Follow us: Subscribe via RSS Feed Connect on YouTube Connect on YouTube
Maganga One Blog kwa habari za kitaifa,kimataifa,burudani na michezo kila siku. Tutumie habari na matukio yoyote kwa email yetu ya magangaone@gmail.com

Jul 25, 2016

Safari ya nchi kuhamia Dodoma yaanza rasmi

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana
SIKU moja baada ya Rais John Magufuli kutangaza Serikali kuhamia Dodoma ifikapo 2020, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana amesema tayari mkoa huo umejipanga kufanikisha azma hiyo ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Pamoja na Mkuu huyo wa Mkoa, pia wasomi kadhaa wamempongeza Rais Magufuli kwa kuonesha dhamira ya kutimiza ndoto ya muda mrefu ya kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma na kusisitiza hatua hiyo, itajenga zaidi umoja wa kitaifa.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu jana, Rugimbana alisema tayari mkoa huo wa Dodoma umeainisha mikakati ya kufanikisha azma hiyo ikiwemo kutenga maeneo kwa ajili ya huduma mbalimbali.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni eneo la Ihumwa ambalo ni maalumu kwa ajili ya kujenga nyumba za Serikali zikiwamo wizara na makazi ya watumishi wa Serikali.
Alisema kabla ya Rais Magufuli kutangaza rasmi azma ya kuhamishia Serikali Dodoma, tayari Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa agizo la mkoa huo wa Dodoma kutenga eneo la bandari kavu na kituo cha biashara.
Alisema bandari kavu itakuwa inahudumia mikoa inayoizunguka Dodoma na hivyo kuiongozea uwezo Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kupunguziwa kwa kiasi kikubwa msongamano wa bidhaa na makontena.
Aidha alisema Serikali ya Mkoa wa Dodoma inaendelea kujipanga kupanua huduma za kijamii kama vile afya na elimu ili kukabiliana na ongezeko la watu watakaohamia katika mkoa huo.
“Tunatarajia pindi serikali itakapohamia hapa, kutakuwa na ongezeko kubwa la mahitaji ya afya lakini pia elimu kwani kutakuwa na idadi kubwa ya wanafunzi. Hili nalo tumeanza kulifanyia kazi,” alisema Rugimbana.
Hata hivyo, Rugimbana alisema japokuwa mkoa huo unajiandaa kupokea Serikali haizuii wizara na taasisi za Serikali kuhamia mkoani humo na kuendelea kutumia vituo na wizara zilizopo wakati wakisubiri eneo rasmi kukamilika.
“Namhakikishia Rais na serikali yake kwa ujumla, mkoa umejipanga kikamilifu katika kutekeleza hili na ndani ya miaka mitano litakuwa limekamilika,” alisisitiza Rugimbana.
Tayari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama amebainisha kuwa serikali imeanza kutengeneza sheria ya kutambulisha Dodoma kama Makao Makuu ya nchi na inatarajiwa kupelekwa bungeni ili kuondoa changamoto ya migogoro baina ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na wananchi.
Alisema kuanzishwa kwa sheria hiyo kutarahisisha kuhamia Dodoma pamoja na kuondoa migongano ya kisheria kati ya taasisi mbalimbali inayosimamia masuala ya ardhi mkoani Dodoma, ikiwa ni pamoja na kueleza mipaka ya CDA.
Alisema watahakikisha migogoro yote inaisha kwa kufuata sheria na maridhiano kwa kuwapatia wananchi haki, na pale sheria inapowataka wananchi waipe haki serikali waoneshe ushirikiano. Waziri huyo alisema mji wa Dodoma utajengwa kisasa na kuonesha kweli ni makao makuu kama ilivyo miji mingine duniani kwa kuwa kioo cha nchi ilivyo.
Wasomi waeleza utekelezaji wake
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Benson Bana, alisema kauli ya Rais Magufuli katika Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM juzi, imedhihirisha azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuhakikisha serikali yote inahamia Dodoma kwa gharama yoyote.
