Reli ya kisasa
MCHAKATO wa ujenzi wa mradi mkubwa wa Reli ya Kati nchini kwa kiwango cha kisasa ‘Standard Gauge’, umeanza rasmi baada ya Serikali ya Tanzania kusaini mkataba wa ushirikiano (MoU) na Benki ya Exim ya China.
Mkataba huo ulisainiwa jana katika ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dk Servacius Likwelile na Naibu Meneja wa Kitengo cha Mikopo Nafuu wa Benki hiyo, Zhu Ying.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba huo wa ujenzi wa kilometa 2,190 za reli, Dk Likwelile alisema mkataba huo ni makubaliano ya pamoja ya matayarisho mbalimbali, ikiwemo kupata sehemu ya fedha za ujenzi huo na kugawana majukumu ya kila mmoja.
Alisema katika kufikia malengo waliyojiwekea, ikiwemo ya ushirikiano katika kuleta mapinduzi ya viwanda, kutaundwa kikosi kazi cha pamoja, kwa ajili ya kushughulikia masuala ya miradi mbalimbali inayofadhiliwa na benki hiyo.
Miongoni mwa mambo yatakayoshughulikiwa na kikosi kazi hicho, alisema ni pamoja na kuandaa mradi kwa kuangalia masuala ya kiutawala na kiufundi na kusimamia kufanyika kwa upembuzi yakinifu na kufungua fursa mbalimbali.
Dk Likwelile alisema mradi huo mpaka utakapokamilika, unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh trilioni 16, ambapo reli hiyo ya kiwango cha kisasa (Standard Gauge), itatoka Dar es Salaam – Tabora –Isaka – Mwanza; Tabora – Mpanda –Kalemela; Tabora – Uvinza – Kigoma na Isaka – Keza – Msongati.
Alitaja njia mpya zilizopendekezwa kuwa ni Isaka-Keza –Kigali (Rwanda) nyingine ni Isaka-Keza-Gitega (Burundi ); Mpanda-Karema, Uvinza –Musongoti; Mtwara-Songea-Mbambabay mpaka Liganga na Mchuchuma na Arusha-Musoma.
Awali, Rais wa Benki ya Exim ya China, Liu Liang alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais John Magufuli, alikubali benki hiyo kuchangia katika ujenzi wa reli iyo ya kisasa ikiwa ni pamoja na kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ujenzi na uendeshaji wa reli.
Katika mazungumzo hayo Rais Magufuli alisema mradi huo utagawanywa vipande kwa wakandarasi wanne hadi watano, kwa lengo la kuharakisha ujenzi huo na tayari utaratibu wa kupata wakandarasi hao toka nchini China umeanza.
Alisema serikali imetenga katika bajeti ya mwaka huu Sh trilioni moja kwa ajili ya ujenzi wa reli hiyo, ambapo Rais Magufuli alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo utasaidia kuinua uchumi wa Tanzania na nchi jirani zisizopakana na Bahari ya Hindi, ikiwemo Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).