Rais John Magufuli
AMIRI Jeshi Mkuu, Rais John Magufuli atakuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Siku ya Mashujaa Kitaifa, yatakayofanyika mjini hapa leo.
Hiyo itakuwa ni mara ya kwanza kwa maadhimisho hayo kufanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, tangu Tanzania ipate Uhuru wake mwaka 1961. Pia, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Rais Magufuli kuongoza maadhimisho hayo tangu alipochaguliwa Oktoba mwaka jana.

"Maadhimisho ya Siku ya Kumbukumbu ya Mashujaa yatafanyika kitaifa mkoani Dodoma katika Uwanja wa Mashujaa siku ya Jumatatu (leo) Julai 25, 2016 kuanzia saa 1 kamili asubuhi hadi saa 4:30 asubuhi. “Mgeni rasmi atakuwa Rais John Magufuli," alisema Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, kwenye mkutano wake na waandishi wa habari, jana.
Alisema anaishukuru serikali kwa kuupatia mkoa huo, ambao ni Makao Makuu ya nchi, heshima ya kipekee katika historia ya nchi ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo kitaifa.
Rugimbana alitaja shughuli zitakazofanyika siku hiyo kuwa ni gwaride la maombolezo litakaloshirikisha vikosi vya majeshi ya ulinzi na usalama vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Polisi na Magereza.
Kutakuwa pia na upigaji mizinga na uwekaji wa silaha za asili na shada la maua kwenye mnara, kama ishara ya kumbukumbu kwa mashujaa. Shughuli nyingine ni utoaji wa dua na sala, utakaofanywa na viongozi wa madhehebu ya dini.
Rugimbana aliwataka wakazi wa Dodoma kujitokeza kwa wingi siku hiyo kwenye Viwanja vya Mashujaa kushiriki kwenye maadhimisho hayo. Alisema hadi jana, maandalizi yote muhimu kwa ajili ya shughuli hiyo yalikuwa yamekamilika.