Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
UPANDE wa Jamhuri katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 14 inayowakabili wafanyabiashara wawili, leo unatarajiwa kujibu hoja za upande wa utetezi ulioiomba mahakama iwafutie washitakiwa shitaka la utakatishaji fedha.
Washitakiwa katika kesi hiyo ni mfanyabiashara Mohamed Yusufali “Choma”, aliyewahi kutajwa kuwa anajipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu kutoka katika mapato ya serikali, na Mkurugenzi wa kampuni ya Northern Engineering Works Ltd, Samwel Lema.

Washitakiwa walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, juzi na kusomewa mashitaka 222 ya kughushi stakabadhi za malipo pamoja na nyaraka za kodi ya ongezeko la thamani (VAT) , utakatishaji fedha na kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 14.
Baada ya kusomewa mashitaka, upande wa utetezi ukiongozwa na Wakili Alex Mgongolwa uliiomba mahakama ifute shitaka la utakatishaji fedha kwa kuwa lina mapungufu makubwa ya kisheria ambayo hayawezi kurekebishwa wala kufumbiwa macho isipokuwa kufutwa.
Alidai ili shitaka liwe la utakatishaji wa fedha lazima kuwa na dhamira ya kuficha chanzo cha fedha au lengo la washitakiwa kukwepa adhabu lakini kama hakuna mambo hayo sheria inatoa mamlaka kwa mahakama kuyafuta mashitaka hayo.
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo ili wajiandae kujibu hoja za upande wa utetezi. Hakimu Mashauri alipanga leo upande wa jamhuri uwasilishe majibu ya ombi hilo.