielezwa na Naibu Spika kwamba Said Kubenea wakati akitoa mchango wake kwenye hotuba ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, alidai kuwa Waziri Dk Mwinyi ameingia mkataba na kampuni ya ujenzi wa China, ambayo itajenga nyumba za jeshi pamoja na nyumba yake binafsi.
Naibu Spika alisema kauli hiyo ililalamikiwa na Waziri Mwinyi kwamba ni taarifa za uongo na kutaka mchangiaji kuthibitisha.
Pamoja na kutakiwa na Naibu Spika kuondoa maneno yake, Kubenea alikataa na alipotakiwa kutoa maelezo yake kwa maandishi katika siku nne alifanya hivyo, lakini alishindwa kuthibitisha maneno yake hayo kwenye kamati na hivyo kuonwa kwamba amesema uongo.
Katika shauri la Millya, Naibu Spika alisema mbunge huyo wa Simanjiro alishindwa kuthibitisha kauli yake kwamba Martin Mhagama ana undugu na Waziri Jenista Mhagama, baada ya kutoa madai hayo bungeni kwamba zabuni kwa Kampuni ya Sky Associates ilitokana na ushemeji uliopo na Waziri Mhagama na Martin Mhagama.
Kauli hiyo ilipingwa na Waziri Mhagama aliyesema kuwa hana undugu na kuomba mwongozo wa Spika wa kutaka Millya kuthibitisha au aadhibiwe kwa kusema uongo. Adhabu za wabunge wote hao, zinaanza kutekelezwa kuanzia Juni 30, mwaka huu.