DAR ES SALAAM: Yule mchungaji aliyejitokeza hivi karibuni kumuombea muigizaji wa sinema za Kibongo, Wema Sepetu, Daudi Mashimo, amedaiwa kuvurumishiwa matusi na mama wa staa huyo, Mariam Sepetu alipokuwa akimpigia simu kumuombea.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mchungaji huyo anayeongoza kondoo katika Huduma ya Injili ya Maumivu na Uponyaji iliyopo Mbezi-Msakuzi jijini Dar, anadaiwa kukutwa na dhahama hiyo hivi karibuni ambapo pasipo kuelewa sababu, alijikuta akilowa mvua ya matusi.
“Mchungaji baada ya kumuombea Wema kanisani kwake, alipewa namba ya simu ya mama Wema ili aweze kuzungumza naye kama mzazi kuhusu kumhimiza mwanaye afanye maombi. Sasa bahati mbaya siku alipompigia mama Wema alikuwa hajisikii vizuri.
“Akamuangushia maombi, mama Wema akashukuru na wakawa wanaendelea kuwasiliana. Sasa kuna siku mchungaji akampigia mama Wema, ghafla akashangaa anaporomoshewa matusi.Wema na Mama yake
“Inadaiwa mama Wema alisikia kuwa, mchungaji huyo amekuwa akimchoresha kwa waandishi wa habari kila anapozungumza naye anawaambia waandishi. Siku moja aliongea naye, walipomaliza, akapigiwa simu na waandishi na kuulizwa jambo waliloongea na mchungaji huyo, ndipo akaona kumbe anamchoresha, ndiyo maana akamshushia matusi,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Kama unavyomjua tena mama Wema ni mtu wa kampa… kampa tena. Alimpa mazimamazima, mchungaji mwenyewe akawa mpole.”
Baada ya Amani kumegewa ubuyu huo, lilimtafuta bi mkubwa huyo ili kumuuliza kulikoni hadi afikie hatua ya kumporomoshea matusi mtumishi huyo wa Mungu ambapo alipopatikana, alisema hamfahamu mchungaji huyo na hajui anataka nini kwake.
“Mimi simjui huyo mchungaji, atakuwa anatafuta kiki kupitia jina langu. Kwanza hata aliposema anamuombea mwanangu, alisikia ni mgumba? Hana lolote huyo! Sijui namba yangu ya simu aliipata wapi, akawa ananipigiapigia simu,” alisema mama Wema.
Kwa upande wake, mchungaji Mashimo alipotafutwa na Amani, alishtuka na kudai analishughulikia suala hilo kiroho zaidi.
“Nyinyi hilo suala mmelisikia wapi? Tambueni tu nalishughulikia kiroho hivyo nisingependa kulizungumzia kwa kirefu kwa sasa kwani Mungu ni mwema sana kwetu,” alisema mchungaji huyo.
Imelda Mtema, Amani
0 Comments