Alisema suala hilo limeanza kuzungumziwa tangu miaka 40 iliyopita na marais mbalimbali walionesha dhamira ya kulitekeleza bila mafanikio. Hata hivyo alisema Serikali ya Awamu ya Tano imeanza kuonesha kwa vitendo utekelezaji wa suala hilo, kwani tayari hatua kadhaa zimeanza kuchukuliwa kwa ajili ya kufanikisha lengo hilo.
“Nampongeza Dk Magufuli ameonesha ni Rais wa vitendo na nina imani hili litafanikiwa. Hakuna sababu ya watu kutohamia Dodoma wengi hasa watendaji hawapendi hili kwa kuwa wanahofia kupoteza fursa ya kupata viposho lakini ki ukweli kuhamia Dodoma kutasaidia Serikali kubana matumizi,” alisisitiza Bana.
Alisema kwa sasa serikali inapoteza fedha nyingi kugharimia watendaji wanaohudhuria shughuli za serikali zinazofanyikia Dodoma ikiwemo Bunge, kwa kulipia mafuta ya magari yao, posho za kujikimu na malazi.
Dk Bana alisema endapo Serikali yote itahamia Dodoma, hata mji wa Dar es Salaam utaweza kutengenezwa na kuwa mji mkubwa wa kibiashara, majengo ya Serikali ya sasa yatapangishwa na kuiingizia serikali fedha nyingi.
Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally alisema kuna faida nyingi za kuhamishia serikali Dodoma, mojawapo ikiwa ni upungufu wa usalama jijini Dar es Salaam kutokana na msongamano wa watu na miundombinu mibovu.
Alisema wazo la kuifanya Dodoma Mji Mkuu wa Tanzania lilipitishwa kama Azimio mwaka 1970 na Tanganyika African National Union (TANU) lengo likiwa ni kuutumia mji huo ulio katikati ya Tanzania kuwa kituo cha kuhudumia Watanzania wote.
Alisema endapo serikali itahamishiwa Dodoma, itatoa fursa kwa Watanzania kutoka pande zote nchini kupata huduma za Serikali bila kusafiri umbali mrefu hadi Dar es Salaam kama ilivyo sasa.
“Niseme wazi kati ya mambo ambayo Dk Magufuli ameyazungumza jana hili la kuhamia Dodoma limenifurahisha sana kwani linaonesha dhamira ya kujenga utaifa. Ninaomba serikali ijipange kutekeleza agizo hili kikamilifu, lakini pia mji wa Dodoma ujengwe kwa tahadhari na kuepuka yanayotokea sasa Dar es Salaam,” alisema Ally.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Edwin Ngonyani, alisema kwa sasa miundombinu ya Dodoma iko tayari kuipokea serikali yote isipokuwa kama itahitajika marekebisho zaidi.
Alisema katika kufanikisha azma hiyo ya kuhamia Dodoma, wizara yake imeanza mchakato wa upanuzi wa uwanja wa ndege ili kuwezesha ndege kubwa zaidi kutua. “Mji huu tayari una master plan yake na utakuwa unaendelezwa kwa kufuata mpango huo,” alisisitiza Ngonyani.
Naye Mbunge wa Dodoma Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Anthony Mavunde, alimpongeza Dk Magufuli kwa hatua yake hiyo ambayo inatekeleza ahadi aliyoitoa katika kampeni.
“Wakati wa kampeni moja ya ahadi nilizotoa ni kuhamisha serikali Dodoma, nimefurahi sana na ninajisikia faraja kuona ahadi yangu imeanza kutekelezwa. Ni kweli suala hili ni la miaka mingi, lakini kupitia Serikali hii ya Awamu ya Tano naamini sasa litatekelezeka kwa vitendo,” alisema Mavunde.
Aliwataka wafanyabiashara na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kutumia fursa hiyo na kuwekeza zaidi katika mji huo wa Dodoma ambao ndio Mji Mkuu wa Tanzania.
Juzi mara baada ya kukabidhiwa kijiti cha uenyekiti wa CCM Taifa, Dk Magufuli pamoja na mambo mengine alitangaza rasmi kuwa kabla ya kumaliza kipindi chake cha miaka mitano, serikali yote itakuwa imeshahamia Dodoma.
Alisema pamoja na miundombinu ya Dodoma sasa kuwezesha serikali kuhamia huko, yeye mwenyewe atakuwa mfano kwa kuhamia Ikulu ya Chamwino ambayo ina kila hitaji analotaka huku akisisitiza anatarajia Makamu wa Rais, Waziri Mkuu, Mawaziri na serikal 
Share this article :

0 Maoni:

 
Maganga One Blog © Copyright 2017. All Rights Reserved.

Powered by Maganga One.
Back to TOP