Watu tisa wameuawa na wengine 10 kujeruhiwa baada ya watu wenye bunduki waliowafyatulia risasi watu katika jumba moja la kibiashara mjini Munich, Ujerumani.
Polisi wanasema washukiwa bado hawajakamatwa na wamewatahadharisha watu na kuwashauri kutotoka nje.
Wanachunguza iwapo mmoja wa waliofariki ni mtuhumiwa.

Image copyright

Operesheni kubwa ya kiusalama inaendelea katika jumba la kibiashara la Olympia, ambalo linapatikana mtaa wa Moosach, kaskazini magharibi mwa Munich.
Watu walioshuhudia tukio wanasema wamewaona watu watatu waliokuwa na bunduki.

Image copyrightEPA

Maafisa wa polisi jimbo la Bavaria wamekuwa katika hali ya tahadhari tangu Jumatatu kijana mhamiaji alipowadunga visu na kuwajeruhi watu kadha katika treni, shambulio ambalo kundi la Islamic State lilidai kuhusika.
Polisi wamesema shambulio hilo ni la kigaidi.
Wanasema habari za kwanza kuhusu ufyatuaji wa risasi kwenye jumba hilo linalopatikana katika barabara ya Hanauer zilitokea muda mfupi kabla ya saa thenashara jioni.
Kituo kikuu cha treni katika mji huo wa Bavaria kimefungwa na watu kuondolewa.

Image copyrightEPA

Watu wengi wamekwama kutokana na kustishwa kwa uchukuzi na kutokana na hali kwamba hawawezi kusafiri kurudi nyumbani, wanapewa malazi ya wenyeji.
Kumeanzishwa kampeni kwenye Twitter inayotumia kitambulisha mada#Offenetür(fungua mlango).
Helikopta za maafisa wa polisi zinapaa angani na maafisa maalum wa usalama wanashiriki katika operesheni kubwa ya kuwasaka watuhumiwa.
Kituo cha redio cha serikali ya Bavaria kimesema kikosi maalum cha polisi wa mpakani kwa jina, GSG9, kinaelekea Munich kikitumia helikopta kadha.


Waziri mkuu wa Bavaria Horst Seehofer anaongoza mkutano wa dharura na washauri wa masuala ya usalama.
Jamhuri ya Czech, inayopakana na Ujerumani imeimarisha usalama mpakani.